Sau Kilimanjaro yapata safu mpya ya viongozi

Moshi. Chama cha Sauti ya Umma (Sau) kimekamilisha uchaguzi wake katika Mkoa wa Kilimanjaro kikimchagua Isack Kireti kuwa mwenyekiti wa mkoa huo, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Machi 2, 2025 mjini Moshi, Mohamed Amir alichaguliwa kuwa katibu wa chama hicho Kilimanjaro huku Gadiel Kisima akichaguliwa kuwa katibu mwenezi.

Wengine waliochaguliwa ni Richard Shangau ambaye anakuwa naibu katibu, Simon Mathari (mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa) na Victor Paradiso (mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa).

Akizungumza leo Jumatatu, Machi 3, 2025, kuhusu uchaguzi huo, katibu wa chama hicho aliyechaguliwa, Mohamed Amir amesema wamekamilisha uchaguzi na sasa kilichobaki ni kujipanga na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu.

“Niwashukuru wanachama wenzangu kwa kuniamini na kunipa nafasi ya ukatibu, tayari tumeunda timu kwa ajili ya kusimamia mapambano kuelekea uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais,” amesema Amir.

Ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kukipambania chama hicho kupata wawakilishi.

“Kwa sasa tumepata uongozi, niombe wanachama watuunge mkono na niombe sasa wakati wa uchaguzi utakapofika wajitokeze kugombea na wale watakaopitishwa kugombea nafasi, wote kwa umoja wetu tuwaunge mkono ili tushinde,” amesema Amir.

Mwenyekiti wa Sau Mkoa wa Kilimanjaro, Isack Kireti amewataka wanachama wote kushirikiana kukijenga chama hicho na kukivusha katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais, baadaye mwaka huu.

“Chama chetu ni cha kidemokrasia, tuko imara na tumejipanga kikamilifu katika uchaguzi mkuu mwaka huu, niwaombe wanachama wenzangu tujipange vema na uchaguzi ili kushinda na kuleta mabadiliko chama kwa Taifa letu,” amesema Kireti.