
LICHA ya kufunga tena baada ya siku 1,235 katika michuano ya Europa League wakati PAOK ikipoteza nyumbani kwa mabao 2-1 mbele ya Steaua București ya Romania, nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ameweka rekodi ya kucheza na kufunga akiwa na timu tatu tofauti.
Samatta ambaye mkataba wake na PAOK unamalizika Juni 30, 2025 amekuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kuweka rekodi hiyo, licha ya kwamba hakutumika katika michezo ya awali, usiku wa jana Alhamisi, mshambuliaji huyo alipewa jukumu la kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Akiwa na jezi namba 70 mgongoni mbele ya mashabiki zaidi ya 28,000 kwenye Uwanja wa Toumba mjini Thessaloniki, Ugiriki, nahodha huyo wa Stars aliwapa raha mashabiki wa timu hiyo baada ya kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 21 akimalizia pasi ya Dimitrios Pelkas.
Katika dakika ya 45+5, chama hilo la Samatta lilijikuta likienda mapumziko likiwa pungufu baada ya Taison kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu. Licha ya mabadiliko ambayo PAOK iliyafanya ili kufanya vizuri katika mchezo huo, juhudi zao ziligonga mwamba.
FC Steaua București ilitoka nyuma na kushinda mchezo huo kupitia Gheorghita na Dawa waliofunga mabao hayo katika dakika ya 50 na 60 wakiwa na wachezaji walioingia kutokea benchi.
Samatta aliyetumika kwa dakika 61 katika mchezo huo ndiye mchezaji ambaye alikuwa na ufanisi mkubwa huku akipewa alama 7 kwa upande wa wenyeji.
Mchezaji huyo ambaye huo ni mchezo wake wa pili anafunga mfululizo katika mashindano yote, mara yake ya mwisho kabla ya jana kucheza michuano hiyo na kufunga ni Novemba 25, 2021 wakati huo alikuwa akiichezea Antwerp ya Ubelgiji na ulikuwa mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya Eintracht Frankfurt.
Katika mchezo huo ambao ulichezwa Ujerumani, Samatta aliisaidia Antwerp kutoka sare ya mabao 2-2.
Mara ya kwanza nahodha huyo wa Stars kucheza michuano hiyo midogo ya Ulaya baada ya Ligi ya Mabingwa ilikuwa msimu wake wa kwanza Ulaya 2016/17 baada ya kujiunga na KRC Genk akitokea TP Mazembe.
Samatta akiwa na Genk alicheza michuano hiyo kwa misimu mitatu na kuweka rekodi kibao kabla ya kutua Aston Villa ya Ligi Kuu England, ikiwemo kufunga bao kwenye uwanja mgumu wa Liverpool, Anfield.
WENYEWE WAMEMRUDISHA
Awali, Samatta alikosekana katika michezo iliyopita ya PAOK baada ya jina lake kutoorodheshwa miongoni mwa wachezaji watakaotumika, hivyo alikosekana katika michezo 10 ikiwemo dhidi ya Manchester United (timu anayoishabikia).
Samatta alionekana kutokuwa katika mipango ya kocha wa sasa wa PAOK, Razvan Lucescu lakini nahodha huyo amepambana na sasa anaonekana kupewa nafasi na ameanza kuonyesha makali yake, jambo linalofufua matumaini mapya.
Samatta na wenzake sasa wana kazi ya kupindua meza Romania katika mchezo wa marudiano ambapo watakuwa wakisaka ushindi ili kutinga hatua ya 16 baora ambayo watakutana mshindi kati ya Lyon au Eintracht Frankfurt.
MATOKEO MENGINE
Fenerbehce 3-0 Anderlecht
Ferencvaros 1-0 Plezen
Midtjylland 1-2 Real Socieadad
Royalae Union SG 0-2 Ajax
AZ Alkamaar 4-1 Galatasaray
FC Porto 1-1 AS Roma
Twente 2-1 Bodo/Glimt
COMFERENCE LEAGUE
Celje 2-2 APOEL
Molde 0-1 Shamrock Rovers
TSC 1-3 Jagiellonia
Vikingur Reykjavik 2-1 Panathionaikos
Borac Banja Luka 1-0 O. Ljubljana
FC Copenhagen 1-2 Heidenheim
Gent 0-3 Betis
Omonia 1-1 Pafos