Samia awatega Ma-DC, DED, watumishi wanaotaka ubunge

Dar/Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan, amewataka wakuu wa wilaya (DC), wakurugenzi wa halmashauri (DED) na watumishi wengine wa Serikali wanaotaka kujitosa katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu kutoa taarifa mapema, la sivyo watakosa vyote.

“Kuna Ma-DED wangu, wakuu wa wilaya… wana hamu sana kurudi kwa wananchi. Nilimwambia Katibu Mkuu Kiongozi apeleke mwongozo wa Serikali za mitaa, nadhani Waziri (Mohamed Mchengerwa – TAMISEMI) umeupata kwamba yeyote mwenye nia ya kugombea atuambie mapema,” amesema Rais Samia.

Rais Samia anatoa angalizo hilo kipindi ambacho vuguvugu la uchaguzi katika majimbo limepamba moto, huku viongozi wakiwemo Ma-DC, DED, wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa taasisi na mamlaka mbalimbali wakionyesha nia ya kuwania ubunge.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (Alat) katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 11 Machi, Machi 11, 2025. Picha na Ikulu

Katika baadhi ya maeneo, minyukano imekuwa mikubwa, hali iliyowafanya viongozi wakuu wa CCM, akiwemo Rais Samia, kwa nyakati tofauti kuonya kuhusu kampeni za mapema, huku wakisisitiza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua.

Tofauti na maelekezo ya Rais Samia, mwaka 2019, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli, aliwaonya baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi waliokuwa wakijipanga kusaka ubunge katika Uchaguzi Mkuu 2020, ambapo aliwafananisha na watu wenye tamaa.

“Hao wanaojipanga kugombea uchaguzi ujao (mwaka 2020) wakiwemo wakurugenzi, sijui Ma-RC (wakuu wa mikoa) na wakuu wa wilaya… waacheni tu, wakagombee, nyie chapeni kazi zenu. Nataka niwahakikishie kwamba huwezi kuwa na vyote, Watanzania tupo milioni 53,” alisema Magufuli.

Leo Jumanne, Machi 11, 2025, akifungua Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Rais Samia amesema hatua hiyo itawezesha Serikali kujaza nafasi zao mapema kwa kuwapandisha watumishi walioko chini yao.

Amesisitiza kuwa wasingependa kuona wakati wa mchakato wa utoaji wa fomu, watendaji wote wanaacha ofisi na kuzikimbilia huku Serikali za mitaa zikibaki hazina viongozi au wasimamizi.

“Mnabakia kujaza watu wasiokuwa na uwezo, lakini tukijua mapema tutaanza kujaza watu katika nafasi hizo kwa kuwapa miongozo na kuwafanyia mafunzo ili kuwa tayari kukabiliana na uchaguzi,” amesema Rais Samia.

“Sasa usiposema mapema, ukija kuchukua fomu, umekosa yote. Umekosa fomu, umekosa cheo na nafasi yako utaiacha. Ukituambia mapema, ukajaza au umejaribu na umeshindwa, wewe ni mzuri basi tutakufikiria tena. Ukituambia mapema, umekosa yote, my dear (mpendwa wangu),” ameongeza Rais Samia.

Amesema Serikali haitaki kufanya uchaguzi kwa kubahatisha, bali inataka kufanya uchaguzi tukiwa na watu makini kwenye field.

“Kama ni siri, leo imekuwa dhahiri hapa hapa… nimewaibia siri. Wanaotaka kuomba ridhaa, nawatakie kila la kheri,” amesema Rais Samia.

Tumewanyoosha watendaji

Katika mkutano huo, Rais Samia amesema Serikali imepata alama 85 kati ya 100 katika kuwaondoa watendaji wa Serikali za mitaa wasiotimiza malengo yaliyokusudiwa.

Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, amekuwa akitoa mikeka mingi ya mabadiliko katika Serikali za mitaa kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya hadi halmashauri, si kwa raha au kwa kupenda, bali kutafuta watendaji bora watakaosimama na Serikali ili kutekeleza majukumu ipasavyo.

Mikeka hiyo anayoizungumzia Rais Samia ni hatua yake ya uteuzi na utenguzi wa watendaji mbalimbali wa ngazi hizo, hasa wakurugenzi wa halmashauri, majiji na manispaa. Tangu kushika wadhifa huo, Rais Samia alijipambanua wazi kuwa asiyeenda na kasi, basi kalamu itaongea.

“Sasa kama maksi (alama) ni 100, tupo kwenye 85, tumeshanyooka, zimebaki alama 15… tutakwenda kunyooshana polepole hadi wote tusimame kwenye njia sahihi,” amesema Rais Samia.

Mwaka 2021, wakati akifungua mkutano, alizitaka mamlaka hizo kushughulikia kero za usimamizi madhubuti kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), sambamba na kuwachukulia hatua maofisa wabadhirifu.

“Ndiyo ile niliyosema ‘mikeka, mikeka’… ili kuchuja watumishi wabadhirifu na wazembe wote. Tumechuja, tumefikia asilimia 85,” amesema Rais Samia.

Ataka umakini ukusanyaji mapato

Katika maelezo yake, Rais Samia amesema bado kuna changamoto katika ukusanyaji wa mapato, akifichua kuwa licha ya kuwepo kwa mifumo halali, bado kuna watu wasio waaminifu wanaounda mifumo ya pembeni inayokusanya fedha ambazo haziingii serikalini.

“Waziri na wakurugenzi, nataka muwe macho katika hili, kwa sababu fedha hizi zikikusanywa zitaingia katika mfumo halali na zitakwenda kufanya maendeleo. Tukiachia zikaenda mikono mingine, maendeleo yetu yatadorora,” amesema Rais Samia na kuongeza;

“Mheshimiwa Waziri (Mchengerwa), kama mmewabaini hawa watu, tafadhali sana… lile jicho lako la huruma hapa hapana… Ukishindwa kuwachukulia hatua, nitakuita na kukuuliza umefanya nini? Hukufanya kitu? Mimi nitafanya kwako na kwao, wao uliowasemehe na wewe uliyewasamehe,” amesema Rais Samia.

Amezitaka halmashauri kujipanga zaidi katika ukusanyaji wa mapato, hasa kwa kuziba mianya ya risiti feki.

Pia, amezitaka halmashauri kusimamia vibali vya ujenzi ili viendane na uhalisia wa jengo litakalojengwa.

“Kuna nyumba za ajabu zinajengwa, mfano mzuri ni Kariakoo, jijini Dar es Salaam au katika halmashauri nyingine. Mtu anapewa kibali cha ujenzi wa nyumba, lakini nyumba anayojenga anaweka na ‘lumbesa’ juu,” amesema Rais Samia.

“Lumbesa zimeacha sasa kuwa za mazao ya kilimo, zinakwenda katika ujenzi. Twendeni tukasimamie sheria zetu ambazo wakati mwingine tunazivunja wenyewe,” ameongeza.

Awali, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa, amesema pamoja na ukusanyaji wa mapato kwenda vizuri, bado kuna watu wilayani Meatu, Simiyu wanaotengeneza risiti bandia, na kusababisha hasara kwa halmashauri.

“Nimewaelekeza watendaji katika eneo hili kuhakikisha wanaohusika kuchukuliwa hatua mara moja. Lakini pia, tulipata taarifa kule Mbeya kutoka kwa mkurugenzi kwamba vibanda vilivyopo katika halmashauri, baadhi yao walikamatwa kwa kughushi risiti na kusababisha upotevu wa mapato,” amesema Mchengerwa.

Naye Mwenyekiti wa Alat, Murshid Ngeze, amesema kila mwaka wanafanya mkutano huo, lakini safari hii wameamua kushirikisha wenyeviti wa Serikali za mitaa kwa kuwa jumuiya hiyo inafanya kazi hadi vijijini na mitaa.

Kwa mujibu wa Ngeze, mkutano utajadili taarifa ya mapato na matumizi ya Alat, bajeti ya 2025/26, taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja na masuala mbalimbali ya mkoani kwenye Serikali za mitaa.

“Alat kwa sasa tumeimarika, tofauti na huko nyuma ambako taarifa za mapato na matumizi hazikuwa zikiwasilishwa. Sasa hivi tumeimarika na taarifa zipo wazi, tupo vizuri,” amesema.

Mbali na hilo, Ngeze amemwomba Rais Samia kurudisha utaratibu wa wiki ya Serikali za mitaa ili halmashauri zionyeshe shughuli zinazofanyika zitakazowezesha umma wa ndani na nje ya nchi kutambua kazi zao.