Salah alivyovivaa viatu vya Messi katika rekodi

Billingham, England. Liverpool imeshindwa kupata matokeo ya ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa jana dhidi ya Aston Villa kwenye Uwanja wa Villa Park huku mshambuliaji wake Mohamed Salah akiandika rekodi inayofanana na Lionel Messi.

Salah ambaye aliandika rekodi mpya inayofanana na ile ya Messi ya mwaka 2015 alikuwa wa kwanza kuitanguliza Liverpool baada ya kufunga bao katika dakika ya 29 akiunganisha kwa shuti kali pasi aliyopewa na Diogo Jota.

Zilipita dakika tisa ambapo Youri Tielemans aliisawazishia Aston Villa akimalizia kwa kupiga shuti kali ambalo lilimshinda kipa wa Liverpool, Alisson Becker.

Kabla ya kwenda mapumziko Ollie Watkins aliiandikia Aston Villa bao la pili katika dakika ya 45+3 akimalizia kwa kichwa pasi ya Lucas Digne.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Liverpool ikiwa nyuma kwa mabao 2-1 kabla ya Alexander-Arnold kufunga bao la kusawazisha kipindi cha pili katika dakika ya 61.

Mpaka dakika 90 zinamalizika timu zote mbili ziliambulia pointi moja baada ya kutoka sare ya mabao 2-2.

Rekodi ya Salah

Mohamed Salah amekuwa mchezaji wa kwanza kufunga na kutoa pasi za mwisho kwenye mechi 10 tofauti katika Ligi kubwa Ulaya ndani ya msimu mmoja tangu alipofanya hivyo  Messi mara 11 msimu wa 2014-2015 alipokuwa na Barcelona.

Mabao na pasi za mwisho alizotoa Salah mpaka sasahivi zimeipa Liverpool jumla ya pointi 31 akiwa ni mchezaji wa pili kufanya hivyo kwenye Ligi Kuu ya England tangu Jamie Vardy wa  Leicester City alipofanya hivyo msimu wa 2015-2016 alipohusika kuchangia pointi 32.

Liverpool inabaki katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 61 mbele ya Arsenal ambayo inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 53 huku ikiwa na mechi moja mkononi.

Aston Villa inabaki katika nafasi ya sita ikiwa na pointi 39 ambapo mpaka sasa imeshinda mechi 10, sare mechi tisa na kupoteza mechi saba katika mechi 26 ilizocheza.

Mchezo unaofuata Liverpool itakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Anfield kukabiliana na Manchester City Februari 23, 2025, wakati Aston Villa wataikaribisha Chelsea kwenye Uwanja wa Villa Park, Februari 22, 2025