
LICHA ya kutopata nafasi kwenye kikosi cha Wydad AC, mshambuliaji wa Kitanzania, Selemani Mwalimu ‘Gomez’ ameanza kuingia kwenye mfumo wa kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco.
Januari 31 nyota huyo alitambulishwa kwa mabingwa hao wa zamani wa Ligi ya Mabingwa Afrika akitokea Fountain Gate alikokuwa anacheza kwa mkopo kutoka Singida Black Stars kwa mkataba wa miaka mitatu.
Tangu atambulishwe kikosini hapo Wydad imecheza mechi nane, Gomez akicheza mechi mbili akitokea benchini na nyingine hakuwa sehemu ya kikosi hicho.
Mechi yake ya kwanza ilikuwa Februari 22 akicheza kwa dakika 31 dhidi ya COD Meknes, Wydad ikitoa suluhu.
Kwenye mchezo ule ambao ulikuwa wa kwanza kwa nyota huyo kucheza kimataifa alionyesha kiwango bora licha ya bao alilofunga kukataliwa mwamuzi akiamuru mshambuliaji huyo aliotea.
Baada ya hapo Februari 28 Wydad ikacheza na RS Berkane na kutoa sare 0-0, Machi 09 dhidi ya FUS Rabat 2-2 Gomez hakuwepo hata benchi.
Machi 15 alipewa dakika sita kwenye mchezo dhidi ya IR Tanger na kuonyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji kuanzia anapopata mpira, pasi zake jambo linaloonyesha anaitaka namba mbele ya kocha Rulani Mokwena.
Gomez aliondoka Fountain Gate akiwa ameifungia mabao sita akiwa kinara wa mabao wa timu hiyo inayotumia uwanja wa Kwaraa, Manyara na hadi kufikia sasa hakuna mchezaji wa timu hiyo aliyempita kwa mabao.
Kabla ya kutua Singida, alitokea KVZ ya Ligi Kuu ya Zanzibar ambako alikuwa mfungaji bora wa ligi kwa mabao 20.