
Dar es Salaam. Ndoa ni muungano wa maisha kati ya wanandoa unaotarajiwa kudumu kwa muda mrefu, mara nyingi hadi kufikia uzeeni.
Pamoja na agano hilo kufungwa kwa mujibu wa taratibu za kidini au kiserikali, huambatana na desturi na mila tofauti zinazoakisi urithi wa kijamii.
Moja ya desturi zinazotajwa mara kwa mara ni kitendo cha wanandoa wapya kukanyagana miguu siku ya harusi.
Katika baadhi ya jamii, inaaminika kuwa yule anayeweza kumkanyaga mwenzake kwanza atakuwa na mamlaka makubwa katika ndoa.
Kwa wengine, ni ishara ya upendo na mshikamano kati ya wanandoa, ikionyesha mshikamano wa kimwili na kiroho katika maisha yao mapya.
Akizungumza na Mwananchi, Amina Abdallah amesema aliambiwa na bibi yake kuwa afiche miguu yake wakati mume wake atakapomshika kichwa kwa ajili ya kusoma dua, bila kumwambia ina maana gani.
“Baadaye katika kufuatilia ili nijue tafsiri ya kitendo hicho, niliambiwa kuwa atakayewahi kumkanyaga mwenzake ndiye atakayekuwa juu ya mwenzake, ”amesema.
Nyasatu Ngaya amesema ni kama desturi tu ambayo baadhi ya watu wanaifanya, wakiamini atakayewahi kumkanyaga mwenzake ndiye atakayekuwa mtawala katika maisha yao ya ndoa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa tovuti ya Turkiye, chimbuko la desturi hiyo ni nchi za Uarabuni.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, utaratibu huo umekuwa ukifanywa katika harusi zinazofanyika katika jamii mbalimbali ikiwa ni ishara ya kitamaduni inayoashiria nguvu katika ndoa.
“Inaaminika kwamba yule anayekanyaga kwanza atakuwa na mamlaka katika maisha yao ya ndoa, huku ikichukuliwa kama utani wa kugombea madaraka kati ya wanandoa,”imeeleza tovuti hiyo.
Akizungumza na Mwananchi, Sheikh Yakub Ndembo amesema amekuwa akisikia utamaduni huo ukitekeleźwa katika baadhi ya ndoa na wengine kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha, huwa wanahusianisha kitendo hicho na dini.
Amesema katika upande wa dini ya Kiislamu utamaduni huo haupo katika mambo yanayopaswa kufanyika siku ya ndoa.
“Miongoni mwa taratibu muhimu zinazosisitizwa baada ya kufungwa kwa ndoa, ni wanandoa kuomba dua, kuswali rakaa mbili pamoja na kunyweshana maziwa. Hayo ya kukanyagana miguu hayapo katika dini, “anasema.