Sababu za Watanzania kuendelea kutapeliwa

Dar es Salaam. Licha ya vilio vya mara kwa mara, baadhi ya Watanzania wameendelea kulalamika kutapeliwa fedha zao na watu au taasisi zinazodai kuwatajirisha kupitia upatu ama miradi mbalimbali.

Kilio cha hivi karibuni ni cha wiki iliyopita ambapo baadhi ya wanachama wa Tanzania Community Empowernment Association (Tancea) waliibuka wakilalama kutapeliwa.

Wanachama hao walidai kupoteza mamilioni ya fedha walizokuwa wakichangishwa na taasisi hiyo tangu mwaka 2021, baada ya kuahidiwa kujengewa mabanda, kupewa vifaranga 1,000, vyakula na dawa za mifugo.

Hata hivyo, mambo hayo hayakutekelezwa, badala yake walichangishwa fedha kwa viwango tofauti ikiwemo kiingilio cha kati ya Sh6,000 hadi Sh27,000.

Pia baadhi walilipia bima za biashara hizo ambazo ni Sh250,000 kwa mtu mmoja, licha ya kuwa hadi sasa hakuna walichofaidika.

Kwa mujibu wa Sheria za Tanzania ni kosa kufanya biashara ya upatu. Kanuni ya adhabu Sura ya 16 inataja kuwa, 171A-(1) mtu anayeongoza au anasimamia mpango wa piramidi atakuwa ametenda kosa.

Madai hayo yanakuja wakati kukiwa na malalamiko kama hayo miaka nenda rudi. Mwaka 2018, Jeshi la Polisi lilipeleleza madai ya wanachama wapatao 150 wa kampuni Namaingo Business Agency iliyoanzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kutoa ushauri wa biashara na ujasiriamali ambayo iliwatapeli wanachama wake jumla ya Sh1.5 bilioni.

Wanachama hao walidai kutozwa Sh250,000 kwa ajili ya kujiunga, Sh20,000 kwa ajili ya mkataba, Sh76,000 kwa ajili ya kupatiwa bima ya afya, Sh45,000 bima ya biashara.

Michango mingine ni pamoja na Sh20,000 kwa ajili ya kukaguliwa, Sh50,000 mafunzo ya darasa la hesabu, Sh50,000 mafunzo ya kufuga samaki na Sh50,000 kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.

Madai mengine ya utapeli yaliibuka mwaka 2020, ambapo aliyekuwa Mkurugenzi wa kampuni ya Mr Kuku Farmer Ltd, Tariq Machibya maarufu Mr Kuku alilipa faini ya Sh5 milioni na kukwepa kifungo cha miaka mitano jela, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumhukumu kulipa fidia ya zaidi ya Sh5.4 bilioni baada ya kukiri mashtaka ya kushiriki katika upatu na kupokea miamala ya fedha kutoka kwa umma.

Katika hukumu hiyo, Mahakama iliagiza Sh5.4 bilioni ambazo zipo katika akaunti za mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali, ikitaka kiwango hicho cha fedha kuhamishiwa katika akaunti namba 9921169817 iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa jina la Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Kampuni nyingine zilizoibua malalamiko ni pamoja na Jatu PLC na Kalyinda. Suala la Jatu bado lipo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Tatizo nini?

Baadhi ya wataalamu wa uchumi wametaja tatizo la biashara kutokwenda kama ilivyopangwa, usimamizi mbovu na tamaa ya kupata utajiri ni sababu ya watu kuingia kwenye mtego wa kutapeliwa.

Hiyo ni kutokana na wao kuamini kuwa na uwezo wa kupata fedha nyingi ndani ya muda mfupi, jambo linalowafanya washindwe kujipa muda wa kusoma hata masharti ya mkataba.

Profesa wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo anasema Serikali inapaswa kuwa na usimamizi madhubuti wa kumlinda Mtanzania wa kawaida, kwani kampuni inapoanzishwa na kutangazwa hadharani watu hudhani ipo kwa mujibu wa sheria.

“Mtanzania akiona kampuni imesajiliwa au inajitangaza kwenye mitandao ya kijamii anaona si uongo kwa sababu mwizi hawezi kujitangaza. Mtu anajiuliza kuwa kama ni waongo kwa nini Serikali haisemi chochote au kutoa onyo? Mwisho anajikuta anaamini iko sawa,” anasema Profesa Kinyondo.

Anasema wakati mwingine shida walizonazo wananchi na wanapokuwa katika hali ya ukosefu wa ajira au biashara kutokwenda vizuri inakuwa rahisi kuingia katika mambo yanayokaribiana na kamari, wakiamini ndiyo njia pekee ya kufanikiwa.

“Umaskini unamfanya mtu aamini katika njia za mkato itatokea miujiza, kukosekana kwa fursa na ajira ni moja ya sababu,” anasema Profesa Kinyondo.

Mtaalamu mwingine wa uchumi kutoka chuo hicho, Dk Thobias Swai anasema shida kubwa ni watu kudhani hela inakuja kwa haraka, jambo ambalo linafanya waamini katika faida za haraka.

Anatolea mfano wa watu kutokuwa tayari kuwekeza katika mifumo ambayo huwapa asilimia 15, 10 au 5 ya uwekezaji walioufanya kwa kuona ni kiasi kidogo na kukimbilia katika sehemu ambazo faida inatajwa kuwa asilimia 40 au 50.

“Wakati mwingine haya hufanyika yakihusisha watu wenye majina bila wao kujua, mtu akialikwa akazungumza kwenye shughuli hiyo watu wanaamini ni kweli na watu wanawekeza kupitia wao kuwapo katika eneo hilo,” anasema Dk Swai.

Anasema wakati mwingine kutodhibitiwa kwa taarifa zinazokwenda kwa umma ni moja ya jambo linalofanya watu wengi kuendelea kupoteza fedha, kwani baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikifanya promosheni ya vitu ambavyo hufanya watu kuamini kuwa ni kweli.

“Tatizo lingine ni watu kukosa uelewa katika shughuli za uwekezaji, kwa sababu hela haiji kwa urahisi kwa sababu hata uchumi haukui kwa urahisi hivyo, wajaribu kusoma na kuelewa sheria za uwekezaji,” anasema Dk Swai.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi anasema kuendelea kuwapo kwa vitendo hivvyo ni ishara wananchi wana uhitaji wa kuwekeza fedha zao mahali ili wapate faida.

Anasema Taifa linapaswa kuendeshwa na kanuni na sheria mbalimbali, lakini ni vema vyombo mbalimbali vinavyosimamia sheria hizo kuweka utaratibu wa kusajili kampuni na kuziweka wazi ili watu wajue sehemu gani zinatambulika kisheria kabla ya kuweka fedha zao ili wasije kuambulia patupu.

“Walipaswa kusajili na kuweka hadharani zile zinazotambulika kwa kuzitangaza mitandaoni au katika vyombo vya habari kwa sababu mwisho wa siku watu wanaamini wanaofanya biashara kwa uwazi katika mitandao ya kijamii kuwa wametambuliwa kiserikali, ndiyo maana hawajifichi,” anasema Dk Lawi.

Mchambuzi mwingine wa uchumi na biashara, Oscar Mkude anasema kujirudia kwa hali hiyo kunatokana na watu kuamini kuna njia ya mkato kufikia mfanikio.

“Ukiona mtu anakwambia kuwa biashara hii hakuna kukosa ni kufanikiwa tu, lazima ujiulize mara mbili, kwenye biashara mtu anapaswa kujua kuwa kuna kukosa na kupata,” anasema Mkude.

Anasema kwa kawaida kama biashara zote zingekuwa hazina hasara kila mtu angekuwa ameshaifanya, jambo ambalo ni ngumu kutokea kutokana na kuwapo na kupanda na kushuka.

Pia kukosekana kwa ujuzi wa kuhoji baadhi ya mambo yanayohusu masuala ya uwekezaji ni moja ya jambo linalofanya mtu kushindwa kujua athari anazoweza kupata baadaye.

“Kwenye masuala ya uwekezaji watu wanakuwa tayari kuuliza maswali ili kujihakikishia katika kile wanachokifanya, lakini wakati mwingine tunaweza kuwa hatuna elimu ya uwekezaji na tunatumia ujuzi wa elimu ya uwekezaji ya mababu zetu ambayo kwa sasa haizai matunda,” anasema Mkude.

Pia tabia ya watu kushindwa kutenga muda wa kutaka kulielewa suala hilo vizuri ni moja ya jambo linawafanya watu kuendelea kupigwa fedha zao.

“Kama unataka kufanya biashara ya bodaboda, unakwenda kukopa jipe muda wa kupiga hesabu na kuelewa jambo hilo vizuri, wakati mwingine unaweza kuona marejesho yako unaweza kulipa mara mbili ya fedha ambayo ungetumia kununua pikipiki moja, kwa nini usijipe muda kupiga hesabu kuona hali halisi?” anahoji Mkude.

Simulizi za waathirika

Mmoja wa waliowahi kupoteza fedha zao katika kampuni hizo, Francisca Msellem anasema siku alipoambiwa mkurugenzi wa kampuni aliyokuwa amewekeza fedha zake amefikishwa mahakamani alihisi kuchanganyikiwa.

“Mara ya kwanza kulikuwa na mvutano kwenye kundi la wawekezaji (waliokuwa wameweka fedha kwenye kampuni hiyo) watu hawajalipwa miezi miwili uongozi unapiga kalenda kesho, kesho kutwa sasa ilipofika mahakamani nilikuwa na matokeo chanya na hasi,” anasema.

Anasema mara zote alipokuwa akiwaza alidhani itakuwa ni njia rahisi ya wao kupata fedha zao kupitia amri ya mahakama, lakini wakati mwingine alihisi vitaibuka vitu ambavyo hakutarajia.

“Matokeo yake sikupata chochote, Sh12 milioni zilikwenda na maji, sikuwahi kupata hata shilingi na hapo ndiyo nilipata vidonda vya tumbo,” anasema Francisca.

Maumivu hayo hayaishii tu kwa walioweka fedha zao, bali pia kwa baadhi ya waliowahi kuwa wafanyakazi wa kampuni hizo wamebaki katika majuto.

Hiyo ni kutokana na baadhi ya ndugu kuamini kuwa sehemu wanazofanya kazi ni salama na kuamua kuweka fedha zao na hali ilipogeuka kila mtu aliwaona ni matapeli.

“Nilipokuwa nafanya kazi niliwaaminisha ndugu zangu wengi kuwa watapata fedha zao, karibu kila mtu aliyenizunguka aliweka fedha zake, kampuni ilipokufa nilionekana tapeli, ndugu wakanitenga na kuonekana sina maana,” anasema kijana huyo.

Hali hiyo ilimfanya kuhamisha makazi yake kutoka Dar es Salaam kwenda mkoa mwingine ili akae mbali na familia huenda watamsamehe kuliko kumuona kila siku.

Mbali naye, Laurian Mwenda alitengwa na ndugu kwa kudhani fedha alizowadhamini kuwekeza katika moja ya kampuni alishalipwa faida yake na ameila tofauti na kile anachowaambia kuwa kampuni ilifilisiwa.

“Siaminiwi, hakuna anayeniamini, siku hizi nikisikia hizi kampuni nahuzunika kwa sababu hakuna uhalisia wowote, natamani watu waamke waelewe ni uongo lakini ni ngumu kumshawishi mtu aliyeaminishwa kuwa atapata faida,” anasema Mwenda.

Nini kifanyike?

Profesa Kinyondo anasema moja ya kitu kinachopaswa kufanyika ni kuhakikisha kuna sheria zinazosimamia suala hilo na kutoa uelewa kwa wananchi ili wasiwe watu wanaoingia katika mitego ileile kila siku.

“Fomula zilizotumika ni zilezile kasoro majina tu, sheria zisimamiwe na watu wajengewe uelewa kuwa hata kama una shida na unahitaji vitu, mtu akikuambia ukitoa Sh10 unapata Sh100,000 usihadaike,” anasema Profesa Kinyondo.

Katika hilo, Dk Lawi anasema wananchi wanahitaji elimu ya uwekezaji kwa ujumla, kwani wakati mwingine kukosekana kwa elimu kunafanya wananchi kuendelea kuumizwa.

“Tunayo mifuko ya uwekezaji kama UTT (Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji) ipo na inafanya vizuri na watu wengi wamewekeza kule, ikiwemo watumishi wa serikali, nafikiri ni wakati sasa wa kuendelea kufanya ubunifu zaidi ili iwepo mifuko kama hii na kutoa fursa kwa watu wanaotaka kuwekeza,” anasema Dk Lawi.

Kwa upande wa Mkude, anasema ni wakati sasa wa kuhakikisha sheria inazidi kuzibana biashara hizo ili kuweka urahisi katika ufuatiliaji kuanzia katika utendaji na hata watu kufikia taarifa hizo.

“Kama taasisi zimesajiliwa na kufahamika katika mifumo ya kiserikali inakuwa rahisi kufuatiliwa, lakini baadhi wamekuwa wanaficha taarifa sasa ili kuwadhibiti lazima mteja apewe taarifa kikamilifu kwa kila kitu kinachohusu kampuni ili awe na haki ya kukataa,” anasema Mkude.

Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Aurelia Kamuzora anasema bado kuna pengo halijazibwa vizuri linalotumiwa na watu wanaofanya shughuli hizo.

“Mfumo bado una tobo haujawa thabiti, hivyo ni vyema kutafuta mifumo ya kuzuia upigaji huo ili kubaini wenye nia mbaya na kuwadhibiti,” anasema Profesa Kamuzora.