Sakata la Trump na Zelensky lachukua sura mpya

Washington. Tukio la Rais wa Marekani Donald Trump kugombana hadharani na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kumewaibua viongozi wa dunia wakitamka kuiunga mkono Ukraine huku Umoja wa Ulaya ukisema ‘Ulimwengu huru unahitaji kiongozi mpya.’

Kauli ya Umoja wa Ulaya na matamko ya viongozi wengine wa dunia kuweka huruma kwa Zelensky baada ya juzi kushambuliwa kwenye ikulu ya ‘White House’ na Turmp huku akiungwa mkono na makamu wake JD Vance, kumewashitua wengi.

Trump alianza kuitikisa dunia kwa kusaini amri kadhaa za kiutendaji za rais ikiwamo kusitisha misaada kwa mataifa yanayoendelea ikiwamo Afrika, na hasa misaada ya dawa muhimu kama za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi.

Jana Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas alisema “ulimwengu huru unahitaji kiongozi mpya” baada ya Trump kugombana na Zelensky katika Ikulu ya White House juzi.

“Ni jukumu letu, Wazungu, kuchukua changamoto hii,” aliongeza katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii.

Pia, Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz alithibitisha msaada wake kwa Rais Zelensky baada ya kutokuelewana na Trump.

“Hatutakiwi kamwe kuchanganya mashambulizi na mwathirika katika vita hii mbaya,” aliandika Merz kwenye X.

Waziri Mkuu wa Canada, Melanie Joly alisema,” Ukraine inapigania uhuru wake, tunaamini katika kusaidia Ukraine. Tunaona Waukraine wanapigania uhuru wao na wetu,” alisema Joly.

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni alitaka kuitishwa mkutano kati ya Marekani, Ulaya na washirika wao kuhusu Ukraine, kufuatia mzozo kati ya Trump na Zelensky.

“Mkutano bila kuchelewa unahitajika kati ya Marekani, mataifa ya Ulaya na washirika wao ili kuzungumza kwa uwazi tutakavyokabiliana na changamoto kubwa za leo, kuanzia na Ukraine, ambayo tumeitetea pamoja kwa miaka ya hivi karibuni,” alisema Meloni.

Tofauti na wengine, Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban alimshukuru Trump kitendo cha juzi akisema alisimamia haki.

“Vijana imara huleta amani, dhaifu huleta vita. Trump alisimama kwa ujasiri kwa amani. Hata kama ilikuwa vigumu kwa wengi kuikubali. Asante, Mheshimiwa Rais,” alindika Orban kwenye chapisho la X.

Mataifa mengine yanayomuunga mkono Zelensky ni Ufaransa, Ujerumani, Poland, Hispania, Denmark, Uholanzi, Ureno, Jamhuri ya Czech, Norway, Finland, Kroatia, Estonia, Latvia, Slovenia, Ubelgiji, Lithuania, Luxembourg na Ireland. Viongozi wa Canada, Australia na New Zealand.

Pia, Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese alisisitiza msaada wa nchi yake kwa Ukraine.

“Tutaendelea kusimama na Ukraine kwa muda wote utakaohitajika,” alisema Albanese na kuongeza kuwa msaada kwa taifa la Ulaya linalokumbwa na vita ni masilahi kwa Australia.

“Tunasimama bila shaka na Ukraine katika mapambano yao, kwa sababu tunayaona kama mapambano ya kutetea sheria za kimataifa.”

Hii ni mapambano ya taifa la kidemokrasia dhidi ya utawala wa kidikteta unaoongozwa na Vladimir Putin, ambaye dhahiri ana malengo ya kifalme, si tu kwa Ukraine, bali katika eneo lote hilo,” alisema.

Ilivyokuwa Ikulu

Tukio la Rais Donald Trump kumshambuliana hadharani ndani ya Ikulu ya ‘White House” na rais mwenzake ambaye ni mgeni wake, halijawahi kutokea katika historia ya Marekani.

Ni tukio la aina yake ambapo Trump na makamu wake wa Rais JD Vance walimuweka ‘mtu kati’ Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky na kumpa maneno yake ikiwamo hataki amani kwenye nchi yake na kumshutumu kushiriki kampeni za Kamala Harris kwenye uchaguzi wa Marekani.

Taarifa zingine zinasema Zelensky alifukuzwa kutoka Ikulu na kuondoka akiwa na uso wa huzuni.

Mkutano huo uliofanyika juzi kwenye Ikulu ya Marekani ndani ya ofisi ya Rais Trump kusaini mkataba wa Marekani na Ukraine, uliohusisha upatikanaji wa mafuta, gesi na madini adimu ya Ukraine.

Hata hivyo, mkutano huo ulivunjika ndani ya dakika kumi baada ya kutokea vita vya maneno kati ya Trump, Zelensky na Makamu wa Marekani JD Vance walionekana kumbana Rais Zelensky asaini makubaliano ya kumaliza mapigano na Rais Vladimir Putin wa Russia.

Hali ya hewa ilichafuka baada ya Vance, aliyehudhuria mkutano huo pamoja na wanasiasa wengine, kumwambia Zelensky kwamba vita vinapaswa kumalizwa kwa njia ya diplomasia.

Ilionekana kama kuamsha hasira za Zelensky, aliyejibu kwa kuuliza, “diplomasia ya aina gani?”, akirejelea makubaliano ya kumaliza vita yaliyofikiwa mwaka 2019 ikiwa ni miaka mitatu kabla ya uvamizi wa Russia, na mengine mengi  lakini hayakutekelezwa na upande wa Russia.

Hata hivyo, Vance alikataa kujibu na kumtuhumu Zelensky kwa kukosa heshima na “kushughulikia” hali hiyo mbele ya vyombo vya habari.

Kutoka hapo, mjadala uliongezeka haraka, kwani Trump na Vance walimlaumu Rais wa Ukraine kwa kutoshukuru msaada wa Marekani wa miaka mitatu wakati wa vita dhidi ya Urusi, ambapo Trump alisema Zelensky hakuwa na nafasi ya kuwaambia Wamarekani jinsi wanavyopaswa kuhisi.

Pia, Vance alimkumbushia Rais Zelensky kwamba alienda Pennsylvania na kufanya kampeni kwa ajili ya upinzani Oktoba mwaka jana huku akimwambia; “Toa maneno ya shukrani kwa Marekani na Rais ambaye anajaribu kuokoa nchi yako,” alisema Vance.

Tuhuma za Vance kwa Zelenski ni kwamba alishiriki kufanya kampeni kwa ajili ya Makamu wa Rais wa zamani Kamala Harris katika mbio za urais za 2024 kwenye jimbo la Pennsylvania.

Septemba 2024 Zelensky alifanya ziara kwenye kiwanda cha silaha kilichopo Scranton, Pennsylvania, jimbo lenye ushindani mkali ambalo lilimpa Trump ushindi mdogo kwenye uchaguzi wa Novemba, 2024.

“Nilianza ziara yangu nchini Marekani kwa kutoa shukurani kwa wafanyakazi wote katika kiwanda hicho na kwa kufikia makubaliano ya kupanua ushirikiano kati ya Pennsylvania na Zaporizhzhia yetu,” Zelensky aliandika kwenye chapisho lake la X wakati huo.

Ingawa ziara hiyo haikutangazwa kama tukio la kampeni, wabunge wa Republican walidai kuwa ilikuwa ni kituo cha kampeni, wakisema kuwa si sahihi kwa kiongozi wa kigeni kuhudhuria tukio la kisiasa miezi michache kabla ya uchaguzi.

Rais wa Ukraine, Volorymyr Zelensky akiaga wakatiki akiondoka White House jana Februari 28, 2025.

Hii ilisababisha uchunguzi kutoka kwa wabunge wa Republican, iwapo kuonekana kwa Zelensky kulikuwa matumizi yasiyofaa ya fedha za walipa kodi.

Si hivyo tu, Trump alimwambia Zelensky kwamba msaada wa Marekani wa silaha na fedha ndio umempa nguvu ya kupigana na Russia, akiongeza kwamba bila msaada huo, asingekuwa na uwezo wa kudumu katika vita hata kwa miezi miwili.

Hata hivyo, Zelensky alijibu kwa kusema asingekuwa na uwezo wa kudumu hata kwa wiki mbili.

Majibizano yaliyochochewa na kauli ya Trump kwamba kama hawezi kusaini makubaliano ya kumaliza vita, aache, yalimfanya Zelensky kuamua kususa mkutano huo na kuondoka.

Mzozo wa Zelensky, Marekani

Si mara ya kwanza kwa Rais Zelensky kukwaruzana na Marekani. Neno ‘shukurani’ limeendelea kumgharimu, kiasi cha kutia doa uhusiano wake na Marekani.

Mara ya kwanza ilitokea Juni 2022, wakati Rais Joe Biden alimjia juu Zelensky kwenye mazungumzo ya simu baada ya kiongozi huyo kuomba msaada zaidi kutoka Marekani, akiorodhesha misaada aliyohitaji lakini haikutolewa.

Biden alikubali kutoa msaada mwingine wa kijeshi wa dola bilioni 1 kwa Ukraine, lakini wakati Zelensky akiorodhesha misaada ambayo haikutimizwa na Marekani, Biden alikasirika na kusema kwa sauti ya juu, akimtaka Zelensky kuonyesha shukurani kwa kile anachokipata kutoka Marekani.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao