
Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya mauaji inayomkabili Fred Chaula (56) na wenzake wawili bado haujakamilika, mahakama imeelezwa.
Mbali na Fred Chaula, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Bashir Chaula (49), dereva bodaboda na mkazi wa Tegeta, pamoja na Denis Mhwaga, mkazi wa Iringa. Watatu hao wanakabiliwa na shtaka la mauaji ya Regina Chaula (62), ambaye ni ndugu yao.
Leo Alhamisi, Machi 27, 2025, kesi hiyo ilipotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wakili wa Serikali Tumaini Mafuru alieleza kuwa upelelezi bado unaendelea, hivyo akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Rahim Mushi, upande wa mashtaka uliwasilisha ombi hilo, ambalo mahakama ililikubali na kupanga kesi hiyo kutajwa tena Aprili 3, 2025.
Kesi hiyo imesikilizwa kwa njia ya video, huku washtakiwa wakiwa rumande kutokana na shtaka la mauaji linalowakabili kutokuwa na dhamana kisheria.
Kwa mara ya kwanza, watuhumiwa walifikishwa mahakamani hapo Machi 12, 2025, ambapo walitajwa kwa shtaka hilo.
Kwa mujibu wa mashtaka, Januari 18, 2025, katika eneo la Bahari Beach, wilaya ya Kinondoni, watuhumiwa walimuua Regina Chaula na kisha mwili wake kuutupa kwenye shimo la maji machafu lililopo ndani ya nyumba ya marehemu, wakifahamu kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria.