Kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Uganda jana kumeifanya timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kuwa timu ya kwanza kuaga fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo (AFCON U17) zinazoendelea Morocco.
Maumivu kwa Serengeti Boys hayajaishia kwa Serengeti Boys kutolewa tu bali pia kupoteza rasmi fursa ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huop zitakazofanyika Qatar baadaye mwaka huu.

Mabao ya Simon Manyama, Richard Okello na James Bogere katika kipindi cha pili, yalimaanisha kuwa Serengeti Boys haiwezi kufikisha pointi nne ambazo Morocco na Zambia zilizotoka sare tasa kila moja inazo na hivyo haitoweza kutinga robo fainali.
Kwa kuwa imebakiza mchezo mmoja, Setengeti Boys inaweza kumaliza ikiwa na pointi tatu tu lakini bado itaishia kushika mkia kwenye kundi A la mashindano hayo.
Kanuni ya 60 ya mashindano hayo inabainisha kuwa iwapo timu zitalingana kwa pointi katika hatua ya makundi, kigezo cha kwanza ni iliyofanya vizuri katika mechi baina ya timu hizo itasonga mbele.
“Ikiwa kuna ulingano wa pointi baina ya timu mbili mwishoni mwa hatua ya makundi, timu zitapangwa kwa mtiririko wa vigezo vifuatavyo, idadi kubwa ya pointi zilizokusanywa katika mechi baina ya timu husika, tofauti ya mabao katika mechi zote za makundi, idadi kubwa ya mabao yaliyofungwa katika mechi zote za makundi na mchoro wa kura uliofanywa na kamati ya maandalizi,” inafafanua kanuni hiyo.
Hata ikipata ushindi katika mechi iliyobakiza dhidi ya Morocco, Aprili 6 mwaka huu, Serengeti Boys haitoweza kufikisha pointi nne na hivyo haiwezi kuingia robo fainali, hatua ambayo ingeweza kuipatia tiketi ya kushiriki moja kwa moja Kombe la Dunia.
Fursa pekee ambayo ilibakia kwa Serengeti Boys ni kufuzu Kombe la Dunia kupitia mechi za mchujo kwa kushika nafasi ya tatu kwenye kundi (best loser) lakini kumaliza kwenye nafasi hiyo haiwezekani kwa vile ikishinda mechi ya mwisho itakuwa sawa na Uganda kama nayo itapoteza kwa Zambia lakini Serengeti Boys itamaliza ya nne kwa vile Uganda imepata matokeo mazuri kwenye mechi baina ya timu hizo.
Serengeti Boys imekuwa haina historia nzuri kwenye fainali za AFCON U17 ambapo kuanzia fainali za 2017 hadi sasa, imepata ushindi mara tu ambao ulikuwa dhidi ya Angola, Mei, 18, 2017 zilipofanyika gabon ambapo ilishinda mabao 2-1.
Mechi nyingine saba, imepata sare moja na imepoteza michezo sita.
Kocha wa Serengeti Boys, Aggrey Morris amesema kuwa wamesikitishwa na matokeo waliyopata na hesabu zao ni mchezo wao wa kukamilisha ratiba dhidi ya Morocco.
“Mchezo tulianza vizuri kama tulivyokuwa tumepanga, vijana walijitahidi kwa nafasi yao nawapongeza kwa hilo ila mpira ni mchezo wa makosa na yametuadhibu. Kwa sasa tunaangalia mchezo wa mwisho ili tuone kama tunaweza kupata kitu vijana wajione kama walikuja kwenye mashindano,” amesema Morris.