Sarakasi kuenguliwa wagombea uchaguzi serikali za mitaa

Dar/Mbeya. Vyama vya upinzani vimebainisha sababu mbalimbali, zilizotumika kuwaengua wagombea wao kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27.

Licha ya kuzibainisha, vimeendelea kusisitiza haki kutendeka ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wenye haki,  kwa wagombea wao kurejeshwa kwenye mchuano huo ili kuwapa fursa wananchi kuwa na machaguo mengi.

Sababu hizo wamedai zimewang’ata wagombea wa upinzani kwa sehemu kubwa huku wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiendelea na hatua inayofuata,  ambayo ni kusubiri kampeni za uchaguzi huo zitakazoanza Novemba 20 mwaka huu.

Miongoni mwa sababu walizozibainisha ambazo wamezikatia rufaa ni, fomu zao kuchezewa kwa kuongezwa herufi au tarakimu, kukosa kipato halali, kushindwa kujaza fomu, kuandika tarehe, siku na mwaka wa kuzaliwa.

Pia zilitajwa sababu kama kutokuwa wakazi wa eneo wanalogombea,  kukosekana mihuri na wagombea kutoandika majina matatu  na ya wadhamini wao.

Mchakato huo umeibua kilio kwa vyama hivyo vya upinzani baada ya wagombea wao kwenye vijiji, vitongoji na mitaa mingi,  kushindwa kuteuliwa na hata walipoweka mapingamizi wameenguliwa.

Mathalani, Chama cha ACT-Wazalendo kimedai wagombea wake 51,423 wameenguliwa katika uchaguzi huo kwa kigezo cha kukosa udhamini wa chama ngazi ya kata.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu na msemaji wa uchaguzi wa chama hicho, Rahma Mwita,  wagombea wao waligongewa mihuri ngazi ya kata ambayo ni ngazi yao ya chini, lakini wakaenguliwa kwa kigezo hicho cha muhuri.

Rahma amesema wagombea wa Temeke, Mkuranga, Kibiti, Rufiji, Kilimajaro na Arusha na maeneo mengine mengi wameenguliwa.

“Ni jambo la kustaajabisha kuwa katika nchi moja, wapo baadhi ya wagombea wetu wameteuliwa kwa kudhaminiwa na ngazi ya kata lakini wengine wengi wameenguliwa,” amesema Rahma.

Kilio kama hicho kimezungumzwa na Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Bara, Joseph Selasini,  aliyesema moja ya sababu zilitajwa za kuenguliwa wagombea wao ni ujazaji wa fomu kukosewa.

“Wengi waliokataliwa ukiangalia unakuta majina yamekosewa, muhuri kukosewa, mtaa kukosewa lakini ni mambo ambayo tulishajadili na kukubaliana yasiwepo kwa sababu jina la mtu au chama ukikosea herufi moja si sababu kumfanya mtu asigombee,” amesema.

Amesema sifa za kugombea zipo kwa mujibu wa Katiba ikiwemo kuwa raia wa Tanzania, kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza na umri usipongua miaka 18 na awe hadaiwi kodi.

“Sababu zingine zinazotumika kuwaondoa ni mihuri kwa sababu muongozo unasema kuwe na muhuri wa chama wa ngazi ya msingi,  sasa kuna mkanganganyiko kwa sababu kuna vyama ngazi za msingi si tawi kama ilivyo CCM, kuna vyama ngazi ya msingi ni kata,” amesema

Amesema watu waliopigiwa mihuri ya kata wameondolewa na inakuwa si sahihi wanataka kulazimisha chama ambacho hakijafika ngazi ya kijiji kiwe na muhuri wa kijiji.

Amesema jambo la tatu liliowaengua ni kutokuwa na  kazi maalumu ya kuwawezesha kuingiza kipato. Amesma  ni hoja  yenye mkanganyiko kwa sababu kuna walioandika kazi yao ni ujasiriamali wameenguliwa na wengine waliojaza hivyo hivyo wameteuliwa.

“Kuna vyama vingine wameandika ujasiriamali wameachwa kwa sababu ujasiriamali ni biashara na ni kazi. Huwezi kusema wafayabisahara wakatazwe kugombea na kuna walioenguliwa bila kupewa sababu,”amesema Selasini.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya amesema maeneo mengi malalamiko yao yametupwa nje na wale wachache waliopitishwa wamepigiwa simu jana usiku kuwa wameenguliwa.

“Wameenguliwa tena licha ya kwamba majina yao yalishapita na muda wa mapingamizi umeshapita,” amedai.

Amesema sababu ya kuenguliwa kwao ni kushindwa kujaza fomu kwa kukosea kuandika nafasi wanayogombea, akitoa mfano wa  mgombea nafasi ya uenyekiti Kijiji cha Kaliua aliyeenguliwa jana usiku.

“Kosa lake ameambiwa alitakiwa aandike Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kaliua, kwa akili ya kawaida hauhitaji kusoma angeandika anagombea nafasi ya mwenyekiti wa halmashauri watu wangemtafsiri tofauti,  kwa sababu kuna kijiji cha Kaliua na Halmashauri ya Kaliua,” amesema. 

Ilichokisema Chadema

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, amesema baadhi ya wagombea wao wameenguliwa kwa sababu wadhamini waliowadhamini hawakuandika majina matatu.

“Hoja ambayo haipo kwenye kanuni za uchaguzi. Mfano mtu kaandika John E Mrema wanawaengua na wanataka waandike majina yote kama John Emmanuel Mrema,” amesema.

Amesema sababu nyingine wasimamizi wamedai wagombea wao hawakudhaminiwa na chama cha siasa na pia kuwapo kwa maeneo yaliyojazwa kwa mkono.

“Kuna sababu nyingine ambayo haieleweki ya jumla wanasema hawajakidhi vigezo lakini hawasemi ni kigezo gani wakati kanuni ya 16 imeweka wazi ni sababu zipi akikosa anaweza kuenguliwa,” amesema.

Amesema wagombea wao wengi wa Jiji la Dar es Salaam,  wameenguliwa kwa kigezo cha kukosa kipato halali cha kujiingizia huku akieleza wagombea wao waliojaza ujasiriamali walielezwa hiyo si kazi halali.

“Inashangaza sana wajasiriamali hawa hadi walipewa vitambulisho vya umachinga na wanalipa kodi Sh20,000 leo wanaambiwa hiyo si kazi halali inashangaza. Lakini kuna wagombea wa vyama vingine wamejaza ujasiriamali na wameteuliwa,” amesema.

Mwananchi limezungumza na mchambuzi wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya, Dk Balozi Morwa kujua maana ya ujasiliamali ambapo amesema ni shughuli yeyote halali inayomuajiri mtu na kumpatia kipato cha uhakika.

“Unatakiwa kufanya kazi halali kama vitu unavipata kwa njia halali na si kwa wizi. Kuibuka kwa shughuli za ujasiriamali kunatokana na kukosekana kwa ajira kwa watu wengi walioenda shule,” amesema.

Amesema kuanzisha ujasiriamali si dhambi kwani hata Serikali haiwezi kuajiri watu wake wote na ni ajenda ya kimataifa isipokuwa watu wanatakiwa kuzingatia taratibu zote ikiwemo kulipa kodi.

Maelezo ya Tamisemi

Kutokana na vilio hivyo, Mwananchi limezungumza na Mwanasheria kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kadete Mihayo ambaye amesema uchaguzi huo unaendeshwa kwa kuzingatia kanuni na wasimamizi wasaidizi wanaolalamikiwa,  wanapaswa kuendesha shughuli hiyo kwa kuzingatia kanuni hizo.

“Uchukuaji na urejeshaji fomu ni takwa la kanuni na anatakiwa kubaki na nakala yake. Malengo ya nakala  ni kubaki na kumbukumbu ya kile ulichokijaza na kuhakikisha nakala yako imepokelewa na yakitokea malalamiko kama hayo uwe na kitu cha kuonyesha,” amesema.

Mbali na hilo, Kadete amesema kanuni inaeleleza asiyeridhika na uamuzi ya msimamizi msaidizi wa uchaguzi, aweke pingamizi.

“Kinachotakiwa ni kuandika pingamizi kuwasilisha kwa msimamizi msaidizi ukimtaka kupitia upya uamuzi wake kama unaona kuna eneo hakulifanya sawa,” amesema.

Amesema msimamizi akishapokea mapingamizi anatakiwa kuyatolea uamuzi na kama umepeleka mapingamizi na hujaridhika na aliyefanya uteuzi kanuni zinamtaka asiyeridhika na uamuzi kwenda kukata rufaa kwenye kamati za rufani.

“Kanuni zetu zimeanzisha kamati ya rufani,  ni chombo huru na wajumbe wake hawajashiriki kwa namna yoyote kwenye  mchakato wa uteuzi na tulifanya hivyo ilikuwa na dhana ya uhuru na uwazi,” amesema Kadete.

Mwanasheria huyo amesema kamati hiyo ina siku nne tangu uamuzi ulipotolewa na msimamizi kupokea hizo rufani kisha kuzitolea uamuzi. Kwa mujibu wa Tangazo la Uchaguzi, rufaa hizo zinasikilizwa kuanzia Novemba 10-13 mwaka huu.

CCM yatamba kushinda

Wakati huohuo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla  akizungumza katika uwanja wa CCM Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani leo Jumatatu, amesema kuna maneno yanasemwa mitandaoni kuwa upinzani wamewekewa mapingamizi na au wameenguliwa lakini, hata CCM imewekewa mapingamizi.

“Wanafanya hadaa, upotoshaji wa takwimu feki na kujisahaulisha kwamba hata wagombea wa CCM wamewekewa mapingamizi. Juzi nilisema tunaamini Tamisemi itatenda haki kwa vyama vyote kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki na atakayeshinda atangazwe kwa haki,” amesema Makalla na kuongeza:

“Kwa hesabu zetu na wagombea tuliowaweka, tunaamini CCM tutashinda kwa haki. Kwa hiyo rufaa zinaendelea, baada ya uteuzi wa wagombea CCM kitatoa taarifa baadaye.”

‘Tunasubiri rufaa’

Wakati Chadema mkoa wa Mbeya kikisisitiza kuwasilisha rufaa za wagombea wao baadhi ya wsimamizi wasaidizi wa mchakato huo wamesema hadi mchana wa leo Jumatatu hawajapokea rufaa yoyote kutoka chama chochote.

Jana Novemba 10, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema mkoani hapa (Bavicha), Elisha Chonya aliliambia Mwananchi yapo baadhi ya maeneo ambayo wagombea wao walikatwa bila sababu kwa kuwawekea pingamizi akieleza kuwa watakata rufaa na wanasubiri majibu tarehe ya mwisho.

Hata hivyo, msimamizi msaidizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Anakreti Michombelo amesema hadi mchana analipozungumza na Mwananchi hakuwa amepokea rufaa yoyote kutoka chama chochote akieleza wanaendelea kusubiri kwani muda bado unaruhusu.

Kwa upande wake Mohamed Fakii ambaye anasimamia Wilaya ya Mbeya Mbeya, amesema bado hajapokea rufaa yoyote akieleza kamati yake bado inasubiri hadi tarehe ya mwisho ambayo ni Novemba 13.

“Hapa kwangu sijapokea rufaa kutoka popote japokuwa mchakato si wa leo tu bali hadi Novemba 13,  hivyo ofisi zitakuwa wazi muda wote kuhakikisha haki inatendeka kwa wote” amesema Fakii.