Bunge la Seneti la Australia limemkaripia seneta mtetezi wa haki za wakazi asili wa nchi hiyo, Lidia Thorpe, kwa matamshi yake yaliyozusha utata dhidi ya Mfalme wa Uingereza Charles III na kutokana na kuutuhumu utawala wa kifalme wa Uingereza kuwa unahusika na mauaji ya kimbari.
Kwa kujibu wa ripoti ya ABC News, wakati wa hotuba ya Mfalme Charles III wa Uingereza katika Bunge la Australia mwezi uliopita, Seneta Thorpe alimshutumu kwa kuhusika na mauaji ya kimbari.
Baada ya tukio hilo, seneta Lidia Thorpe alifichua kuwa hakula kiapo cha utiifu kwa mfalme huyo wa Uingereza alipoapishwa mwanzoni mwa muhula wake wa useneta, madai ambayo yalizua maswali na mjadala kuhusu kuendelea kuwepo kwake katika Seneti ya Australia.
Kulingana na ripoti hiyo, Thorpe amekemewa kwa kile kilichotajwa kuwa tabia ya “kukosa heshima” na “kufanya uharibifu”.
Serikali na muungano unaotawala wa Australia inadai kuwa Thorpe amedharau taasisi za kidemokrasia kwa mwenendo huo. Pia imeamuliwa kuwa hatakuwa tena na haki ya kuwakilisha Seneti katika jumbe rasmi, ikiwa ni pamoja na safari ijayo ya Visiwa vya Pasifiki.

Mwaka 2022, Seneta Lidia Thorpe alimtaja Malikia Elizabeth II wa Uingereza kuwa ni malkia “mkoloni” na aliinua ngumi yake juu kama alama ya nguvu ya watu weusi, wakati akila kiapo katika Bunge la Australia.