Sababu za kupanda kwa bei ya samaki, dagaa Mbeya

Kyela. Imeelezwa kuwa ongezeko la kina cha maji katika mwambao wa Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya ndicho chanzo cha mfumuko wa bei ya samaki na dagaa katika kipindi cha miaka miwili sasa.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo, Jumatatu, Machi 31, 2025, baadhi ya wavuvi katika mwalo wa Mtaa wa Forodha, eneo la Matema, wamesema msimu huu hali ni mbaya na imeathiri uchumi wao.

Mvuvi, Festo Wille, amesema kipindi hiki kuna ongezeko kubwa la maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mara kwa mara, hali ambayo imesababisha upatikanaji wa samaki na dagaa kuwa mgumu.

“Unajua vitoweo hivyo (samaki) vina tabia ya kutoishi kwenye maji mengi, hukimbilia maeneo ya mbali yenye kina kifupi. Katika Ziwa Nyasa, hupendelea kukimbilia upande wa nchi jirani ya Malawi,” amesema.

Amesema changamoto hiyo imesababisha kuadimika kwa samaki maarufu aina ya mbasa sambamba na dagaa na kuuzwa kwa bei ya juu tofauti na miaka ya nyuma.

“Kwa miaka ya nyuma, msimu huu endapo mvua si nyingi, bei ya dagaa kwa plastiki la kilo 20 tunauza kwa Sh10,000 mpaka 15,000, lakini sasa imepaa na kufikia Sh40,000 mpaka 45,000 kwa ujazo huo,” amesema.

Amesema samaki aina ya mbasa, ambao kwa miaka ya nyuma walikuwa wakiuzwa kati ya Sh5,000 mpaka 10,000, kwa sasa bei imepaa na kuuzwa kati ya Sh30,000 na 35,000 kulingana na ukubwa.

“Mabadiliko ya tabianchi nayo yamechangia, hususani utulivu wa maji ziwani na kukosekana kwa mawimbi makubwa, ambayo yakiwepo husaidia kusukuma samaki kwenda maeneo ya kina kifupi,” amesema.

Naye mvuvi Seleman Julius amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa zana za kisasa za uvuvi kwa ajili ya kutega samaki kwenye maeneo yenye kina kirefu.

“Shida ni zana za uvuvi. Wengi wetu tunatumia uvuvi wa kizamani kwa kutumia mitumbwi, hivyo tunaomba Serikali kutushika mkono, ili kutoathiri shughuli za kiuchumi zitokanazo na uvuvi,” amesema.

Amesema suala hilo linapaswa kupewa kipaumbele ikizingatiwa kuwa Ziwa Nyasa ni tegemeo kwa kitoweo cha samaki watamu, hivyo kuna kila sababu ya wavuvi kujengewa uwezo na kuwezeshwa ili kuchangia mapato ya Serikali.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Matema, mwambao mwa Ziwa Nyasa, Wilaya ya Kyela, Emmanuel Zachalia, amesema msimu huu kumekuwa na hali ngumu katika eneo la uvuvi kufuatia changamoto ya maji kujaa, hali inayosababisha samaki kupatikana maeneo ya mbali.

“Kimsingi, wavuvi walio wengi hutumia mitumbwi kutega samaki, tofauti na wavuvi wengine wanaotumia boti kuzifuata maeneo ya mbali ambako samaki hukimbilia,” amesema.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni mwenendo wa ziwa kwa miezi hii kutokuwa na mawimbi makubwa, ambayo husaidia kusukuma samaki kufika maeneo ya jirani ambako wavuvi wanaweza kuwafikia kwa urahisi.

“Ombi kwa Serikali na wadau ni kusaidia nyenzo bora za uvuvi ili kuwasaidia vijana wanaoishi kwa kutegemea shughuli za uvuvi kujikwamua kiuchumi, kwani uhaba wa samaki umepelekea kuathiri maisha na kukwama kuwapeleka watoto shule,” amesema Emmanuel.

Naye mchuuzi wa dagaa wa kukaanga katika Mtaa wa Forodha, Matema, Aisha Joel, amesema kwa sasa upatikanaji wake si rahisi, na wakifika ni lazima upambane ili kuwapata.

“Miaka miwili sasa hali ya upatikanaji wa vitoweo katika Ziwa Nyasa si rafiki, ambapo kwa sasa kipimo ambacho awali tulikuwa tukiuza kwa Sh500 tunauza kwa Sh1,000 mpaka 1,500,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *