Salah ni mwendo wa rekodi England

Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah ameendelea kuonyesha kiwango bora ndani ya kikosi hicho kinachoongozwa na kocha, Arne Slot baada ya jana kufanya mambo makubwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Man City.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Etihad, Liverpool walikuwa wageni wa Man City ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku Mo Salah akiendelea kuweka rekodi mpya kwenye ligi hiyo ambayo imebakiza mechi tisa kumalizika.

Salah ambaye alifunga bao la kwanza pamoja na kutoa pasi ya bao la pili amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Ligi Kuu England, Premier kuhusika katika mabao zaidi ya 40 ndani ya misimu miwili tofauti.

Msimu wa 2017-2018, Salah alihusika katika mabao 42, ambapo alifunga mabao 32 na kutoa pasi za mwisho 10, huku katika msimu huu wa 2024-2025 tayari amehusika katika mabao 40 akiwa amefunga 25 kwenye Ligi Kuu na kutoa pasi za mwisho 15.

Salah ndiye mchezaji wa kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kufunga na kutoa pasi ya mwisho katika mechi zote mbili dhidi ya mabingwa watetezi ndani ya msimu mmoja, akifanya hivyo dhidi ya Man City.

Pia Salah amefikisha idadi ya mechi 49, alizofunga na kutoa pasi za mabao akiwa ligi tofauti ndani ya Ligi tano bora za Ulaya wakati Lionel Messi akiwa wa kwanza ambapo amecheza mechi 102 alizofunga na kutoa pasi za mwisho huku Cristiano Ronaldo akiwa amecheza mechi 65 alizofunga na kutoa pasi za mabao.

Mbali na Mo Salah, mchezaji mwingine aliyeweka rekodi jana ni Alexander Isak wa kikosi cha Newcastle United ambaye alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-3 iliyoupata timu yake dhidi ya Nottingham Forest kwenye Uwanja wa St. James’ Park.

Mabao mawili aliyofunga Isak yalimfanya afikishe jumla ya mabao 50 katika michezo 76 aliyocheza ndani ya Ligi Kuu ya England akiwa ndiye mchezaji wa kwanza kutoka Sweden mwenye mabao mengi EPL akimpita mchezaji wa zamani wa Arsenal Freddie Ljungberg, ambaye alifunga mabao 48.