Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema Serikali itashirikiana na Kanisa Katoriki kumsaidia mtoto wa marehemu Wande Mbiti (38), aliyeuawa nyumbani kwake na kufungiwa mlango kwa nje.
Marehemu Wande alikutwa amefariki dunia Machi 02, 2025 huku mlango wa nyumba yake ukiwa umefungwa na kufuli kwa nje.
Wande alibainika amefariki baada ya majirani kuhisi harufu kali kutoka nyumbani kwa marehemu na kuchukua hatua za kubomoa mlango.
Mwanamke huyo ameacha mtoto, Everine Moses anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Montessory, hivyo Kanisa Katoliki limebeba jukumu la kumsomesha, litashirikiana na Serikali kuhakikisha anafikia malengo yake.

Wananchi wakijenga kaburi la Wande Mbiti (38), aliyeuawa nyumbani kwake na kufungiwa mlango kwa nje.
Mtatiro alikwenda nyumbani kwa marehemu jana Machi 03, 2025 katika kitongoji cha Busalala kilichopo katika Kijiji cha Nheleghani, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na kueleza kusikitishwa na tukio hilo la kinyama.
“Serikali itashirikiana na Kanisa Katoliki ili kuhakikisha mtoto huyu (Everine) anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Montesory. Atapata mahitaji yake yote muhimu, tutakuwa tunawasiliana na Kanisa Katoliki kujua kama kuna hitaji lolote, ili tusaidiane,” amesema.
Mmoja wa wananchi katika eneo hilo, Annastazia John ameeleza kuwa walikuwa na takriban siku tano hawajamuona Wande na mlango wake ulikuwa umefungwa, wakajua hayupo.
“Tulivyokuwa hatujamuona na mlango wake umefungwa kwa nje tukajua amesafiri, kumbe alikuwa ndani. Kwa ufupi, tuliishi naye vizuri na alikuwa anashirikiana vizuri na jamii inayomzunguka,” amesema Annastazia.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kennedy Mgani alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na uchunguzi wa awali unaonyesha hakuna dalili zozote kuonyesha kuwa marehemu aliuawa.
“Kutokana na uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa hakuna kitendo chochote cha ukatili alichofanyiwa marehemu na baada ya hapo tuliruhusu baba mzazi akishirikiana na wananchi kumsitiri Wande maana mwili ulikuwa umeharibika sana,” amesema Mgani.