Sekta ya madini kuvuka lengo, wadau wachambua

Dodoma/Dar es Salaam. Sekta ya madini nchini imevuka malengo yake baada ya kuchangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa (GDP) mwaka 2024 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya muda ulilengwa na Serikali kwenye Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano wa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema ongezeko hilo limetokana na mageuzi makubwa, usimamizi madhubuti wa taasisi na uongozi wa kimkakati wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Hili ni tukio la kihistoria,” amesema Mavunde. “Lengo lilikuwa ni kufikia asilimia 10 ya mchango kufikia mwaka 2026. Tunajivunia kuwa tumelifikia mapema.”

Kufuatia hilo wachambuzi wamepongeza juhudi za mageuzi ya Serikali huku wakatahadharisha kuwa kudumisha kasi hii kutahitaji mikakati maalumu, ikiwemo kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na kupanua mnyororo wa thamani katika usindikaji wa madini.

“Ukuaji huu unatokana na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali,” amesema Humphrey Simba, mtaalamu wa madini kutoka kampuni ya ASNL Advisory Limited.

“Lakini ili kuhakikisha mafanikio yanaendelea, lazima tuvutie wawekezaji wa ndani zaidi katika maeneo kama grafiti, nikeli, shaba na makaa ya mawe,” ameongeza.

Simba amebainisha kuwa kuongezeka kwa bei ya dhahabu kimataifa kumechochea ukuaji wa sekta hiyo. Amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani kwa kusafisha na kuchakata madini nchini, akisema hatua hiyo inaweza kuleta zaidi ya Dola bilioni moja katika fursa mpya za biashara.

Bei ya dhahabu imeongezeka kwa asilimia 88.12 katika kipindi cha miaka sita iliyopita, kutoka wastani wa Dola 1,269.23 kwa wakia moja mwaka 2018 hadi Dola 2,387.70 mwaka 2024.

Ongezeko hili limesababishwa na wawekezaji wanaotafuta maeneo salama ya kuhifadhi thamani ya fedha katikati ya misukosuko ya kiuchumi duniani na migogoro ya kisiasa, ikiwa ni pamoja na janga la Covid-19, vita ya Urusi na Ukraine, vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Moscow na mgogoro wa hivi karibuni katika ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), bei ya dhahabu imepanda zaidi wiki hii kutoka Sh8,899,135 (takriban Dola 3,324.71) kwa wakia moja Aprili 22 hadi Sh9,215,483 (takriban Dola 3,443.47) Aprili 23, ongezeko la Sh316,348 (takriban Dola 118.18).

Mchambuzi wa masuala ya fedha, Oscar Mkude amesema kupanda kwa bei hiyo kunadhihirisha wasiwasi wa kiuchumi duniani.

“Watu wana wasiwasi kuhusu mfumuko wa bei na thamani ya fedha zao. Dhahabu inaonekana kuwa njia salama ya kuhifadhi mali,” ameliambia gazeti dada la The Citizen.

Ameongeza kuwa Tanzania, kama muuzaji wa dhahabu, inaweza kunufaika ikiwa itaweza kuelekeza vizuri katika mazingira ya soko la dunia.

“Ingawa kuna ongezeko la mahitaji duniani, soko la dhahabu limejaa na haliwezi kutabirika kwa urahisi,” alisema Mkude. “Wanunuzi ni waangalifu. Muda sahihi na uaminifu wa soko ni mambo muhimu.”

Ili kuongeza mapato, Simba amesisitiza umuhimu wa viwanda vya kuongeza thamani. “Mengi ya mauzo yetu bado ni ya dhahabu iliyoyeyushwa tu. Kuanzisha vituo zaidi vya usindikaji na utengenezaji wa vito nchini kutachangia pakubwa kwenye pato la Taifa.”

Amegusia pia fursa kubwa ambazo bado hazijatumika kwenye madini kama nikeli na makaa ya mawe. “Baadhi ya maeneo ya uchimbaji bado hayajaanza kazi. Serikali inapaswa kuharakisha shughuli katika maeneo haya ili kupanua na kuimarisha sekta.”

Kuhusu makaa ya mawe amesema, ni muhimu katika kuendesha viwanda na kuzalisha umeme, hivyo kuna haja ya kuendelea kuchunguza na kuwekeza katika sekta hiyo.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania, Benjamin Mchwampaka ameeleza hali bora kwa wawekezaji. “Mageuzi yameleta mazingira bora kwa uwekezaji wa ndani na wa kigeni, kuanzia kwenye utafiti hadi usindikaji,” amesema.

Kauli hizi ziliungwa mkono na Shida Zakria, mmiliki wa kampuni ya Zasco Mining Society iliyopo Kahama. Amesifu mageuzi ya Serikali yanayowaunga mkono wachimbaji wadogo. “Sasa tunachangia asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini na tunafanya kazi sambamba na wachimbaji wakubwa,” amesema.

Zakria amesema hali bora ya soko na usimamizi mzuri kumeongeza ubora na bei ya dhahabu. “Sasa tunauza kwa ubora wa asilimia 98, tukipata hadi Sh300,000 kwa gramu.”

Mwaka 2023, sekta hiyo ilichangia asilimia 9.1 ya Pato la Taifa. Mavunde amesema ongezeko la mwaka 2024 limetokana na mageuzi endelevu, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa minada ya vito vya thamani, masoko ya ndani ya madini na vituo vya ununuzi, pamoja na hatua madhubuti za kudhibiti magendo.

Mchango mkubwa umetolewa na ushiriki wa moja kwa moja wa BoT kwenye soko la dhahabu.

BoT imekuwa ikinunua hadi asilimia 20 ya dhahabu inayozalishwa na wachimbaji wadogo. Tangu Julai 2024, imekwisha nunua tani mbili za dhahabu, na inalenga kufikia tani sita hadi mwisho wa mwaka wa fedha.

“Mageuzi ya kisheria na ya kitaasisi yameongeza uwazi, ufuatiliaji na ufanisi,” aMEsema Mavunde. “Uzalishaji katika sekta yote, hasa kwa wachimbaji wadogo, umeimarika kwa kiasi kikubwa.”

Amewataka wadau wote kufuata Sheria ya Madini na akaahidi kuwa serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa udhibiti utakaohakikisha uendelevu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *