Sekta ya madini yaajiri Watanzania 19,000 tangu 2021

Dodoma. Watanzania 19,371 wameajiriwa kwenye kampuni za uchimbaji wa madini katika kipindi cha kati ya mwaka 2021/22 hadi Januari mwaka 2025.

Hayo yamesemwa leo, Jumanne Machi 4,2025 na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Ramadhani Lwamo alipokuwa akielezea mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita na mwelekeo wa tume hiyo.

“Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye kampuni mbalimbali za uchimbaji ambapo katika kipindi cha 2021 hadi Januari 2025. Kati ya ajira 19,874 zuilizotolewa, 19,371 ni za Watanzania sawa na asilimia 97.5,” amesema.

Amesema ajira za wageni ni 503 ambazo ni sawa asilimia 2.5 ya ajira zote zilizozalishwa kwenye kipindi hicho.

Aidha, Lwamo amesema katika kipindi hicho zimetolewa leseni za uchimbaji mkubwa wa madini ya Kinywe, nikeli, dhahabu na nyinginezo.

Ametaja maeneo ambayo miradi hiyo ilitekelezwa kuwa kuwa ni Mahenge (Morogoro), Ngualla (Songwe), Ngara Kagera), Sengerema (Mwanza) na Pangani (Tanga).

Lwamo amesema tume imefanya ukaguzi katika masuala ya usalama, afya, mazingira katika migodi midogo 60,761 iliyopo katika mikoa 26 ya a Morogoro, Tabora, Arusha, Kahama, Mwanza na Tanga.

Maeneo mengine ni Manyara, Iringa, Njombe, Mbogwe, Shinyanga, Dodoma, Kigoma, Kagera, Chunya, Geita, Mara, Mbeya, Rukwa, Lindi, Ruvuma, Mtwara, Songwe, Pwani, Dar es Salaam na Katavi kwa uchache.

“Kwa mapungufu yaliyobainika katika kaguzi hizo, wahusika walielekezwa kuyafanyia kazi mapungufu hayo kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini Sura ya 123,”amesema.

Aidha,  Lwamo amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 hadi Februari, 2025, tume imekusanya jumla ya Sh690.76 bilioni sawa na asilimia 69.08 ya lengo la mwaka 2024/25

Mmoja ya wachimbaji wadogo, Mary Mathew ameiomba tume hiyo kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata mitaji ili waweze kuboresha shughuli  zao za uchimbaji wa madini.

“Kutukagua ni sawa lakini pia Serikali ingetuangalia wachimbaji wadogo tuweze kupata mitaji itakayotusaidia vifaa vya kuboresha shughuli zetu,” amesema.