
Dodoma. Serikali imetoa wito kwa wazazi na walezi kutimiza jukumu lao la msingi katika malezi na makuzi ya watoto wao.
Pia, imesisitiza kuwa ni muhimu kwa wazazi kuandaa kizazi cha baadaye kilicho na maadili mema.
Aidha, Serikali imetoa ombi kwa watu wenye uwezo kusaidia wahitaji katika jamii, ili kuimarisha ustawi wa watoto na familia kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Machi 24, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati akizungumza na wazazi na walezi wa watoto waishio katika mazingira hatarishi wakati akikabidhi vyakula, nguo na magodoro kwa vituo 13 vinavyolea watoto hao mkaoni hapa.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kila mtu akitimiza wajibu wake, hakutakuwa na mahali penye upungufu lakini inatokea hivyo kwa sababu wengi wanakwepa majukumu yao na kuwaachia watu wengine.
Senyamule amesema maisha ya mwanadamu hapa duniani yanahitaji amani, umoja na mshikamano lakini bila kuwasahau wenye uhitaji na siku zote kutenda hiyo ndiyo kupata thawabu mbele za Mungu.
“Shime kwa watu wenye uwezo tujitahidi kujijenga kwenye imani kwa kutoa sadaka kwa ndugu zetu wenye mahitaji,” amesema Senyamule.
Amewaagiza wakuu wa wilaya ambako vituo hivyo vipo kuhakikisha kila kitu kilichopangwa kupelekwa, kinafikishwa kwa walengwa na mapema iwezekanavyo ofisi yake ipokee taarifa.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya ambazo vituo hivyo vimekabidhiwa msaada, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabil Shekimweri amewataka maofisa Ustawi wa Jamii mkoani Dodoma kuendelea kutoa ushirikiano na watu wanaowalea watoto hao.
Alhaj Shekimweri amewataka maofisa hao kutokuwahukumu wenye vituo kwa kuwafungia pale wanapobaini kuna mapungufu kidogo, badala yake waendelee kuwapa elimu ili wafanye maboresho.
“Maofisa Ustawi wakati mwingine tumieni busara, siyo mnapofika kwenye kituo mnakuta mapungufu kidogo mnakimbilia kuwafungia, wakati mwingine busara ziwaongoze kwa kuwapa elimu na kuwataka waondoe mapungufu kidogo mtakayobainisha,” amesema Alhaj Shekimweri.
Mwakilishi wa watu wanaowalea watoto waishio kwenye mazingira magumu, Hajat Aisha Nobo amesema ni vema Serikali na wadau wengine kuendelea kutupia macho kwenye vituo vya kulelea watoto hao, kwani kuna mahitaji mengi yanayotakiwa katika malezi yao.