Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA aliwasili mjini Tehran Jumanne jioni ambapo amekutana na kuzungumza na viongozi husika wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Safari hiyo ambayo ni ya kwanza kufanywa na Grossi mjini Tehran baada ya kuundwa serikali ya 14 ya Iran inayoongozwa na Rais Masoud Pezeshkian, imefanyika siku chache kabla ya mkutano wa msimu wa Bodi ya Magavana ya wakala huo.
Safari ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki mjini Tehran na za maafisa wa masuala ya nishati ya nyuklia wa Iran katika makao makuu ya wakala huo mjini Vienna Austria au mikutano ya pande mbili inayofanyika pembezoni mwa vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, imekuwa ikijadili njia za kuondoa tofauti zilizopo kati ya wakala huo na Iran, baada ya Marekani kujiondoa kwenye Makubaliano ya Nyuklia ya Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA).
Katika muhula wa kwanza wa urais wake, Donald Trump alijiondoa katika mapatano ya JCPOA kwa uchochezi wa Wazayuni na Warepublican wenye itikadi kali mwaka 2018 kama sehemu ya siasa za mashinikizo ya juu zaidi ya nchi hiyo dhidi ya Iran. Trump na Warepublican wenye itikadi kali walidhani kwamba kupitia siasa hizo wangeweza kuidhoofisha Iran na hatimaye kuilazimisha ikubali matakwa yao ya kidhalimu yanayohudumia maslahi ya Wazayuni. Kwa mujibu wa ripoti 15 zilizotolewa na Yukio Amano, Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa wakala wa IAEA, wakati wa utekelezaji wa mapatano ya JCPOA na hata mwaka mmoja baada ya Trump kujitoa katika mapatano hayo, Iran ilitekeleza majukumu yake yote. Hata hivyo ikiwa ni katika radiamali yake ya kukabiliana na uvunjaji ahadi wa pande nyingine katika mapatano hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo ililazimika kusimamisha taratibu na katika hatua tano utekelezaji wa wajibu wake katika mapatano hayo.

Pamoja na hayo, utawala wa Kizayuni na waitifaki wake barani Ulaya na Marekani mara kwa mara wamekuwa wakijaribu kuonyesha kuwa mpango wa nyujlia wa Iran unaotekelezwa kwa malengo ya kiraia unafuatilia malengo ya kijeshi, ikiwa ni katika njama zao za kuchochea woga na chuki dhidi ya Iran. Kwa ajili hiyo wametumia vibaya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ili kufikia lengo lao hilo ovu. Kwa msingi huo, IAEA chini ya usimamizi wa Rafael Grossi mara nyingi umevuka nafasi yake ya kiufundi ya kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran, ambapo ripoti za mkurugenzi mkuu huyo kwa Bodi ya Magavana zimekuwa zikiathiriwa pakubwa kisiasa na lobi za Wazayuni na makundi yanayopinga Iran huko Ulaya na Marekani.
Hii ni katika hali ambayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikijaribu kuendeleza ushirikiano wake wa kiufundi na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ndani ya fremu ya makubaliano ya pande mbili.
Hivi sasa Rafael Grossi amesafiri Iran katika hali nyeti kikanda. Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba wako tayari kushirikiana na wakala huo kuhusiana na madai ya kuwepo urutubishaji wa kushukiwa wa madini ya urani katika baadhi ya maeneo ya Iran, katika fremu ya mkataba wa NPT. Iwapo mkurugenzi mkuu wa shirika hilo anataka kutatua kiufundi tu hitilafu zilizopo kati ya Iran na wakala huo na bila kubuni mafaili bandia kwa lengo la kuziridhisha lobi za mashinikizo za Wazayuni, ni wazi kuwa atapata ushirikiano wa kutosha kutoka Iran. Uzoefu unaonyesha kuwa wakati wowote ushirikiano wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na Iran unapofanyika kwenye misingi ya kiufundi chini ya wakala huo wa kimataifa na bila kuingizwa ndani masuala ya kisiasa, mazingira yanayofaa ya kufanyika mazungumzo kati ya Iran na kundi la 5+1 huandaliwa kirahisi.
Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Masuala ya Kisheria na Kimataifa na ambaye alikutana na Grossi mjini Vienna wiki mbili zilizopita amesema kuhusu safari hii kwamba: ‘Safari hii imefanyika katika muendelezo wa maingiliano kati ya Iran na wakala wa IAEA na pia kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya pande mbili hizi iliyotolewa tarehe 4 Machi 2023. Iran imeazimia kuendeleza ushirikiano na wakala huo isipokuwa tu iwapo baadhi ya nchi zenye nia ya kisiasa zitajaribu kuharibu juhudi za Mkurugenzi Mkuu na ushirikiano unaoendelea kuimarika kati ya Iran na wakala huo.