
Ligi Kuu nchini Italia ‘Seria A’ inazidi kuwa ya aina yake ambapo mpaka sasa timu inayoongoza Ligi ni Napoli yenye pointi 26 ikitofautiana pointi mbili na Juventus inayoshika nafasi ya sita.
Tukiwa tunaeleka kwenye mapumziko ya kupisha kalenda ya kimataifa ya FIFA (FIFA international break) Napoli inaongoza Ligi kwa pointi 26 tofauti ya pointi moja dhidi ya timu nne zinazofuata kwenye msimamo ambazo ni Atalanta, Fiorentina, Inter Milan na Lazio zote zina alama sawa 25. Na Juventus ipo nafasi ya sita ikiwa na alama 24.
Bingwa mtetezi Inter Milan wana kibarua cha kuutetea ubingwa, ambapo ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 25, ikiwa imeshinda michezo saba, ikipata sare nne, na imefungwa mchezo mmoja.
Mateo Retegui wa Atalanta ndiye anayeongoza kufunga akiwa na mabao 11 kwenye mechi 12 alizocheza huku akimuacha kwa mabao sita aliyekuwa mfungaji bora msimu uliyopita Lautaro Martinez mwenye mabao matano.
Ligi ya Seria A, itaendelea tena Novemba 23 baada ya mapumziko ya timu za taifa ambapo itachezwa michezo mitatu kati ya Verona watakao kuwa nyumbani kukabiliana dhidi ya Inter Milan, AC Milan dhidi ya Juventus wakati Parma itakuwa nyumbani kuwakaribisha Atalanta.