SAS Logistics Ltd yaongoza njia katika umahiri wa sekta ya usafirishaji mizigo nchini

Dar es Salaam. Kila mtu anaweza kuwa msafirishaji wa bidhaa, lakini si kila msafirishaji atakufikishia mzigo ukiwa salama kama inavyotakiwa kama anavyofanya SAS Logistics Ltd.

Ikiwa na uzoefu wa zaidi ya miongo mitano sokoni, SAS Logistics Ltd imeendelea kukua huku ikijijengea heshima na weledi katika sekta ya usafirishaji nchini.

Wiki iliyopita, kampuni hiyo ilishinda tuzo mbili za ‘Kampuni Kinara ya Usafirishaji Mizigo inayozingatia Usalama’ na ‘Kampuni Bora ya Usafirishaji Mizigo’ katika Mkutano wa Wadau wa Usafirishaji Mizigo Ukanda wa Afrika Mashariki (EACC) uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mlimani City. Tuzo hizi zinadhihirisha jitihada zisizo na kikomo na uchapakazi wa kampuni hiyo.

Chini ya Ofisa Mkuu wa Biashara wa SAS Logistics Ltd, Alex Lugendo, kampuni hiyo imeendelea kuacha alama katika sekta ya usafirishaji mizigo.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Lugendo anaeleza mambo mengi yanayohusu historia ya kampuni, ushiriki wake katika tuzo hizo na biashara yake kwa ujumla. Mazungumzo hayo yalikuwa kama ifuatavyo:

Swali: Tuelezee kwa ufupi kuhusiana na SAS Logistics Ltd! Mnajishughulisha na nini?

Lugendo: SAS Logistics Ltd ni kampuni kongwe inayojishughulisha na usafirishaji wa mizigo kwa njia ya barabara iliyoanzishwa miaka 1970 na Seif Abdallah Said (SAS), ambaye ndiye aliyeasisi jina la kampuni.

Ili kukuza biashara hiyo, mtoto wake wa kiume, Salim Seif El-Busaidy, ambaye hivi sasa ndiye Mkurugenzi Mkuu, aliiendeleza zaidi na ilipofika mwaka 2006 alibadili mifumo ya kiutendaji ili  kuhakikisha kampuni inakuwa shindani katika sekta ya usafirishaji.

Tunasafirisha mizigo ya kontena na ile ya kawaida kutoka kwenye bandari zetu zote kuelekea kwenye kila kona ya nchi. Pia tumekuwa tukisafirisha bidhaa hatarishi (vilipuzi na kemikali) kwa wingi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo kuna shughuli za migodi. Pia, tumekuwa tukisafirisha mizigo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Zambia.

Sehemu ya malori 160 aina ya Scania yanayomilikiwa na SAS Logistics Ltd

SAS Logistics Ltd, kampuni iliyoanza na malori tisa pekee hivi sasa ina malori yanayofikia 160. Ni miongoni mwa kampuni chache zinazotumia malori chapa ya Scania pekee kusafirisha mizigo.

Swali: Mwaka huu, umeanza vizuri kwenu kwa kunyakua tuzo mbili katika Mkutano wa EACC. Ushindi huo una maana gani kwenu?

Lugendo: Kushinda tuzo mbili za Kampuni Kinara ya Usafirishaji Mizigo inayozingatia Usalama’ na ‘Kampuni Bora ya Usafirishaji Mizigo’ kwa mwaka huu ni jambo tunalojivunia.

Ushindi huu una maana kubwa kwetu, ni ishara mojawapo ya kukubalika na kuaminika kwetu ambako tumekujenga pamoja na wateja wetu na wadau wetu kwa miaka kadhaa sasa.

Tuzo tuliyoshinda mwaka jana ya Usalama ya EMEA SC tuliyotunukiwa na ORICA EMEA inadhihirisha shauku yetu ya kuendelea kutoa huduma bora inayozingatia weledi.

Sababu ya ushindi wetu ilikuwa ni umahiri katika ukaguzi wa shughuli  za usafirishaji, uboreshaji magari, mafunzo ya uhakiki wa Afya ya Akili mahala pa kazi na mafunzo ya mifumo ya Tehama katika usafirishaji barani Afrika. na hivyo kuifanya kampuni yetu kuwa  miongoni mwa kampuni shindani za usafirishaji zilizopo Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika.

Mafanikio haya si tu yanapeperusha bendera ya Tanzania juu zaidi lakini yanatupa nguvu ya kutaka kuendelea kufanya zaidi ya hapa, kuboresha huduma zetu, na kuhakikisha kampuni yetu inaendelea kuzingatia weledi na kuamimiwa katika sekta ya usafirishaji mizigo.

Swali: Je, nini siri ya mafanikio haya? Mlidhani kuwa mngeibuka vinara?

Lugendo: Niseme wazi kuwa siri ya mafanikio haya ni kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na ushirikiano wa wafanyakazi wetu. Kujifunza kutoka kwa wengine imekuwa siri nyingine kubwa ya ukuaji wetu. Mwaka jana, timu yetu ilitembelea Afrika Kusini, Australia na China kujifunza namna gani wenzetu wanafanya ufuatiliaji wa mizigo, na taratibu za maswala ya  forodha na mbinu za usafirishaji salama wa mizigo.

Kujitolea na uthubutu wa  wafanyakazi wetu  ndiyo chanzo cha sisi kufikia mafanikio haya, na hivyo kuweza kufanikisha mipango yetu ya utendaji bora kuwa halisia  Timu yetu ndiyo kila kitu kwenye hili.

Swali: Kwa kiasi gani ushindi huu unakwenda kuboresha biashara yenu?

Lugendo: Tuzo hizi ni ushahidi wa ukuaji wetu thabiti na kielelezo cha fursa ya ukuaji wa siku zijazo. Zinanyanyua chapa ya kampuni na kutuhakikishia uongozi wa soko katika sekta ya usafirishaji mizigo inayokua kwa kasi zaidi.

Tunapanga kutumia fursa hii kukuza shughuli zetu, na kuzidi kuipamba taswira yetu na kuboresha huduma zetu, yote ikiwa ni katika kuendelea kuwa washindani na kuendana na mahitaji yaliyopo.

Swali: Hii ni mara ya ngapi mnashiriki Mkutano huu? Na nini lengo lake?

Lugendo: Hii ni mara ya pili tunashiriki, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2024 ambapo Mkutano huu ulikuwa unafanyika nchini kwa mara ya kwanza huku mgeni rasmi akiwa Waziri Mbarawa.

Mkutano huu unawakutanisha kwa pamoja wadau wa sekta ya usafirishaji na mamlaka za udhibiti kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki kujadili mambo mbalimbali ikiwamo changamoto, fursa na mikakati ya ustawishaji wa sekta. . Tuzo ni sehemu ya mkutano huu ambapo kampuni zilizofanya vyema kwa mwaka husika hutambuliwa na kutunukiwa.

Swali: Mnadhani mambo gani mmeyachukua kama masomo katika hafla hiyo?

Lugendo: Tulichoondoka nacho katika mkutano huo ni kuwa sekta ya usafirishaji nchini inakua kwa kasi na kuna fursa za masoko ya nchi zisizokuwa na bandari ambayo hayajafikiwa ipasavyo.

Mkutano huo umekuwa ukitoa fursa adhimu za namna gani wadau wa sekta hiyo wanaweza kukutana na kubadilishana uzoefu huku viongozi wa masoko wakipata nafasi ya kuchagiza ubunifu mwingi na mawazo mapya.

Kama hiyo haitoshi, tulifanikiwa kukuza wafuasi wetu wa mitandao ya kijamii kwa kuwepo ukumbini na kushinda tuzo hizo kwa kishindo.

Swali: Nini mngeshauri kiboreshwe ili kuvutia washiriki wengi katika miaka ijayo?

Lugendo: Kwa kuwa masoko ya nchi nyingine za ukanda wetu yanafunguka, waandaaji wa tuzo wangeona namna ya kualika wadau wa sekta ya usafirishaji kutoka nchi zisizo na bahari ili kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kikanda.

Pia, kubadilisha waandaaji wa mkutano kila mwaka miongoni mwa washiriki kutaimarisha utengamano na ujumuishi wa wadau katika sekta. Baada ya TATOA kuandaa mkutano huu kwa miaka miwili, ni wakati sasa tupate sura ngeni.

Swali: Kutokana na ushindi huu, tutarajie nini zaidi kutoka SAS Logistics?

Lugendo: Huduma bora ndiyo kipaumbele chetu. Tunapanga kuongeza magari hadi kufikia 400 taratibu, kuhakikisha tunabakia kuwa washindani.

Pia tunajenga maghala manne Tanga na Bagamoyo, maeneo ya kimkakati ambayo Serikali inaendelea kupanua shughuli za bandari zake. Ghala moja kubwa la ukubwa wa mita za mraba 12,000 na mengine matatu ya ukubwa wa mita za mraba 4,000 kila moja. Lengo ni kusaidia jitihada za Serikali katika kukuza uchumi wa nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *