Serikali kuongeza mikopo ya wanafunzi wa stashahada

Dodoma. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imejipanga kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati vinavyotoa stashahada lengo ni kuongeza idadi ya wataalamu.

Utoaji wa mikopo katika ngazi za stashahada kwa wanafunzi wa ngazi hiyo ya elimu ulianza mwaka 2023/24, kwa fani sita za kipaumbele ambazo zina uhitaji mkubwa wa wataalamu ambazo ni afya na sayansi shirikishi, ualimu wa hisabati.

Fani nyingine ni fizikia na mafunzo ya amali, uhandisi na nishati, madini na sayansi ya ardhi, kilimo na mifugo ambapo Sh48 bilioni zilitengwa kwa ajili ya wanafunzi 8,000.

Akizungumza leo Jumanne Aprili 29,2025 wakati wa kufungua mkutano mkuu wa Shirika la Mtetezi wa Mama, Profesa Mkenda amesema Serikali ya awamu ya sita, imefanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu ikiwamo ya kutoa mikopo kwa ngazi ya stashahada.

Amesema katika kuzalisha vijana wenye ujuzi, Serikali iliamua kuanza kutoa mikopo ngazi ya stashahada kwa kozi za kipaumbele na mpango wa sasa ni kuongeza wigo wa kozi zitakazonufaika na mpango huo.

Aidha, Profesa Mkenda amesema pia Serikali imewezesha maboresho ya sera na mtalaa ambayo imeelekeza kuwa elimu ya lazima kuwa miaka 10 badala ya saba, na kurejesha elimu ya kujitegemea kupitia mafunzo ya amali.

Amesema pia Serikali imesogeza elimu ya juu kwa kuhakikisha mikoa ambayo haikuwa na vyuo vikuu inajengewa kampasi za vyuo hivyo.

Mkenda amesema pia Serikali imehakikisha wilaya zisizokuwa na Vyuo vya Ufundi (Veta) vinajengewa vyuo hivyo na kwa sasa 64 zinajengwa ngazi ya wilaya.

“Naungana na ninyi katika kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu na mnaposema mitano kwa Rais Samia nawaelewa sana,” amesema.

Aidha, Profesa Mkenda amehimiza Watanzania kuendelea kudumisha mshikamano na umoja.

 Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mtetezi wa Mama, Neema Karume  amesema lengo la umoja huo ni kumwinua mwanamke katika nyanja ya uchumi pamoja na vijana kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu nchi.

“Mheshimiwa waziri hawa ni wapiga kura ambao wapo bega kwa bega na mama lengo ni kuhakikisha anapata kura za kutosha katika uchaguzi mkuu,” amesema Karume.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *