
Nchini Senegal, waziri wa zamani wa sheria chini ya utawala wa Macky Sall ameshtakiwa kwa jaribio la rushwa na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa bangili ya kielektroniki. Ismaïla Madior Fall ni mjumbe wa pili wa zamani wa serikali inayomaliza muda wake kushtakiwa na Mahakama Kuu ya Haki, mahakama maalum iliyoanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwaka na ina mamlaka ya kuwahukumu marais na mawaziri kwa vitendo walivyofanya katika utekelezaji wa majukumu yao.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Aliyekuwa Waziri wa Madini Aïssatou Sophie Gladima pia anashtakiwa na amefungwa. Anahusishwa na madai ya ubadhirifu wa faranga za CFA milioni 193 (karibu euro 295,000). Kiasi ambacho kilipaswa kutumika kujenga kituo cha wachimbaji dhahabu walioathiriwa na UVIKO-19, lakini ambacho hakijawahi kujengwa.
Matumizi ya pesa nyingi wakati wa mzozo wa Covid-19
Siku ya Jumatatu, Waziri wa zamani wa Masuala ya Wanawake, Salimata Diop alishtakiwa kwa “kuhusika katika ubadhirifu” wa fedha zilizokusudiwa kufadhili mpango wa kupambana na UVIKO-19 kati ya mwaka 2020 na 2021. Aliachiliwa kwa dhamana baada ya kulipa Euro 87,000, pamoja na mawaziri wengine watatu wa zamani, akiwemo shemeji yake Macky Sall, Mansour Faye. Salimata Diop anahusishwa katika usimamizi wa mfuko huu. Katika ripoti yake, Mahakama ya Wakaguzi ilibaini msururu wa ukiukwaji wa uhasibu, kama vile kutoza fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa mchele kwa kaya zisizojiweza au ununuzi wa jeli za kileo.
Huu ni msururu wa mashtaka ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya mawaziri wa zamani. Hili ndilo pingamizi zima la Mahakama Kuu ya Haki iliyowekwa mnamo Desemba 28, 2024, ili mamlaka ya juu zaidi ya taifa pia iweze kuwajibika mbele ya mfumo wa haki wa Senegal.
Taasisi imefanya mageuzi
Kwa mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la 3D, Moundiaye Cisse, anasema hii inadhihirisha utendakazi mzuri wa taasisi: “Ni vyema, kwa sababu tuna mfumo wa haki ambao unajaribu kuweka kila mtu kwenye usawa. Ni chombo kizuri, lakini kinahitaji kufanyiwa marekebisho ili kukiweka sawa na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.”
Mageuzi, kwa sababu Mahakama Kuu ya Haki, iliyopewa mamlaka ya kuhukumu marais na mawaziri, na iliyoanzishwa mwezi wa Desemba mwaka jana, haitoi uwezekano wa kukata rufaa dhidi ya maamuzi yake. Kwa Babacar Ba wa Jukwa la utekezaji wa haki, huu ni ukiukwaji wa hukumu ya haki ambayo lazima irekebishwe: “Ili tuweze kusema kwamba mtu amenufaika na kesi ya haki, ikiwa mtu hajaridhika na hukumu, mtu huyo lazima awe na uwezekano wa kukata rufaa katika mahakama ya juu ili kesi iweze kusikilizwa tena kwa misingi ya haki. Lakini kwa Mahakama Kuu ya Haki, watu hawana chaguo hilo.”
Kwa hivyo mashirika kadhaa ya kiraia yanatoa wito kwa mamlaka kurekebisha kwa haraka sheria ya ndani ya mfumo wa haki inayohusiana na Mahakama Kuu ya Haki ili kuhakikisha kesi ya haki.