Sampuli za walioteketea kwenye ajali ya malori zapelekwa kwa mkemia

Morogoro. Ndugu wa marehemu wawili waliofariki kwenye ajali ya malori yaligongana na kuwaka moto eneo la Nanenane barabara ya Morogoro – Dar es Salaam wamejitokeza na tayari sampuli zimeshapelekwa kwa mkemia ili ndugu hao waweze kutambua miili ya wapendwa wao.

Akizungumza na Mwananchi Digital Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama amesema kutokana na hali ya miili hiyo kuteketea  kabisa kwa moto haikuwa rahisi kuitambua kwa kuangalia kwa macho hivyo ilibidi vipimo vya kisayansi vifanyike ili kila mwili uwezo kutambuliwa na ndugu.

“Baada ya kujitokeza watu wanaodai kuwa na uhusiano na marehemu hao ilibidi tuchukue sampuli kutoka kwa watu hao na sampuli kutoka kwenye mabaki ya miili ya marehemu na kuipeleka kwa mkemia, majibu yatakayotoka huko ndio tutaweza kutambua ndugu wa marehemu hao,” amesema Kamanda Mkama.

Amesema baada ya kutambua mabaki hayo ya miili ya marehemu tutayakabidhi kwa ndugu kwa ajili ya taratibu mazishi.

Malori mawili yaliyoteketea kwa moto baada ya kugongana uso kwa uso eneo la nane nane barabara ya Morogoro -Dar es Salaam wiki iliyoisha na kusababisha vifo vya watu watatu. Picha Hamida Shariff, Mwananchi

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Machi 4 mwaka huu eneo la Nanenane nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro baada ya lori lililobeba tenki mbili za mafuta ya petroli na diseli kugongana uso kwa uso na lori lenye mizigo na kuwaka moto

Katika ajali hiyo watu watatu akiwemo dereva wa lori la mafuta walifariki na miili yao kuteketea kabisa kwa moto, kiasi cha kutotambulika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *