Serengeti. Ili kuendelea kuwavutia watalii wa ndani na nje ya Tanzania, Hifadhi za Taifa za Serengeti na Tarangire zinakusudia kuanzisha vivutio vipya, ikiwemo utalii wa usiku na kuwabainisha tembo wanaozaa pacha.
Lengo la hatua hiyo ni kuwafanya watu mbalimbali waliotembelea hifadhi hizo kubwa nchini Tanzania, ikiwamo ya Kilimanjaro, warejee. Hifadhi ya Serengeti iliyopo mkoani Mara ndiyo inayoongoza kwa kuingiza watalii wengi pamoja na mapato.
Kilimanjaro inashika nafasi ya pili, huku Tarangire ya mkoani Manyara ikiwa nafasi ya tatu, ikichangia asilimia 11 ya mapato yote ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Uongozi wa hifadhi hizo umebainisha hatua hiyo na mikakati ya kukabiliana na wingi wa watalii, unaotokana na jitihada za Serikali za kutangaza vivutio kwenye hifadhi, jambo linalochangia ongezeko la watalii wa ndani na nje ya nchi.

Mikakati ya Serikali ni pamoja na ule wa Rais Samia Suluhu Hassan aliposhiriki utengenezaji wa filamu ya The Royal Tour, aliyoanza kuirekodi Agosti 29, 2021, kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii.
Aprili 18, 2022, Rais Samia alishiriki uzinduzi wa filamu hiyo nchini Marekani, kisha filamu hiyo ikazinduliwa jijini Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar, na tangu wakati huo, idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka.
Mwananchi limepata fursa ya kutembelea hifadhi hizo pamoja na waandishi wengine na kuzungumza na viongozi wa hifadhi, watalii na waongoza watalii, ambao wanasema janga la Uviko 19 lilitikisa sekta nyingi, ikiwamo ya utalii.
Uviko 19 ilitokea mwaka 2021 na kuathiri sekta mbalimbali, ikiwamo zuio la wasafiri kutoka taifa moja kwenda lingine. Ni kwa sababu hiyo, utalii unaotegemea wageni kutoka ng’ambo uliathirika kwa sehemu kubwa.
Takwimu za watalii na waongozaji watalii zinaonyesha kuwa idadi inapanda, huku hali za kiuchumi zikiimarika tofauti na huko nyuma. Hii ni kutokana na mkakati huo wa Rais Samia kucheza filamu ya The Royal Tour. Hifadhi nazo zinaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuwavutia zaidi watalii.
Mkuu wa Kitengo cha Watalii wa Hifadhi ya Tarangire, Upendo Massawe, anasema kuwa kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika, zimebaini uwepo wa familia ya tembo ambao huzaliwa pacha, jambo ambalo ni adimu na likitumika vizuri linaweza kuwavutia wageni wengi kufika kujionea.
Upendo, ambaye pia anakaimu mkuu wa hifadhi, anasema wanaendelea na jitihada za kuwaomba Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri) “ili waweke kora ili kuwatumia kuwatangaza. Karibu Tarangire ili ujionee tembo wanaozaa pacha.”
Anasema kwa sasa inakuwa vigumu kuwabaini, lakini maofisa wa Tawiri wanawafahamu, na ikikamilika itasaidia zaidi kuwafahamu.
Magreth Maina, aliyekuwa na wanafunzi kutoka nchini Canada waliofika Hifadhi ya Tarangire, anasema: “The Royal Tour imekuwa sababu ya wao kutembelea Hifadhi ya Tarangire na Ngorongoro ili kujionea kile ambacho Rais alikionesha kwenye filamu. Niwasihi Watanzania wenzangu tutembelee vivutio vyetu.”
Mwongoza watalii, Gedion Paul, anakiri kuwa idadi ya wageni imeongezeka kwa kasi huku akitoa wito kwa wadau wengine, akisema: “Sasa imebaki jukumu letu kama waongozaji kuhakikisha wageni wanapata huduma bora na wanaridhika na uzuri wa Tarangire.”
Utalii wa usiku ukoje?
Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambaye pia ni Ofisa Mhifadhi Mkuu, Victor Ketansi, akijibu swali kuhusu ni mikakati gani inawekwa kuwafanya watalii waliotembelea hifadhi warejee, anasema ni kuanzisha mazao mawili ya utalii.

Anasema kwa kuwa vivutio vilivyopo ni vya asili, hawana mpango wa kuviboresha zaidi: “Tunataka kuongeza mazao mengine ya utalii, kwamba watalii wawe na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kile walichokwisha kukiona.”
Ketansi anasema kuwa katika mwaka ujao wa fedha 2025/26 wanataka kufanya utafiti wa kuanzisha bidhaa mbili ikiwemo: “Utalii wa usiku eneo la Kaskazini mwa Serengeti. Yaani watalii waingie kwenye magari yao, watembee usiku na kuangalia wanyama usiku kama wanavyofanya mchana.”
Anasema ikiwa hilo litapita, mtalii aliyetembelea Serengeti miaka miwili au zaidi atakuwa na sababu ya kurejea. Eneo jingine ni kuongezwa kwa hifadhi hiyo karibu na Ziwa Victoria.
“Tunaanzisha utalii wa Ziwa Victoria, na mtalii akija anakwenda kutembelea kule kuona shughuli zinazoendelea. Sasa haya mazao mawili yakipita, yataingizwa na kuwafanya watalii zaidi kutembelea kwenye hifadhi yetu,” anasema Ketansi.

Aidha, anasema kuwa kutokana na kuongezeka kwa watalii, wameanza kujipanga kwa miaka mitano ijayo kwa kujenga miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi. Hilo linafanyika kwa kushirikiana na wadau wa utalii na ujenzi wa malazi ndani ya hifadhi.
Katika maelezo yake, Ketansi anasema kuwa idadi ya watalii inaongezeka kutokana na jitihada za Serikali zinazochagiza kuongezeka kwa watalii kwenye hifadhi mbalimbali, ikiwemo filamu ya The Royal Tour.