Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema sera mpya ya mambo ya nje itakayozinduliwa mwezi huu itatatua changamoto kadhaa ikiwamo ukosefu wa mwongozo wa kushirikiana na Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora).
Mambo mengine yatayokuwemo kwenye sera hiyo ya mwaka 2001 ni kushughulikia changamoto zinazolikabili Taifa, zikiwemo uhalifu wa mipakani, uratibu hafifu wa mikataba ya kimataifa, ukosefu wa mwongozo wa ushirikiano na matumizi hafifu ya lugha ya Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa.
Balozi Kombo amesema hayo leo Jumatano ya Mei 7, 2025 alipozungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Kombo, sera hiyo yenye umri wa miaka takriban 25, pia itajumuisha masuala ya mazingira na uchumu wa buluu.
“Kama tulivyosikia baadhi ya changamoto, Serikali ikaona kuna haja ya kuifanyia maboresho sera yetu, ambayo yalilenga kuongeza uzingatiaji wa mila na Katiba, kuweka mfumo wa uratibu wa mikataba, kushirikisha diaspora wa Tanzania, kutumia Kiswahili kama bidhaa na kuingiza masuala ya uchumi wa buluu, mazingira, jinsia na vijana,” amesema.

Amesema sera hiyo iliyofanyiwa maboresho mwaka 2024 itazinduliwa Mei 19, 2024 na Rais Samia Suluhu Hassan.
Sera ya Mambo ya Nje ni muongozo wa Uhusiano wa Kimataifa wa Tanzania ambao unalenga kulinda masilahi ya Taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii, kwa kuzingatia misingi ya uhuru, haki za binadamu, demokrasia na ujirani mwema.
Waziri huyo amesema pia inalenga kukuza diplomasia ya uchumi, kulinda masilahi ya Taifa, kuendeleza uhusiano na nchi na taasisi mbalimbali na kuchangia amani na maendeleo duniani.
Kombo pia amesema sera hiyo imelenga kujenga mazingira wezeshi ya ndani, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kukuza diplomasia ya uchumi, kushughulikia masuala ya madeni, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, na kudumisha misingi ya sera ya kutofungamana na upande wowote.
“Sote tunafahamu kuwa mabadiliko mbalimbali yaliyotokea duniani, na kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuifanyia mapitio sera ya Mambo ya Nje kwa kushirikisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha Taifa linanufaika zaidi na uhusiano wa kimataifa.
“Mapitio ya sera hii yamebaini kuwa misingi ya sera bado inafaa, lakini kuna haja ya kufanya marekebisho ya mikakati badala ya kutunga sera mpya,” amesema Kombo.
Kombo ametaja matokeo chanya yatakayopatikana na marekebisho ya sera hiyo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa masoko ya nje, kuongezeka kwa watalii, kukua kwa matumizi ya Kiswahili, kuongezeka kwa diaspora wa Tanzania na uchumi wa buluu na kuimarika kwa ujirani mwema.
Ujio wa sera mpya ni mwendelezo wa mikakati ya wizara hiyo na January Makamba, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kabla ya Kombo, alitaja mambo matatu yatakayoingizwa kwenye sera hiyo mpya.
Mambo hayo ni diplomasia ya uchumi, uchumi wa buluu na mabadiliko ya tabianchi na kuwa itaendelea kubeba misingi ya sera ya awali ikiwamo ya kuhimiza amani, mshikamano na ushirikiano wa kikanda.
Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, wa wizara hiyo, Justin Kisoka aliwahi kusema baadhi ya misingi ya sera hiyo ni uhuru wa nchi kujiamulia yenyewe, kukuza ujirani mwema, kukuza ushirikiano wa kiuchumi na washirika wa maendeleo.
Alisema misingi mingine ni kutofungamana na upande wowote, kuendeleza umoja wa Afrika na kuunga mkono Umoja wa Mataifa katika jitihada za maendeleo ya kiuchumi, kulinda amani na usalama.
Ziara ya Rais wa Finland
Katika tukio jingine, Kombo amesema Rais wa Jamhuri ya Finland, Alexander Stubb atafanya ziara ya kitaifa nchini kuanzia Mei 14 hadi Mei 16, 2025.
Amesema ziara hiyo inafanyika kufuatia mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan alioutoa kwa kiongozi huyo.
Kombo amesema ziara hii ya kihistoria ni ya kwanza kufanywa na Rais wa Finland nchini tangu mwaka 2003 ambapo aliyekuwa Rais wa Findland wakati huo, Tarja Halonen aliitembelea Tanzania.
“Ziara hii inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara na maendeleo kati ya nchi hizo mbili, pia inathibitisha kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili ambazo zimekuwa na ushirikiano wa miongo zaidi ya sita sasa,” amesema Kombo.

Kombo amesema miongozi mwa shughuli atakazofanya Rais Stubb kwenye ziara yake ni kushiriki semina ya Urithi wa Hayati Martti Ahtisaari, ya kuenzi mchango wake katika upatanishi na kuzindua mradi mpya wa FORLAND, unaolenga kuboresha usimamizi wa matumizi ya misitu, ardhi na kuongeza mnyororo wa thamani.