
Dar es Salaam. Kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Aggrey Morris amesema kuwa lengo lao la msingi katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo (Afcon U17) 2025 ni kufuzu Kombe la Dunia.
Mashindano hayo yatafanyika Morocco kuanzia Machi 30 hadi Aprili 19 mwaka huu ambapo Serengeti Boys imepangwa kwenye kundi A ambalo linaundwa na wenyeji Morocco, Zambia na Uganda.
Timu nane zitakazoingia hatua ya robo fainali zitafanikiwa kufuzu moja kwa moja fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo zitakazofanyika Qatar, Novemba 3 hadi 27 zikiungana na nyingine mbili ambazo zitamaliza katika nafasi ya tatu kwenye hatua ya makundi zikiwa na matokeo bora, kuifanya Afrika iwakilishwe na timu 10.
Morris alisema kuwa pamoja na ugumu wa kundi ambalo Serengeti Boys imepangwa, itahakikisha inafanya vizuri ili ifuzu Kombe la Dunia kwa vijana wa umri kwa mara ya kwanza.
“Kundi letu ni gumu na kila timu inahitaji nafasi. Tupo tayari kwa mashindano na tutajiandaa vizuri sana tufikie malengo na ndoto yetu ya kufuzu Kombe la Dunia ambayo itatusukuma kujitoa zaidi.
“Sasa tunawajua wapinzani wetu. Morocco, Uganda na Zambia ambazo ziko kwenye kundi letu ni nzuri na shindani. Droo imetupa fursa ya kujiandaa vizuri ili tufikie malengo yetu,” alisema Morris.
Mara mbili tofauti ambazo Serengeti Boys ilishiriki Afcon U17 ambazo ni 2017 na 2019 haikufanikiwa kufuzu Kombe la Dunia.
Timu hiyo katika awamu zote hizo iliishia katika hatua ya makundi na Afrika ilikuwa ikiwakilishwa na timu nne tu ambazo ziliingia nusu fainali ya Afcon U17.