Samia atua zigo nafasi ya Jaji Mkuu

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema hana dhamira ya kugombana na majaji, hivyo amedhamiria kumuacha Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma aliyebakiza miezi michache, aende kupumzika.

Amesema hayo leo Jumamosi Aprili 5, 2025 alipozindua majengo matatu ya makao makuu ya Mahakama Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama na nyumba za majaji zilizojengwa katika eneo la Iyumbu, jijini Dodoma.

“Natambua kuwa umebakisha miezi michache kustaafu, na mimi sina tena dhamira ya kugombana na majaji wale, nina dhamira ya kukuacha ukapumzike. Kwa hiyo, majaji jipangeni, jaji huyu anakwenda kupumzika,” amesema.

Samia amesema: “Jaji Mkuu niseme umefanya mageuzi makubwa ya Mahakama yetu. Pamoja na msukumo wa Serikali, lakini mageuzi ya fikra, kusimamia na kuleta mageuzi tunayoyaona leo ni mabadiliko makubwa ndani ya mhimili huu.”

“Sasa Katibu Mkuu Kiongozi (Dk Moses Kusiluka) nimekuona uko hapa, umenipangia kutoa nishani kwenye sherehe za Muungano, naomba uniongezee nishani moja ya Jaji Mkuu wa Tanzania,” amesema.

Muonekano wa nje wa Jengo la Makao makuu ya Mahakama kuu ya Tanzania jijini Dodoma

Juni, 2023 ulizuka mjadala kuhusu ukomo wa muda wa utumishi wa Jaji Mkuu, Profesa Juma ukiibua dosari katika Katiba ikielezwa vifungu vilivyopo katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 vinaleta mkanganyiko wa kisheria juu ya suala hilo.

Mjadala huo ulitokana na taarifa kuwa, Rais Samia amemuongezea muda Profesa Juma wa kuendelea kuwa Jaji Mkuu, jambo lililopingwa na wadau wa sheria, akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani, Stella Mugasha.

Kutokana na uamuzi huo wa Rais Samia, Jaji Stella alimwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel akieleza kilichofanywa ni uvunjaji wa Katiba na kutozingatia misingi ya sheria.

Barua hiyo yenye kurasa 10, nakala yake ilitumwa kwa Rais, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Jaji wa Rufani, Augustine Mwarija, Jaji Kiongozi, Mustapher Siyani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi na Katibu Mkuu Kiongozi.

Hoja ya Jaji Stella msingi wake ni matakwa ya Katiba ya Tanzania, Ibara ya 120 (1) inayosema: “Kila Jaji wa Mahakama ya Rufani atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka 65, lakini masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila kuathiri masharti yafuatayo katika ibara hii.

Hata hivyo, uamuzi wa Rais Samia ni kwa mujibu wa Ibara ya 120 (3) ya Katiba ya Tanzania, inayompa mamlaka mkuu wa nchi kumwongezea muda Jaji wa Mahakama ya Rufani hata akifikisha kipindi cha kustaafu, iwapo ataona kuna manufaa ya umma.

Kulingana na Ibara hiyo, “Iwapo Rais ataona kwa ajili ya manufaa ya umma inafaa Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyetimiza umri wa miaka 65 aendelee kufanya kazi na muhusika akakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi. Rais anaweza kuagiza aendelee kwa muda wowote atakaoutaja.

Maelezo ya vifungu hivyo, ndiyo yaliyoibua mkanganyiko ulioibua dosari katika Katiba, kwa mujibu wa wataalamu wa sheria wakiwemo waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali katika sekta hiyo.

Profesa Juma alitimiza miaka 65, Juni 15, 2023. Alizaliwa Juni 15, 1958, Musoma mkoani Mara.

Aliteuliwa katika wadhifa huo Septemba 10, 2017 na aliyekuwa Rais wa wakati huo, Dk John Magufuli, baada ya Jaji Mkuu, Mohamed Chande kustaafu.

Mahakama za mwanzo

Rais Samia ametaka kutupiwa jicho baadhi ya mambo ya Mahakama za mwanzo na kutofungwa na masharti katika mahakama hizo.

Amesema Ibara ya 107A ya Katiba kifungu kidogo cha pili kinaeleza:

“Katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo, yaani:

Kifungu kidogo (e): “Kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.”

Amewaomba majaji hao,  ibara hiyo izingatiwe hasa katika Mahakama za mwanzo.

Rais Samia amesema anatambua kuwa wameongeza mahakimu na wataalamu wengine, lakini ikiwa Mahakama za mwanzo zitajifunga na masharti ya kiufundi zitashindwa kufikia lengo la kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Amesema sababu hiyo itawafanya wananchi kukimbilia ofisi za mikoa na wilaya au Chama cha Mapinduzi (CCM), lakini kumbe wangeenda mahakamani wakapata vitu wanavyovihitaji.

“Ni lazima tuwajengee wananchi kwamba, mahakama ndiyo kimbilio lao la kwanza, la mwisho na la kipekee katika kudai haki,” amesema.

Uadilifu wa majaji

Ametaja jambo jingine la msingi ni uadilifu kwa majaji na watendaji wa mahakama ili kujenga imani kwa chombo hicho cha kutoa haki kwa Watanzania kwa mahakama zao na kulinda heshima ya mhimili huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama, jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na jengo la makazi ya majaji, jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

“Tuendelee kuhakikisha kuwa miradi ya ujenzi inakuwa na thamani ya fedha. Lakini dhana ya mahakama kuwa people centered (inayolenga watu) ionekane kwa vitendo na hapa napongeza kituo cha huduma kwa wateja,” amesema.

Awali, Jaji Mkuu Profesa Juma amesema wakati mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya miundombinu ulipoanza mwaka 2016/17 kulikuwa kunahitajika ujenzi wa mahakama 104.

Amesema majengo machakavu yaliyohitaji ukarabati yalikuwa 24 na mengine 11 ya mahakama za wilaya yalikuwa katika hali nzuri kati ya wilaya 139.

Profesa Juma amesema hadi kufikia Desemba 2025 kutokana na jitihada zinazoendelea hali kwa majengo hayo itabadilika.

Amesema changamoto kubwa ipo katika Mahakama za mwanzo katika kata na tarafa, ambazo watu wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma za haki.

Changamoto hiyo amesema ni lazima kufanyiwa kazi kwa pamoja hata kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kwa kujenga Mahakama za mwanzo kama inavyofanyika kwenye zahanati na huduma nyingine.

Profesa Juma amesema wamesubiri kwa miaka 104 kabla ya kupata jengo la makao makuu ya Mahakama Tanzania.

Amesema jengo hilo ni la sita kwa ukubwa duniani na la kwanza katika Bara la Afrika, akieleza mifumo ya Tehama imeboreshwa ili kazi zitakazofanyika humo kutotumia karatasi.

“Mifumo ya Tehama iliyoko ndani ya jengo hili imewekwa vifaa vya kisasa kabisa inayowezesha usimamizi wa mifumo na ufuatiliaji wa utendaji wa shughuli za kimahakama na utawala kwa nchi nzima,” amesema.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema tangu Rais Samia aapishwe Machi 19, 2021 ameanzisha  kampeni Mama Samia Legal Aids kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa kuzimudu.

Amesema tangu ianzishwe imefika katika mikoa 23. Amesema hadi Mei, mwaka huu watakuwa wamefika katika mikoa yote 31.

Katika miaka minne, amesema kumetolewa mafunzo kwa wasaidizi wa sheria kutoka 617 waliokuwepo awali hadi 2,205.

Amesema kumekuwapo ongezeko la taasisi za utoaji wa msaada wa sheria kutoka 84 hadi 377.

Kuhusu majengo

Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema miradi yote mitatu iliyozinduliwa ina thamani ya Sh185.4 bilioni.

Amesema jengo la Tume ya Utumishi wa Mahakama limejengwa kwa gharama ya Sh14.5 bilioni, huku makazi ya majaji (nyumba 48) yaliyojengwa Iyumbu yakigharimu Sh42 bilioni.

Profesa Gabriel amesema jengo la makao makuu ya mahakama lililojengwa na mkandarasi kampuni ya CRJE Afrika Mashariki limegharimu Sh129.74 bilioni.

Amesema jengo hilo ambalo lina sehemu tatu ya Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Upeo, limejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 18.9 lililo eneo la NCC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *