Serikali itafute mbadala fedha za ARVs

Amri ya Rais wa Marekani, Donald Trump kusitisha usambazaji wa dawa za Virusi vya Ukimwi (VVU), Kifua Kikuu (TB) na Malaria, Tanzania imejiandaa vipi kukabiliana na hatua hiyo? Hilo ni jambo muhimu linalohitaji kufanyiwa kazi na mamlaka husika.

Hivi karibuni, Trump alisaini amri ya kuiondoa nchi yake katika Shirika la Afya Duniani (WHO), siku chache tu baada ya kuingia madarakani, jambo ambalo limezua taharuki miongoni mwa Watanzania, hususan katika mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanywa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) mwaka 2023, takribani Watanzania milioni 1.5 wanaishi na Virusi vya Ukimwi, huku asilimia 80 ya maambukizi ikiwa kwenye kundi la vijana, hususan wenye umri wa miaka 15 hadi 24.

Aidha, mwanzoni mwa miaka ya 1980, watu walipoteza maisha kutokana na kukosa kinga na tiba ya maambukizi haya, lakini baadaye mwanzoni mwa miaka ya 2000, dawa za kupunguza makali ya Ukimwi ziliingia nchini, hali ilianza kuboreka zaidi baada ya Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuanzisha mipango ya kutoa elimu na uelewa kwa jamii kuhusu ugonjwa huu.

Katika miaka hiyo, dawa kama ARVs (Antiretroviral drugs) zilianza kutolewa kwa watu wanaoishi na VVU. Hatua hiyo ilisaidia kuboresha maisha ya wengi, japo kulikuwa na changamoto kadhaa kama vile uelewa mdogo, upatikanaji wa dawa ulikuwa mgumu maeneo ya vijijini, unyanyapaa, rasilimali fedha kuwa changamoto kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali na mifumo ya afya ilikuwa changamoto katika kutoa huduma.

Lakini pamoja na hayo, Serikali ya Tanzania ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto zilizojitokeza wakati dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi zilipoanzishwa kama vile uhamasishaji ili kuongeza uelewa kuhusu Ukimwi, upanuzi wa huduma za afya, mpango wa kusaidia kifedha, kujenga uwezo wa wafanyakazi wa afya na kukabiliana na unyanyapaa.

Matokeo ya hatua zilizochukuliwa na Serikali yalikuwa mazuri kwa kiasi kikubwa. Kwanza, upatikanaji wa dawa za ARVs uliongezeka, na hivyo kuwasaidia watu wengi wanaoishi na VVU. Hii ilichangia katika kupunguza vifo vinavyohusiana na Ukimwi na kuboresha maisha ya watu wengi.

Pili, elimu na uhamasishaji kuhusu Ukimwi na dawa zake uliboresha uelewa wa jamii, na hivyo kupunguza unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi. Hali hii ilichangia katika kuimarisha ushirikiano kati ya waathirika na jamii zao.

Hatimaye, kuimarika kwa huduma za afya na mafunzo kwa wafanyakazi wa afya kulisaidia kutoa huduma bora zaidi, hivyo kuongeza ufanisi katika matibabu ya Ukimwi. Kwa jumla, hatua hizo zilileta mabadiliko chanya katika kukabiliana na changamoto za Ukimwi hapa Tanzania.

Hata hivyo, mambo yameanza kwenda kombo mwaka huu baada ya Trump kuingia madarakani. Alitoa amri ya kusitisha utoaji wa misaada iliyokuwa ikiwasaidia maelfu ya watu waishio na VVU hapa Tanzania na kwingineko duniani.

Watu wengi wameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu athari za uamuzi huo, wakihisi kuwa msaada huo ni muhimu katika kuendeleza mapambano dhidi ya ugonjwa huo na mengine katika bara la Afrika.

Kupitia mitandao ya kijamii kama vile X, baadhi ya watu wanaeleza kuwa hatua ya Marekani kijiondoa WHO inaweza kuathiri upatikanaji wa dawa za ARVs na huduma za afya, hivyo kuleta madhara makubwa kwa watu wanaoishi na VVU.

Baadhi wanahamasisha umuhimu wa kuendelea kwa msaada wa kimataifa ili kusaidia nchi kama Tanzania katika kukabiliana na changamoto za Ukimwi. Hata hivyo, ni nafasi muhimu kwa Serikali kubeba jukumu la kulinda afya za wananchi kwa kuhakikisha kwamba dawa hizo zinaendelea kupatikana.

Kwa mtazamo wangu, kusitishwa kwa msaada huo kunaweza kuwa na athari kubwa kwa jamii na mfumo wa afya. Ni muhimu kuhakikisha kwamba dawa za ARVs zinaendelea kupatikana kwa watu wanaoishi na VVU.

Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kutafuta vyanzo vingine vya mapato ya kufadhili manunuzi ya dawa hizo ili kuzuia ukosefu wa matibabu, kuongeza elimu kuhusu Ukimwi katika jamii.