Serikali: Abiria wengi hawajui haki zao

Dodoma. Serikali imekiri kuwa, abiria wengi wanaotumia usafiri wa vyombo vya moto, hawajui haki zao.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumanne Aprili 22, 2025 na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ambaye pia ametoa onyo kwa wasimamizi wa mizigo kwa treni ya mwendo kasi akiwataka kuwa makini ili kuepusha malalamiko ya abiria.

Kihenzile alikuwa akijibu swali la msingi na maswali ya nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest ambaye ametaka kujua, nini haki za abiria wa vyombo vya moto nchini na kwa kiwango gani wanatambua haki zao.

Mbunge huyo amehoji ni namna gani Serikali inafuatilia na kusimamia kero kubwa ambayo imekuwa ikiwapata watumiaji wa treni mpya ya SGR ambao wanalalamika kuhusu utozwaji wa gharama kubwa kwenye mizigo hata ile midogo.

Naibu Waziri amesema abiria anayesafiri kwenye basi la njia ndefu (mikoani na nchi jirani), basi la mjini (daladala), teksi, pikipiki za magurudumu mawili au matatu, treni, ndege na meli ana haki ya usalama wa chombo na mazingira salama.

Amesema pia abiria wana haki ya kuchagua chombo cha usafiri, haki ya kulipwa fidia pale anapostahili kama akipata majanga, haki ya kusikilizwa na kuelimishwa, haki ya kupewa tiketi na kufikishwa mwisho wa safari yake.

“Pamoja na jitihada za Serikali, kupitia mabaraza ya watumiaji wa huduma za usafiri wa ardhini na anga (LATRA CCC na TCAA CCC), bado uelewa wa watumiaji wa huduma hizi juu ya haki zao bado uko chini kutokana tabia ya watumiaji kutopenda kufuatilia maelekezo au matangazo mbalimbali yanayowalenga (Consumer apathy),” amesema Kihenzile.

Amesema Serikali kupitia taasisi husika itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya haki za abiria ili kila mmoja aweze kutambua haki zake na kuzitumia inapobidi.

Katika hatua nyingine Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko amelalamikia treni ya SGR kwamba abiria wanaotumia usafiri huo wanapoteza haki zao hasa inapotokea wamekata tiketi lakini wakapata dharura hawawezi kurudishiwa fedha zao akataka kujua ni kwa nini inakuwa hivyo.

Mwenyekiti wa Bunge, Dk Joseph Mhagama amesema jambo hilo linawatia hasara watumiaji wengi kutokana na kushindwa kurudishiwa nauli zao na kulazimisha kukata tiketi upya.

Naibu Waziri Kihenzile amesema jambo hilo nalo wanalichukua na kwenda kulifanyia kazi kisha watatoa majibu ya namna inavyopaswa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *