Sampuli zaidi ya 600 za mboga kufanyiwa utafiti Tanzania

Arusha. Zaidi ya sampuli 600 za mbogamboga hapa nchini zimeanza kufanyiwa utafiti wa awali wa utambuzi kujua uwezo, sifa na tabia zake ili kuzikusanya na kuhifadhiwa katika benki ya mbegu.

Sampuli hizo ni kati ya  1,700 zilizokusanywa kwa ajili ya utunzaji rasilimali mimea za mbogamboga za asili ili zitumike katika uboreshaji wa lishe ya watoto na watu wazima.

Hayo yamebainishwa Machi 23, 2025 na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Taifa cha Nasaba za Mimea, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Dk Mujuni Kabululu wakati wa uzinduzi wa mradi wa awamu ya pili wa utunzaji wa biaonuai za mbegu za mboga wa Taiwan African Vegetable Initiative (TAVI II).

Amesema katika mradi wa TAVI awamu ya kwanza ulioanza mwaka 2021 hadi 2024 wameweza kukusanya sampuli za mbogamboga zaidi ya 1,700 kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Tabora na Zanzibar.

“Katika mradi wa awamu ya kwanza, utafiti wa awali unaendelea katika sampuli zaidi ya 600 zipo shambani kwa ajili ya utafiti wa awali kujua uwezo, sifa na tabia zake. Baada ya hapo tutashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) ambao wana jukumu la kuzalisha mbegu bora na wataanza kuzizalisha,” amesema.

Amesema mradi huo wa kwanza ulihusisha nchi nne ambazo ni Tanzania, Benin, Eswatini na Madagasca na zaidi uliangazia kuimarisha benki za mbegu na kuhakikisha zinakusanywa na kuhifadhiwa katika benki ili zisipotee.

Awali akizindua mradi huo, Mratibu wa Miradi ya Kimataifa inayofadhiliwa na Taiwan kutoka Kituo cha Utafiti wa mbogamboga na matunda cha kimataifa cha World Vegetable Center, Dk Sophia Chan amesema mradi huo wa miaka mitatu utaanza mwaka 2025 hadi 2027.

Amesema mradi huo utatekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya na Eswatini ambapo watoto 80,000 na wakulima 15,000 watanufaika na mradi huo ambao utaongeza usalama wa chakula na lishe.

Amesema licha ya nchi nyingi za Afrika kuwa na mbegu za asili ikiwemo za mbogamboga bado matumizi yake yako chini, hivyo kupitia mradi huo kutaanzishwa mashamba darasa na elimu ya lishe kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji kwa umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *