Sakata ndoa ya Manara, Zaylisa viongozi wa dini watoa mbinu kukabili migogoro

Dar es Salaam. Habari ya mjini kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa ni kuhusu yanayoendelea katika ndoa ya mwanamichezo Haji Manara (Bugati) na mkewe Zaiylisa.

Kufuatiliwa kwa ndoa hii ni matokeo ya umaarufu walionao wawili hao Manara akiwa na jina kubwa kwenye tasnia ya michezo akiwahi kuwa msemani wa vilabu vya Simba na Yanga huku Zaiylisa akiwa nyota wa tamthiliya na mitindo.

Bundi alionekana kutua kwenye ndoa hii Aprili 9, 2025 ambapo wawili hao walianza kutupiana vijembe na kutoleana siri za ndani kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutokuwa na maelewano.

Mwananchi ilimtafuta Manara kutaka kufahamu ukweli wa kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii alieleza kutokuwa tayari kuzungumzia mahusiano yake, akisisitiza alichokiandika kimetosha.
“Sipendi kuzungumzia life (maisha) yangu, nilichoandika kinatosha, kwenye hilo no comment (sizungumzii),” amesema kwa kifupi.

Kupitia ukurasa wa Instagram Zaiylisa aliandika ujumbe ulioonesha kuchoshwa kwake na mambo aliyokuwa akifanya mume wake hivyo yuko tayari kuiacha ndoa hiyo.

Haikupita muda Manara naye akaandika ujumbe akieleza namna anavyokerwa na tabia ya uchoyo ya mke wake na hawezi kuvumilia aina yoyote ya unyanyasaji kwa watoto wake.

Kitendo hiki kimebeba hisia tofauti ambapo viongozi wa dini wamekemea na siyo tu kwa wawili hao bali wanandoa wote wenye tabia za kutoleana siri.

Siyo kwa tukio la Haji na Zaiylisa pekee, viongozi hao wa dini wamesema ni laana wanandoa kutoleana siri zao hadharani pale mapenzi kati yao yanapokwisha.

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaji Nuhu Mruma amesema katika imani ya Kiislamu, kutoleana siri kwa wanandoa si utaratibu wa kawaida.

“Kwanza kabisa huwa hapendezi wanandoa kuachana na umchukiza mwenyezi Mungu, lakini kama ikifikia wameshindwana na kushindwa kuna hatua mbalimbali wanapitia na wakishindwa kuelewana basi hatimaye waachane kwa wema,” amesema.

Amesema kabla ya wanandoa hao kuachana kuna hatua zinapitiwa kwa kuwashirikisha wazazi na viongozi wa dini.

“Msipofikia kuelewana, basi mnaruhusiwa kuachana kwa talaka, mtajadiliana masuala ya maisha kama kuna watoto.

“Suala la kutoleana siri za ndani si maadili, halitegemewi kuwepo, sisi viongozi dini tunaona kiwango cha uvunjifu wa ndoa kinakuwa kikubwa,” amesema.
Amesema katika kukabiliana na hali hiyo, kupitia kwa kadhi mkuu wa Tanzania wameanzisha utaratibu wa kufundisha watu maisha ndoa kabla kuoana ili kuepusha hali hiyo.
Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhani Kitogo amesema kupitia maneno ya Mtume Muhammad amesema amelaaniwa kila mwanaume na mwanamke aishiye kwa muda kadhaa kwenye ndoa kisha kutoa siri baada ya kutengana.
“Kwa wanandoa baada ya mapenzi kuisha na kutengana, si jambo jema kutoleana siri, mtume wetu amelaani hilo.Watu wapewa somo na darasa maalumu kabla ya kuingia kwenye ndoa, wafundishwe mambo ambayo ni mwiko kuyafanya katika ndoa ikiwamo kutoleana siri baada ya mapenzi kuisha,” amesema Kitogo.

Nini kifanyike

Akizungumza kwa muktadha wa kisaikolojia, Mchungaji Daniel Sendoro anasema wanandoa wanapofikia hatua ya kuchokana, watu wanaowashauri na kuwapatanisha katika nyakati hizo wawashauri wanandoa hao kuweka akiba ya maneno.

“Unapogombana na mwenzako na kuropoka, kuna maneno unaweza kuropoka yakasababisha hata mshindwe kusameheana na kurudiana, hivyo kikubwa kwanza wanandoa wanapofikia hatua ya ugomvi, wajizuie kuropoka,” anasema Mchungaji Sendoro ambaye pia ni mtaalamu wa malezi na saikolojia.
Akigusia kiini cha baadhi kutoleana siri za ndani hadharani wanapogombana, amesema inasababishwa na kila mmoja kutokuwa amejiandaa kufikia mwisho mbaya na mwenzake.

“Huo mwisho ndiyo unawaathiri kiasi kwamba kila mmoja anatafuta kuonekana ni mwenye haki kuliko mwenzake katika hilo lililotokea.

Amesema kuna watu kwa kufanya hivyo huona ndiyo anapata unafuu, akieleza katika maisha ya ndoa kuna mambo mengine ni magumu hata kuyasema wanandoa wanakutana nayo.

“Mnapoachana, mmoja anakuwa anaona alijitolea kupita kiasi kwa mwenzake na bado ameachwa, hivyo kuamua kusema hovyo hovyo.

“Hata hivyo kwa muktadha wa kijamii, kutoleana siri huo ni ushamba na kukosa ustaarabu, ni ile hali ya mtu kutokuwa mstaarabu kwa sababu mwisho wa mambo maisha lazima yaendelee, haipaswi kuonyesha tabia ya hovyo kwa mwenzako.”
Amesema ndoa inapofikia hatua hiyo, wanandoa wanapaswa kwanza kuzingatia utu na kuweka mbele ustarabu.

“Watu wasaidiwe kwa amani, wasaidiwe kisaikolojia na kiushauri, ikionekana hapo walipofikia ndiyo mwisho, basi wapewe muda wa kujitafakari na kila mmoja apate nafasi ya kuwa peke yake.
“Wasiachane haraka haraka, hapana wapewe muda kwani kuna watu walitengana miaka 10 na kurudiana na kuishi pamoja kwa furaha na amani, isifikie hatua ya kutengana na kutoleana maneno makali,” amesema.

Historia ya wawili hawa

Baada ya uvumi wa siku kadhaa kuhusu uhusiano kati ya wawili hawa hatimaye Januari 19, 2024 walithibitisha hilo kwa Manara kumvisha Zaiylisa pete ya uchumba na kuutangazia umma kuhusu ndoa yao.

Katika tukio hilo, Manara alitoa ahadi kuwa hiyo ndiyo itakuwa ndoa ya mwisho kwake baada ya nyingine zaidi ya tatu kuvunjika, huenda nayo ikavunjika kutokana na kile kinachoendelea hivi sasa.

Zaiylisa pia aliahidi kumpenda na kumpa kila furaha anayostahili, akisema: “Ndoa zote nilikuwa nataka ziwe za mwisho, lakini binadamu tunapitia mitihani, katika hii naomba Mwenyezi Mungu anivushe iwe ndoa yangu ya mwisho.”

Januari 24, 2024 wakafunga ndoa iliyodumu kwa miezi 14 ambapo kwa mujibu wa waliyoyawekea wenyewe mitandaoni imefikia tamati Aprili 9, 2025

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *