Sekta binafsi inavyoongoza kwa mishahara midogo

Dar es Salaam. Kwa mujibu wa Utafiti wa Ajira na Mapato katika Sekta Rasmi Tanzania wa mwaka  2022/23, mtu mmoja kati ya wawili walio katika sekta hiyo wanalipwa mshahara wa chini ya Sh500,000.

Ripoti iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa, watu 1,996,555 kati ya 3,717,980 walio katika ajira wanalipwa kati ya Sh0 hadi Sh499,999 huku wanaolipwa mshahara wa kuanzia Sh700,000 na kuendelea ni asilimia 27.2 pekee.

Kiwango cha wanaolipwa juu ya Sh700,000 kinajumuisha asilimia 14.5 ya waajiriwa wote kutoka sekta binafsi na asilimia 40.7 ya waajiriwa wote wa serikalini huku wanaolipwa kati ya Sh500,000 hadi Sh699,999 wakiwa 717,570 pekee.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Februari 24, 2025, Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka amesema mishahara ina nafasi ya kuwapa watu nguvu katika uzalishaji huku akitolea mfano wa baadhi ya taasisi kulazimika kutumia motisha ili kuhakikisha malengo yake yanafikiwa.

Hali ilivyo

Sekta binafsi ndiyo inaongoza kwa kuwa na ajira zinazolipa mshahara mdogo licha ya kuwa imeajiri watu wengi kwa kuwa, takwimu zinaonyesha serikalini hakuna mtu anayelipwa chini ya Sh300,000.

Hili linaonekana wakati ambao utafiti unaonyesha kuwa, watu 316,028 wanalipwa mshahara wa Sh140,000 kushuka chini, watu 301,156 wanalipwa kati ya Sh140,001 hadi Sh199,999 huku 278,848 wakilipwa kati ya Sh200,000 hadi Sh299,999 ambao wote wanatoka sekta binafsi.

Hata hivyo, kuanzia mshahara wa Sh300,000 hadi Sh399,999 ndiyo Serikali ilianza kuonekana, ikijumuishwa waliopo sekta binafsi na wale wa umma, hivyo wanakuwa waajiriwa 691,544 kati ya waajiriwa wote.

Kundi hili ndiyo la pili kwa kubeba waajiriwa wengi kutoka serikalini baada ya wale wanaolipwa zaidi ya Sh700,000 kwani takwimu zinaonyesha asilimia 22.8 ya watumishi serikalini wako katika kiwango hiki cha mshahara.

Kwa wale wanaolipwa kati ya Sh400,000 hadi Sh499,999 ni asilimia 11 ya waajiriwa wote, Sh500,000 hadi Sh599,999 inabeba asilimia 11.1 ya waajiriwa wote, Sh600,000 hadi Sh699,999 inabeba asilimia 8.2.

“Hasa viwandani, hii mishahara ya Sh150,000 ipo sana ni vile tu watu hawana kazi nyingine za kufanya na kukaa nyumbani ni ngumu lakini inaumiza watu wengi,” amesema Doreen Mushi mkazi wa Tabata.

Amesema mishahara imekuwa ikilipwa wakati wote bila ya kuwapo kwa nyongeza kila baada ya muda fulani jambo linalowaweka katika wakati mgumu wa kumudu mahitaji yao ya kila siku wakati ambao gharama za maisha zinaendelea kupanda.

Hili huenda likawa halipo kwa watumishi wa sekta ya umma kwani wao kila mwaka sasa wamekuwa wakipatiwa nyongeza ya mshahara kutoka serikalini.

Nyongeza ya mshahara kila mwaka ilirudishwa katika Sikukuu ya Wafanyakazi ya mwaka 2023, Rais Samia Suluhu Hassan ndiye alitangaza kurejea kwa utaratibu huo ikiwa ni miaka saba tangu kuondolewa kwa mfumo huo na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli mwaka 2016.

Akizungumzia suala hilo, Dk Mwinuka wa Udom amesema mishahara ina maana kubwa katika kuwapa watu nguvu ya kununua na kuuza huku ikitegemea vitu vingine ikiwamo mfumuko wa bei.

Hata hivyo amesema ukubwa wa mshahara wa mtu haumaanishi ndiyo kigezo cha yeye kujituma kazini, badala yake zipo taasisi binafsi ambazo zimeamua kutumia motisha kwa wafanyakazi na zinafanya vizuri.

“Kuwa na motisha inayoendana na ufanisi hii ndiyo imesaidia taasisi nyingi kupiga hatua hili linafanyika kwa kuweka malengo ambayo mtu akiyafikia anapewa kitu fulani, hivyo si lazima mtu akilipwa vizuri ndiyo akawa na utendaji mzuri katika kazi,” amesema Dk Mwinuka huku akikubali kuwapo pia kwa mashirika yanayofanya vizuri na kulipa watu wake vizuri.

Dk Mwinuka amesema katika uchumi, vitu vinategemeana ikiwamo shughuli zenyewe, uzalishaji mali na namna zinavyoleta mapato huku akisema kadri zinapokuwa nyingi ndivyo zinavyowalipa watu wake.

“Kadri shughuli hizi zinavyozalisha fedha zaidi ndiyo watu wanaweza kulipwa zaidi kutokana na kutengeneza mzunguko wa fedha. Mzunguko huu unaweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi huku mfumuko wa bei ukitoa tathmini ya thamani ya fedha kwa kuonyesha uwezo wake wa kununua bidhaa kwa kuleta ahueni au makali unapopungua au kuongeza.”

Mikoa inayoongoza

Jiji la Dar es Salaam linaloongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu Tanzania na fursa nyingi za kibiashara pia ndiyo inayoongoza kwa kuwa na waajiriwa wengi katika sekta binafsi Tanzania kwa kubeba asilimia 33.8.

Mkoa wa Morogoro ndiyo unashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya waajiriwa kwa asilimia 8 ikifuatiwa na Arusha yenye asilimia 5.2 ya waajiriwa wote Tanzania, Mbeya inafuata kwa kuwa na asilimia 4.7 ya waajiriwa wote nchini, Mwanza inabeba asilimia 4.5, Tanga asilimia 4.4 na Kilimanjaro asilimia 4.1.

Mikoa yenye waajiriwa kiduchu

Kwa upande wa Tanzania Bara, Mkoa wa Katavi na Songwe ndiyo zinaongoza kwa kuwa na waajiriwa wachache kuliko sehemu yoyote ikibeba asilimia 0.6 na 0.8 mtawaliwa.

Mikoa hii inafuatiwa kwa karibu na Simiyu yenye asilimia 1.1, Rukwa asilimia 1.2, Njombe asilimia 1.3, Geita asilimia 1.4 huku Tabora na Lindi zikifuata kwa kuwa na asilimia 1.5 kila moja.

Sekta vinara

Ripoti hii inabainisha kuwa, asilimia 55.7 ya watu wanaofanya kazi katika sekta ya mawasiliano na habari wanalipwa Sh700,000 na kuendelea, sekta ya maji ikifuata kwa asilimia 51.2 ya waajiriwa wake hulipwa kima hicho cha mshahara.

Sekta nyingine inayolipa wajiriwa wake wengi kima hiki cha mshahara ni ufundi, sayansi, shughuli za kitaaluma (asilimia 50.5), fedha na bima (asilimia 50.4).

Sekta ambazo zinalipa kiwango kidogo zaidi cha mshahara ni wasaidizi wa maofisini ambacho ni asilimia 41.1 na viwandani asilimia 39.4 wote kwa pamoja wanalipwa chini ya Sh200,000.