
Mwanza. Kanda ya Ziwa imetajwa kuongoza kuwa na watu wengi wenye ugonjwa wa selimundu nchini, wakihusishwa na ugonjwa wa malaria.
Utafiti uliofanywa mwaka 2023/24 na Emmanuela Ambrose, daktari na mtafiti wa selimundu katika Chuo Kikuu cha Tiba Bugando, umeonesha wagonjwa wengi wanatokea Kanda ya Ziwa.
Selimundu ni ugonjwa wa kurithi unaosababishwa na hitilafu katika vinasaba vya damu, hivyo kushambulia seli za damu kutoka kwenye umbo la duara ambalo ni la kawaida, kuwa umbo la mfano wa mwezi mchanga na kusababisha damu kushindwa kupita vizuri katika mishipa yake.
Hitilafu hiyo husababisha mgonjwa kuishiwa damu mara kwa mara, kupata nimonia, homa ya manjano, maumivu makali hasa maeneo ya kifua, mbavu, tumbo, mifupa, mgongo na uwezekano wa uharibifu wa viungo mwilini kama vile ubongo, moyo, mapafu, macho na figo.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Molle watoto 11,000 hadi 14,000 huzaliwa na ugonjwa wa selimundu kila mwaka, huku idadi ya wagonjwa ikikadiriwa kuwa zaidi ya 200,000 nchini.
Dk Mollel, aliyekuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Hassan Toufiq aliyeuliza bungeni, ni Watanzania wangapi wenye tatizo la sikoseli na ni mikoa mingapi imeathiriwa sana na ugonjwa huo Novemba, 2023, alisema mikoa inayoongoza kwa ugonjwa huo ni Mwanza, Tabora, Kigoma, Mara, Dar es Salaam na Pwani.
Uhusiano wa selimundu na malaria
Dk Emmanuela, aliyekuwa miongoni mwa washindi wa tuzo ya watafiti waliochapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa kwa mwaka 2024, anasema ukanda wa ziwa umekuwa ukiongoza sana kwenye ugonjwa huo.
“Kanda hii inaonekana kwa Tanzania ndiyo zaidi ina watu wengi wenye sikoseli, wanaoenda sehemu nyingine wanagundulika kwamba wametokea ukanda wa ziwa… kwa nini? Wanasema ni kwa sababu tuko kwenye tropiki,” anasema.
Anasema ukanda wa kitropiki una malaria nyingi ambayo imehusishwa sana kusababisha hitilafu zinazosababisha vinasaba vya selimundu.
“Selimundu zamani haikuwepo… mwanzo kabisa kwenye ukanda wa kitropiki tulikuwa na malaria, lakini kabla hatujapata ufafanuzi wa matibabu ya malaria watu wengi sana walikufa, baadaye mwili ukatengeneza njia mbadala ya kuweza kupingana na malaria kabla dawa hazijaja,” anasema na kuongeza:
“Katika kutengeneza huo mbadala ndio ikatengeneza hitilafu kwenye vinasaba, kwa hiyo watu waliokuwa wanazaliwa kwa kipindi hicho ili kuweza kujikinga na malaria, wakazaliwa na vinasaba vya selimundu …”
Anasema baada ya uhusiano wa kindoa kuzidi, waliokuwa na vinasaba wakajikuta wakioana na wenye vinasaba wengine na hivyo kupata watoto wenye selimundu.
Utafiti wawaokoa watoto wenye selimundu dhidi ya kiharusi
Dk Emmanuela, ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha selimundu katika Hospitali ya Bugando, anasema katika utafiti ambao umeshinda tuzo, waliangalia namna ya kuwaokoa watoto wenye selimundu wanaopata kiharusi.
“Tuliangalia kwamba watoto wengi ambao wanakuja katika hospitali yetu wamekuwa wanapata kiharusi… jinsi gani tunaweza kuwazuia wakapata stroke (kiharusi) ndio tukafanya utafiti tukatumia dawa inayoitwa Hydroxyurea kama itaweza kuwazuia kupata stroke na tunashukuru tuliweza kuchapisha tafiti hii katika majarida ya kimataifa na ukaweza kushinda,” anasema.
Anasema asilimia 11 ya watoto wenye selimundu wanapata kiharusi kutokana na ugonjwa huo. Hata hivyo, dawa hiyo imekuwa mwarobaini kwa kuwa inazuia kiharusi, maumivu na kuwaepusha kulazwa mara kwa mara.
Juni, 2021 hadi Juni 15, 2022 watoto wachanga 5,000 waliozaliwa Hospitali ya Bugando walifanyiwa uchunguzi ambapo watoto 1,300 walibainika kuwa na ugonjwa wa selimundu, huku 150 wakitajwa kurithi kutoka kwa wazazi wao wote.
“Tumeendelea kufanya tafiti nyingine nyingi zinazohusiana na selimundu kuangalia ukubwa wa tatizo na tumeona wadau wengi wamekuwa wakijitokeza na kutaka kusaidia upande wa matibabu. Tutahakikisha tunasambaza majibu ya tafiti zinazokuja ili kila mtu apate uelewa na kujikinga dhidi ya selimundu,” anasema Dk Emmanuela.
Jinsi ya kuepuka selimundu
Mtafiti huyo anasema: “Huu ni ugonjwa wa kurithi, endapo tutaweza kupima afya zetu kama tumerithi hizi chembe chembe za selimundu, itakuwa ni vema kuutokomeza kwa sababu wengi wao hatujifahamu kama tumerithi.”
Anaongeza kuwa kama nchi itaweka mpango mkakati wa kila mtu apime au kabla hajaoa au kuolewa, itapunguza watoto wanaozaliwa na selimundu pamoja na kuwapima wanafunzi waliopo shuleni ili kujua hali zao.
“Wengi wanaingia kwenye uhusiano hawajui hali yao ya afya…wanakuja tu kushangaa mtoto anaumwa katika umri fulani wa mwanzo, hii ndiyo shida,” anaeleza daktari huyo na kuongeza:
“Kwa sasa kwa upande wa hapa (Bugando), tunapima watoto wale waliozaliwa…nadhani kuna mpango mkakati unakuja Kanda ya Ziwa kupima watoto wote walio chini ya miaka mitano.”
Magonjwa Kanda ya Ziwa
Mikoa ya Kanda ya Ziwa inatajwa kuongoza kwa wanawake kujifungua watoto wenye ugonjwa wa mdomo sugura, lakini pia ugonjwa wa pumu ya ngozi unatajwa kuwa kinara wa magonjwa ya ngozi yanayowatesa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Takwimu zinaonyesha wastani wa wagonjwa wapya 300 wanaogundulika kuugua na kutibiwa magonjwa ya ngozi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kila wiki, wagonjwa 120 sawa na asilimia 40 hugundulika kuugua ugonjwa huo.
Ugonjwa mwingine unaodaiwa kuongoza Kanda ya Ziwa ni saratani ambayo inadaiwa kuongezeka mwaka hadi mwaka kutoka wagonjwa 320 waliotibiwa kitengo cha kuhudumia saratani kilipoanzishwa hospitali ya Bugando na kufikia wastani wa wagonjwa 14,000 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, asilimia 52 ya Watanzania, sawa na watu milioni 22 wanaugua ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo, Kanda ya Ziwa inaongoza kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 50 hadi 80 ya magonjwa hayo ambayo hayapewi kipaumbele.