Sababu za kusalia imara Kambi ya Muqawama: “Imani na kutawakali kwa Mola Muumba”

Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika Makala ya Wiki ambayo leo inazungumzia kwa ufupi sababu za kuendelea kuimarika Kambi ya Muqawama na mapambano dhidi ya dhulma na Uonevu.

Kambi ya Muqawama wa Kiislamu kwa miaka kadhaa sasa imeundwa katika eneo la Asia Magharibi na inapambana na dhulma, uvamizi  na vitendo vya kujitanua vya madola ya kiistikbari ya kikanda na kimataifa hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Awali, wanachama wa kambi hii ya Muqawama dhidi ya dhulma hawakuwa na nguvu waliyonayo sasa kijeshi na kisiasa, lakini wamekuwa wakifuata kanuni thabiti na imara, ambayo ndiyo siri ya maendeleo yake ya kuendelea kuwa imara na ngangari. Hapana shaka kwamba, sababu muhimu zaidi ya kuendelea kuwa imara, kustawi na mafanikio ya Mhimili wa Muqawama ni itikadi yao kwa Mwenyezi Mungu na matukufu ya kidini ya wapiganaji Mujahidina wa Muqawama, ambayo imeimarisha imani yao kwa Allah na msaada wake dhidi ya maadui. Kigezo na mfano wa kivitendo wa imani hii ni ushindi wa Mtume Muhammad (SAW) katika vita na maadui, ambapo alipata ushindi mkubwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu licha ya suhula na zana chache alizokuwanazo. Katika Surah Al-Imran, Aya ya 123, tunasoma kuhusu Vita vya Badr, ambapo Waislamu waliokuwa wachache kwa idadi, lakini wenye imani thabiti, walilishinda jeshi la washirikina waliokuwa wamejizatiti kwa silaha na wakiwa wengi kwa idadi.  Aya hiyo inasema: Hakika Mwenyezi Mungu aliwanusuru katika Vita vya Badr hali nyinyi ni wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru. 

Katika zama hizi, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hasa namna, mbinu na jinsi wapiganaji wa Iran walivyopambana na jeshi vamizi la Saddam yanaweza kutambuliwa kuwa mwanzo wa kuundika Muqawama wa Kiislamu katika eneo la Magharibi mwa Asia.  

Mujahidina shupavu na  waliokuwa na ikhlasi hususan vikosi vya wapiganaji wa kujitolea vya wananchi, Basij, walikuwa na imani  ya hali ya juu na kumtegemea Mwenyezi Mungu barabara, na walipata ari na nguvu ya kustaajabisha ya kukabiliana na adui kutokana na ibada, kumtaradhia Mola na kutawasali kwa Mtume na Aali zake watoharifu. 

Japokuwa kwa sasa Mhimili wa Muqawama unatambua kupambana dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani kuwa ndiyo wadhifa wake muhimu zaidi, lakini katika uga mpana zaidi, vita hivi vinatathmini  katika fremu ya vita vya siku zote vya haki dhidi ya batili ambapo Mwenyezi Mungu ameahidi kuwa hatimaye haki itashinda. Hata hivyo Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anabainisha masharti ya ushindi huo mkubwa akisema: “Popote pale panapotokea mpambano kama huu baina ya haki na batili, ushindi utakuwa upande wa kambi ya haki lakini kwa masharti kwamba watu wanaopigania haki wawe na nia na irada thabiti, uvumilivu, subira wasimame kidete na  kupambana;  hapana shaka kuwa wakati huu wataibuka na ushindi.” Wapiganaji shupavu na wachaMungu wa Kambi ya Muqawama wameonyesha kuwa, wamekamilisha masharti ya kupata ushindi kambi ya haki dhidi ya batili, na kwa sababu hii wanashinda katika medani ya Jihadi dhidi ya maadui wa Mwenyezi Mungu na watu, kama vile Marekani na utawala wa Israel. Watu kama hawa ndio wanaokusudiwa katika ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenye Aya ya 30 ya suratu Fussilat inayosema: “Hakika wale ambao wamesema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu; Kisha wakawa na msimamo, huwateremkia Malaika (kuwaambia): Msiwe na hofu, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu , Ayatullah Ali Khamenei 

Tunapozungumzia mapambano ya Mujahidina shupavu wa Muqawama dhidi ya dhulma na ukandamizaji tunaona kuwa silaha yao muhimu na kubwa zaidi dhidi ya  zana za kijeshi za kisasa za adui ni kuwa na imani na msaada wa Mwenyezi Mungu na kutawakali kwake. Ndio maana wapiganaji wa Kambi ya Muqawama wanaziona silaha na zana za kijeshi kuwa wasila na wenzo tu wa istiqama na mapambano katika njia ya kufika kwenye malengo yaliyoanishwa na Mwenyezi Mungu. Si hayo tu, bali hata wanakunasibisha na Mwenyezi Mungu kulenga kwao shabaha, kama inavyosema Aya ya 17 ya Suratul Anfal kwamba: Hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewauwa. Na hukutupa wewe ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa… 

Kwa sababu ya imani hii, wapiganaji wa Kambi ya Muqawama hutaja jina la Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume na Ahlibaiti zake wakati wanapotumia silaha kama makombora, ndege zisizo na rubani na kadhalika katika medani na uwanja wa vita.   

Hisia ya kuridhiwa na Mwenyezi Mungu ya wapiganaji wa Muqawama na matumaini ya kupata usaidizi wake huwapa moyo Mujahidina ambao huwa tayari kusabilia uhai wao kwa urahisi katika kupambana na uvamizi na jinai za maadui. Mapambano haya, kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, huwa na mojawapo ya hatima mbili zenye fakhari, ama kupata ushindi na kufikia lengo lao takatifu, au kuuawa shahidi katika njia ya Allah na kupigania haki, ambacho ni kifo chenye hadhi na uokovu kwa kila Muislamu ambacho Mtume wa Rehma amekitaja kuwa ndiyo kifo bora zaidi. 

Ukweli huu unadhihirika wazi katika vita vya sasa vya wapiganaji wa Kambi ya Muqawama dhidi ya vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mujahidina wa Hamas katika Ukanda wa Gaza na Hizbullah kwenye mpaka wa Lebanon wanaingia vitani kwa ujasiri dhidi ya askari wa Kizayuni walioingiwa na hofu na kuharibu vifaru vyao vya Merkava, ambavyo Wazayuni walitambua kuwa haviwezi kushindwa. Wakati huo huo vikosi vya Muqawama vya Iran, Lebanon, Iraq, Yemen, na kwengineko vinalenga maeneo nyeti ya Israel kulipiza kisasi cha unyama na mauaji ya kimbari ya utawala huo unaosaidiwa kwa hali na mali na madola ya kibeberu kama Marekani na washirika wake.

Wanamuqawama wa Palestina 

Kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa itikadi na imani ya Kambi ya Muqawama kwa msaada wa Mwenyezi Mungu vinaiweka katika hali ya kuyalazimisha majeshi ya Marekani kuondoka katika eneo la Asia Magharibi na kuuweka utawala wa Kizayuni kwenye hatihati ya kuporomoka. Hali hii ni ina maana ya kutimia ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo imetajwa katika Aya ya 7 ya Suratu Muhammad (SAW) ikisema: “Enyi mlioamini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithabitisha miguu yenu.