Sakata la Master Jay, Alikiba liko hivi

Dar es Salaam. Mtayarishaji wa muziki nchini Joachim Marunda ‘Master Jay’ amesema ubanaji pua siyo tusi ni neno lililoanza kutumiwa na wasanii wa Hip-hop tangu mwaka 2000.

Master Jay amesema hayo wakati akizungumza na Mwananchi huku akiongezea kuwa hajawahi kubeza wala kudharau kipaji cha Alikiba.

“Kitu kinachotofautisha RnB na Bongo Fleva ni scale. Miziki inakuwaga na scale tofauti. Waimbaji wa RnB mara nyingi wanaimba ‘major’ na ‘miner’ kama vile nyimbo  za kanisani lakini Bongo Fleva wanaimba Arabic Scale.

“Uimbaji wa Bongo Fleva tangu zamani kina Dully Sykes walikuwa wanaimba kama vile wanabana pua, ndiyo maana wakapewa hilo jina. Hilo neno sijalitunga mimi lilitungwa na watu wa Hip-hop.

“Unajua zamani tulikuwa tu na Hip-hop, walivyokuja wa Bongo Fleva wakawa wanasema wabana pua. Ndiyo maana hata mimi juzi nikasema mtu fulani ni mbana pua kwamba yeye ni shoo ya Bongo Fleva yule mwingine ni Shoo ya RnB sasa watu hawajaelewa,” amesema Master Jay.

Master ameongezea kwa kusema kwa upande wa wasanii wa Bongo Fleva, Alikiba ndiyo Mtumbuizaji Bora Tanzania.

“Hiyo ni kwa Bongo Fleva lakini siyo kwa Bongo RnB. Kwenye hiyo Barnaba ni mkali kuliko Alikiba  ndiyo maana nikasema kwenye Bongo Fleva nampa yeye lakini tukianza kuweka kina Barnaba, Christian Bella Aslay inakuwa ni habari nyingine.

“Mtu kama Bien ni mtu wa band, ndiyo maana yeye wakati anaimba hakutumia nguvu ni kama anaongea. Kwa sababu anaijua na ni ngumu kwa wasanii wetu kushindana na Bien kwenye live. Na hata hapa Bongo ni ngumu wasanii wengi kushindana na Christian Bella. Watu wamechukulia kama nataka kumponda sasa mimi nitampondaje legendary,”amesema Master.

Mbali na hayo akifafanua namna ya uimbaji bora mwalimu wa Muziki kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Heri Kaare amesema kubana pua ni kulazimisha matamshi ya kutokea mdomoni yatokee puani.

“Mfumo wa uimbaji ni sawa na uongeaji, ili mtu aimbe kinachotokea ni hewa imeingia  kwenye mapafu. Hewa ili itoe sauti ni pale ambapo inatoka kwenye mapafu kurudi kwenye sehemu tunaita ‘vocal folds’. 

“‘Vocal folds’ inaweza kuruhusu hewa itoke au isitoke. Ili sauti iweze kutokea ni pale ambapo lazima hewa iliyopo kwenye mapafu ipande ipite kwenye ‘Vocal folds’ na huwa zinafunguka kwa kutetemeka.”

Amesema mtetemeko huo ndiyo huzalisha sauti huku akifafanua kuwa mbali na sauti ambayo huzalishwa huwa na maneno ambayo yanatokana na ulimi, kaa kaa gumu na laini, fizi za chini na fizi za juu, mdomo ya juu na chini pamoja na pua.

“Tunavyosema mtu anaimba kwa kubana pua ni kulazimisha hewa itoke ndivyo sivyo katika mtiririko usio wa kawaida.  Ni kweli wapo wanaoimba bila kuacha mfumo ufanye kazi kama unavyopaswa.

“Inatakiwa maneno ya kwenye pua yaende na mdomoni pia yaende sehemu yake. Sasa  kubana pua ni kulazimisha maneno yote yapitie puani hadi yale yasiyotakiwa kupitia puani. Uimbaji mzuri ni kila silabi itoke kulingana na vile inavyotakiwa kuitoka,”amesema. 

Hata hivyo, ameongezea kuwa kinachowaponza baadhi ya wasanii kushindwa kutumbuiza  moja kwa moja (Live Perfomance) ni kutokuwa na elimu ya muziki.

“Muziki pamoja ni sanaa lakini pia ni taaluma. Unasomewa kama masomo mengine tatizo kubwa ni kukataa kujua muziki ni taaluma. Watu wakikubalika mtaani wanadhani ni wanamuziki. Walio wengi siyo wanamuziki kwa sababu hawaujui.

“Wasanii wengi wanakimbia elimu wanataka umaarufu, tunashauri wasanii wapite shule wasome wengi hawawezi ‘live perfomance’ kwa sababu hawana taaluma ya muziki kwa hiyo akitakiwa kufuata vitu fulani anashindwa,”amesema.

Utakumbuka hayo yote yalitokea katika usiku wa fainali ya BSS 2025 baada ya Master  kuulizwa swali na moja ya chombo cha habari nchini kuwa wasanii gani wanauwezo mzuri wa kufanya live perfomance. Ndipo kwenye majibu yake alidai.

“Kwa wasanii wa Bongo hakuna anayeweza kuimba live japo sio wote, ndio maana marehemu Ruge alikuwa na THT hii ni kwa ajili ya kukuza vipaji, leo hii msanii aliyetoka THT
ukimwambia aimbe live anakimbiza, sio hawa wasanii wenu.