Wakuu wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameazimia mambo 10 ikiwemo kuamuru vikosi vya majeshi yaliyoko chini ya mpango wa walinda amani wa SAMIDRC, kuanza kuondoka kwa awamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uamuzi huo umefikiwa leo Alhamisi Machi 13, 2025, katika mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi na Serikali za SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao huku wapiganaji wa kundi la M23 wakidaiwa kuendeleza mapigano na Jeshi la DRC (FARDC).
Mbali na kuamuru kuondolewa kwa vikosi vyake kwa awamu nchini humo, SADC imempongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia amani na usalama wa kikanda ndani ya jumuiya hiyo.

“Mkutano huo umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ), kutokana na uongozi wake katika masuala ya amani na usalama ya kikanda,” imeeleza taarifa ya SADC.
Mkutano huo uliyoongozwa na Mwenyekiti wa SADC ambaye pia ni Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa umetoa rambirambi za dhati kwa DRC, Afrika Kusini, Malawi na Tanzania pamoja na familia za wanajeshi waliopoteza maisha chini ya SAMIDRC na kuwaombea majeruhi wapone haraka.
“Mkutano umeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya usalama Mashariki mwa DRC ikiwa ni pamoja na kutekwa kwa miji ya Goma na Bukavu, na kuzuiliwa kwa njia kuu za usambazaji, jambo linalokwamisha utoaji wa msaada wa kibinadamu.

“Mkutano umepongeza wanajeshi kwa kujitoa kwao mhanga, mshikamano, bidii na uvumilivu waliouonyesha tangu kuanza kwa ujumbe huo,” imesema taarifa hiyo.
SADC pia kupitia taarifa hiyo imependekeza mambo sita kufanyika nchini DRC ambayo ni wito wa kulindwa na kuhakikishwa uhuru wa raia wanaotafuta usalama na kuwataka wahusika wote kuheshimu misingi ya kimataifa ya kibinadamu, kusitisha mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia na kuhakikisha ufikishaji wa msaada wa kibinadamu bila vikwazo.
Pia imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU), kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu wa DRC.
SADC pia imesisitiza kujitolea kwake kushughulikia mzozo unaoendelea DRC na kuthibitisha dhamira yake ya kusaidia juhudi za kuleta amani na usalama wa kudumu Mashariki mwa DRC, kwa mujibu wa Mkataba wa SADC wa Ulinzi wa Pamoja wa mwaka 2003.
Pia imeahidi kuendelea kuiunga mkono DRC katika kulinda uhuru, mamlaka na uadilifu wa eneo lake pamoja na kuhakikisha amani, usalama na maendeleo endelevu.
Wakati huo, imesisitiza umuhimu wa suluhisho la kisiasa na kidiplomasia kwa wahusika wote, wakiwemo wa Serikali, wasio wa Serikali, washirika wa kijeshi na wasio wa kijeshi ili kurejesha amani na utulivu nchini humo.
Pia imerejelea uamuzi wa pamoja wa Mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC wa kuunganisha Mchakato wa Luanda na Nairobi na kujumuisha waratibu zaidi ili kuimarisha juhudi za ujenzi wa amani.
Mkutano huo ulipokea kwa furaha Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) linalotoa mwongozo wa suluhisho la kudumu, huku likiunga mkono juhudi za kikanda za AU, EAC, ECCAS, ICGLR, na SADC katika kuitisha mikutano ya ngazi ya juu na juhudi za upatanishi chini ya michakato ya Luanda na Nairobi, pamoja na juhudi za katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kurejesha amani na usalama Mashariki mwa DRC.
Pia, ilimpongeza Rais wa DRC, Félix Tshisekedi kwa uimara wake wa kuendelea kukabiliana na changamoto za usalama DRC.
Miongoni mwa wakuu wa nchi za SADC waliohudhuria mkutano huo kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Zimbabwe, Dk Emmerson Mnangagwa, Duma Boko (Botswana), Andry Rajoelina (Madagascar), Daniel Chapo (Msumbiji) na Nangolo Mbumba (Namibia).
Wengine ni Rais Samia Suluhu Hassan (Tanzania), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Hakainde Hichilema (Zambia), Ntsokoane Samuel Matekane (Lesotho).

Pia kuna Waziri Mkuu wa Eswatini, Russel Dlamini, Nancy Gladys Tembo, Waziri wa Mambo ya Nje (Malawi), Dhananjay Ramful, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Biashara ya Kimataifa (Mauritius), Manuel Homem, Waziri wa Mambo ya Ndani (Angola), na Claude Morel, Balozi Mkuu wa Afrika Kusini.