Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, amemuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Simanjiro, Kidwadi Ally kumlaza mahabusu polisi wa Kata ya Loiborsiret, Ester Tairo kwa uzembe wa kushindwa kumchukulia hatua mtu aliyempa mimba mwanafunzi wa shule ya sekondari.
Pia, Sendiga amemweleza Ally, kuwa askari polisi wa eneo hilo wanalalamikiwa kwa kupokea rushwa, hivyo achukue hatua ya kuwasimamia ipasavyo.
Sendiga amechukua hatua hiyo baada ya kusikiliza malalamiko ya mkazi wa kata ya Loiborsiret, Sioni Tupakeni ya mtoto wake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibosho iliyopo mkoani Kilimanjaro, kupewa mimba na mtoto wa familia ya mwalimu aliyemlea mtoto huyo.
Mama huyo Sioni amewasilisha malalamiko hayo kwenye mkutano wa hadhara wa mkuu huyo wa mkoa wa Manyara, Sendiga, uliofanyika Aprili 5,2025.
“Binti yangu, anateseka kwa kupewa mimba na mtoto wa familia ya mwalimu aliyemlea, na nilipofikisha suala hilo kwa ofisa mtendaji wa kijiji na polisi wa kata hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa,” amesema.
“Huyu polisi kata amepewa malalamiko wala hakuchukua hatua yoyote sasa leo naondoka naye ili iwe fundisho kwa wengine,” amesema Sendiga.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, (kushoto) akiwa kwenye ziara ya kutembelea wilaya ya Simanjiro na kuzungumza na wakazi wa eneo hilo na kusikiliza kero zao. Picha na Joseph Lyimo
Hata hivyo, polisi kata huyo Ester Tairo ameeleza kuwa alipata taarifa ya tukio hilo wiki iliyopita na siyo muda mrefu kama ilivyoelezwa.
“Mheshimiwa tukio hilo nimepata taarifa yake siku saba zilizopita na nikawa nafuatilia ili kuchukua hatua,” amesema Tairo.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamepongeza hatua iliyochukuliwa na mkuu huyo wa mkoa dhidi ya tukio hilo la kusikitisha akiwamo Emmanuel Mollel ambaye amesema, haki imeonekana kwa muda mfupi wa kuwasilishwa kwa tatizo na kuchukuliwa hatua.
“Tunampongeza mkuu wetu wa mkoa kwa kuchukua hatua kwa muda mfupi, kwani matukio ya kikatili kama haya yasipofanyiwa kazi yataongeza machungu,” amesema Mollel.