Serikali ivalie njuga migogoro ya ardhi

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameeleza namna migogoro ya ardhi nchini inavyokuwa sehemu ya kiini cha makosa mengi ya jinai, jambo ambalo linailazimu Serikali kuivalia njuga na kuitokomeza nchini.

Bahati nzuri, kauli ya Jaji mkuu ameitoa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria, na hivyo ujumbe huo umefika kwa mtu sahihi.

Vilevile, ujumbe huo umetolewa na mhimili wa pili wa dola, baada ya Novemba 1, 2013 Bunge la Jamhuri kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza chanzo cha migogoro ya ardhi nchini na kuja na mapendekezo kibao na hatua za kuchukua, lakini hali ikabaki ni ileile.

Jaji mkuu katika hotuba yake, amemweleza Rais kuwa iwapo suala la ardhi litawekwa vizuri, litasaidia kutatua matatizo mengi na mahakama itakuwa na migogoro michache, baada ya mingi kuishia kwenye usuluhishi kuliko hali ilivyo sasa.

Inapendeza kuona suala hili linamulikwa na Jaji Mkuu na kuliwekea uzito unaostahili, kuliko ambavyo limekuwa linatazamwa na watu wengine.

Hata ukitazama hukumu na maamuzi madogo kupitia tovuti ya mahakama, migogoro ya ardhi inachukua sehemu ya mashauri yote baada ya yale ya jinai.

Hakuna ubishi kuwa migogoro ya ardhi imekuwa ikisababisha mauaji kutokana na baadhi ya wahusika kuchukua sheria mkononi.

Migogoro hiyo pia imehusishwa na mauaji baina ya wakulima na wafugaji katika mikoa yenye makundi hayo ya wakazi, ambao ama wanagombea eneo la malisho au kilimo.

Si jambo la ajabu tena kusikia taarifa za mauaji baina ya ndugu wa damu au watoto na wazazi, na ukifuatilia kiini unabaini miongoni mwa sababu ni kugombea mipaka ya mashamba, viwanja au mashamba yaliyoachwa na wazazi.

Mathalani, katika kliniki ya wiki moja ya ushauri wa kisheria iliyoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) iliyomalizika Januari 27, 2025 katika mkoa wa Kilimanjaro, asilimia 80 ya waliohudhuria, migogoro yao ilihusu ardhi.

Migogoro hiyo ni pamoja na familia ya mke na watoto kudhulumiwa viwanja, nyumba au mashamba baada ya mume kufariki dunia na unakuta familia inahangaika miaka nenda rudi katika vyombo vya maamuzi kudai haki.

Ipo migogoro mingine ya ardhi imekuwa ikisababishwa na baadhi ya watendaji katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi au ofisi za ardhi za halmashauri na imekuwa ikiifanya Serikali kushitakiwa kortini.

Katika kliniki hiyo ya ushauri wa sheria, ilielezwa kuwa ofisi ya AG imekuwa ikipokea notisi zaidi ya 500 za kuishtaki Serikali, na ukitizama kesi hizi baadhi zinasababishwa na makosa ya watendaji katika kutoa hatimiliki za viwanja.

Ndiyo maana tunaamini kauli ya Jaji Mkuu imetolewa wakati, mahali na kwa kiongozi sahihi wa Serikali, na kwa maana hiyo sasa ni wakati mwafaka wa Serikali kuivalia njuga migogoro ya ardhi iliyotapakaa kila kona ya nchi.

Sisi tunadhani, ifike mahali kama wasababishaji wa migogoro hii ya ardhi, hasa watendaji katika ofisi zetu za umma – idara ya ardhi au ofisi ya msajili wa hati au viongozi wa vijiji na mitaa wawe wanaadhibiwa badala ya kuhamishwa maeneo ya kazi.

Kuendelea kufumbia macho tatizo hilo ni sawa na kukalia bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote.