Saudi Arabia ardhi chungu kwa Al Ahly, Zamalek yatwaa ubingwa

Riyad. Kwa mara ya pili mfululizo, ardhi ya Saudi Arabia imeendelea kuwa chungu kwa Al Ahly baada ya jana kupoteza taji la Caf Super Cup mbele ya watani wa jadi Zamalek baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Mwaka uliopita pia, Al Ahly ilifungwa katika fainali ya kuwania taji hilo na USM Alger ya Algeria kwa bao 1-0 katika mechi iliyochezwa hukohuko Saudi Arabia kwenye Uwanja wa King Fahd.

Refa Mutaz Ibrahim kutoka Libya alilazimika kuamuru mikwaju ya penalti itumike kumsaka mshindi baada ya dakika 90 za mechi hiyo iliyochezwa katika Uwanja wa Kigdom Arena huko Riyadh, Saudi Arabia kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Wessam Abou Ali alitangulia kuifungia bao Al Ahly katika dakika ya 44 kwa mkwaju wa penalti lakini dakika 33 baadaye, Nasser Mansi aliisawazishia Zamalek na kufanya mechi hiyo kwenda kwenye mikwaju ya penalti ambayo ilikuwa na neema upande wa Zamalek.

Waliofunga penalti nne zilizoipa ushindi Zamalek ni Abdallah El Said, Hamza Mathlouith, Nasser Mansi na Hossam Abdelmaguid.

Rami Rabia, Omar Kamal na Taher Mohamed ndio waliofunga kwa upande wa Al Ahly na waliokosa ni Attiyat Allah na Wessam Abou Ali.

Hilo lilikuwa taji la tano la Caf Super Cup kwa Zamalek baada ya kulitwaa pia 1994, 1997, 2003 na 2020.

Al Ahly bado inaendelea kushikilia rekodi ya kuwa timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi zaidi ikichuchua mara nane ambazo ni 2002, 2006, 2007, 2009, 2013, 2014 na 2021 mara mbili.