Serikali kununua ndege maalumu za utafiti wa madini

Chunya. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa kununua wa ndege yenye vifaa maalumu vya kufanyia tafiti za kina maeneo ya madini na shughuli za uchimbaji nchini. 

Amesema tayari kuna mradi kupitia Umoja wa Ulaya (EU) kushirikiana na nchi ya Hispania wa kurusha ndege kwenye eneo lenye ukubwa kilomita za mraba 165,874 sawa na asilimia 18 ya nchi nzima ya Tanzania.

Mkakati huo umetajwa kunufaisha mikoa mbalimbali nchini ikiwepo mikoa ya Songwe na Mbeya hususani wilaya ya kimadini ya Chunya, eneo la Lupa ambako kuna miamba mikubwa ya madini ya dhahabu.

Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 3, 2025 akiwa katika ziara Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya na kuzindua mradi mpya wa uchimbaji wa madini ya dhahabu wa Kampuni ya Shanta Gold Limited katika Kijiji cha Mkola kilichopo Kata ya Saza.

“Nimesikia maombi ya wakuu wa wilaya za Songwe na Chunya kutaka tafiti zifanywe ili kuwezesha serikali kuongeza mapato, nakubaliana nanyi hatuwezi kuendeleza sekta ya madini pasipo tafiti na ndio maana tulijenga hoja kwa Rais Samia Suluhu Hassan atuongezee bajeti,” amesema.

Waziri wa madini, Antony Mavunde akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mgodi wa uchimbaji madini wa kampuni ya Shanta wilayani chunya mkoani hapa. Picha na Hawa Mathias

Amesema ili kufikia malengo ya kukuza sekta ya madini nchini Serikali imetenga bajeti kwa mwaka huu wa fedha kununua ndege yenye vifaa maalumu vya kufanya tafiti za kina.

“Sekta ya madini imeleta manufaa makubwa nchini ambapo kwa mwaka fedha 2022/23 iliongoza kuingizia serikalini fedha nyingi za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa zaidi ya Dola za Marekani 3.6 bilioni sawa na asilimia 56,” amesema.

Kwa upande wa makusanyo ya kodi  imechangia  Sh2.1 trilioni , sawa na  asilimia 15, kutoka  vituo vya ununuzi 102 na masoko 44 ,  huku  Sh 700 bilioni zilikusanywa.

“Ndio maana Wizara imekuja na mikakati ifikapo mwaka 2030 kufikia asilimia 50 ya tafiti mbalimbali za kina ili kuleta manufaa kwa serikali, wawekezaji na wananchi hususani wachimbaji wadogo,” amesema.

Amesema ili kufikia malengo, tayari kuna mradi unahusisha Serikali, Umoja wa Ulaya (EU) kwa kushirikiana na nchi ya Hispania wa kurusha ndege eneo lenye ukubwa kilomita za mraba 165,874.

Waziri wa madini Antony Mavunde akikagua eneo la uwekezaji wa shughuli za uchimbaji wa madini wa kampuni ya Shanta (katikati mwenye shati la kitenge) Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mbaraka Batenga. Picha na Hawa Mathias

“Mradi huo utafanywa maeneo mbalimbali nchini hususani Wilaya ya Songwe na Chunya maeneo la Lupa ambako kuna miamba mikubwa ya madini ya dhahabu,” amesema Mavunde.

Mavunde ameipongeza Kampuni Shanta kwa uwekezaji wenye tija na kufunguwa mgodi huo, hali ambayo italeta tija ya kuchangia uchumi wa kipato na ajira kwa wananchi wa mikoa ya Mbeya na Songwe.

Kuhusu uchangiaji wa mapato kwenye mfuko mkuu wa Serikali, Mavunde amesema kwa mwaka 2015/16, Sh162 bilioni ziliingizwa, huku mwaka 2025 kiwango kilipanda na kufikia Sh753 bilioni na matarajio ni kufikia Sh1 trilioni kwa mwaka huu wa fedha.

Amesema hatua hiyo imefanya ongezeko la makusanyo kitaifa kutoka asilimia 7.2 mpaka asilimia 9, huku wakiwa wamejiwekea mikakati kufikia asilimia 10.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga ameomba wizara kubariki maeneo ya uchimbaji na miamba kufanyiwe tafiti za kina ili kuvutia wawekezaji na wachimbaji wadogo waweze kunufaika.

Batenga amesema katika kuhakikisha sekta ya madini inaendelezwa na kuchangia mapato serikalini, tayari vitalu 1,500 ambavyo havijaendelezwa vitatolewa kwa wachimbaji wadogo wa madini wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itinda ameipongeza sekta ya madini kwa usimamizi mzuri na kwamba shughuli za uchimbaji wilayani humo zinachangia Sh100 bilioni kwa kila mwaka.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni Shanta, Honest Mrema amesema wametenga Dola 5.0 milioni, sawa na Sh12.6 bilioni kwa ajili ya kufanya utafiti wa madini katika maeneo ya Lupa, huku asilimia 80 wakitumia leseni mpya zilizotolewa na Wizara.

Mrema amesema tangu kuanza shughuli za uchimbaji wamewekeza zaidi ya Sh900 bilioni sambamba na kuchangia Sh812 bilioni serikalini  kama kodi na tozo mbalimbali.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Kaimu katibu Tawala, Dk Elizabeth Nyema amesema kama Serikali wataendelea kushirikiana na wawekezaji ili kuona sekta ya madini inafanya vizuri.

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wachimbaji madini, Alex Mwaisaka ameomba Kampuni ya Shanta kuwa sehemu ya kuwainua kwa kutoa elimu ya matumuzi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za uchimbaji ili kuchangia mapato ya Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *