Sababu wahitimu vyuo vya kati kupata ajira zaidi

Dar es Salaam. Robo tatu ya waajiriwa wapya wanaochaguliwa kujaza nafasi katika sekta mbalimbali hawana elimu ya chuo kikuu, inaeleza ripoti ya utafiti wa ajira na mapato katika sekta rasmi Tanzania ya mwaka 2022/2023.

Ripoti inabainisha asilimia 22.3 ya wahitimu wa vyuo vikuu ndio waliopata nafasi ya kuajiriwa katika sekta rasmi, huku nyingine zikijazwa na wahitimu wa vyuo vya kati, ufundi, shule za sekondari, msingi na wasiokuwa na elimu.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni, katika kipindi husika ambacho tafiti ilifanyika waajiriwa wapya walikuwa 132,966 ambao kati yao 103,312 walikuwa hawana elimu ya chuo kikuu.

Ripoti ya utafiti inaeleza kati ya waajiriwa wote, 55,579 walikuwa wahitimu wa vyuo vya kati, huku 8,110 wakiwa wa vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

Waliokuwa na elimu ya sekondari na msingi walikuwa 38,959, huku wasiokuwa na elimu kabisa wakiwa 664.

Utafiti unaonyesha asilimia 57.12 ya waajiriwa walikuwa wanaume, huku wanawake wakibeba kiwango kilichosalia.

Ripoti inabainisha kati ya watu 132,966 walioajiriwa, 56,224 walikuwa na mikataba ya moja kwa moja, 25,980 (mikataba ya kazi maalumu), 46,742 (mikataba ya muda maalumu) na 4,020 (mikataba ya kazi za muda mfupi).

Maoni ya wadau

Akizungumza na Mwananchi Februari 25, 2025 kuhusu utafiti huo, mtaalamu wa uchumi, Kennedy Rwehumbiza amesema watu wanaotoka vyuo vya kati na vya ufundi mara nyingi huwa wanakidhi mahitaji ya soko kutokana na gharama za kuwafundisha kutohitajika kwa kiasi kikubwa.

Pia watu hao mishahara wanayotegemea si mikubwa ikilinganishwa na wale wanaotoka vyuo vikuu, huku kazi zilizopo zikiwa hazihitaji sana watu wa shahada.

“Gharama ya matarajio kwenye mishahara hawa wa vyuo vya kati na ufundi ni ndogo kuliko wanaotoka vyuo vikuu watakuambia bila Sh1.2 milioni au Sh2 milioni siendi,” amesema Rwehumbiza aliyewahi kuwa Meneja wa Programu wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Amesema mara nyingi wahitimu wa kati wanakuja na ujuzi unaowawezesha kuanza kazi moja kwa  moja jambo ambalo linaleta tija mapema, huku kwa upande wa vyuo vikuu hilo likipatikana kwa mtu mmoja kati ya 10.

“Kwa upande wa tabia, hawa wa vyuo vya kati wana hasira ya kazi, utayari wa kujifunza na kutaka kuelewa vitu, hawa wengine wanaona wamesoma,” amesema.

Amesema hali hiyo inaweka ugumu hasa baada ya kazi nyingi kuhitaji utendaji zaidi wakati ambao watu wenye shahada ni kada ya utendaji ambao nafasi zao ni chache.

“Sekta binafsi mara nyingi inahitaji wazalishaji zaidi ndiyo maana vyuo vya kati na Veta wanapata nafasi,” amesema Rwehumbiza.

Mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu, Lugano Bwenda amesema mara nyingi kila nafasi ya kazi huwa na sifa zake, nyingi zikiwa zile za utendaji watu wa stashahada ni bora kuliko wa shahada.

Amesema watu wa shahada mara nyingi wanapoajiriwa huwa wamepata nafasi ya wao kuwa wasimamizi badala ya kutaka kujifunza kazi.

“Wakati mwingine anakuja hajui kazi na wewe ulikuwa na mtu wa diploma ambaye amekaa kwa miaka minne au mitano umempa nafasi ya kusimamia, huyu wa shahada akija akajua hili haridhiki anaona yaani niwe chini ya mtu wa diploma,” amesema.

Mtazamo kielimu

Mdau wa elimu, Alistidia Kamugisha, amesema katika dunia ya sasa wahitimu wa ngazi isiyokuwa ya vyuo vikuu wanahitajika zaidi katika kusukuma maendeleo ya nchi mbele.

Amesema kwa kulitambua hilo, nchi ya China iliamua kuwekeza katika ngazi hizo za elimu, ikiwemo ufundi kwa kuweka miundombinu ya kutosha vikiwamo vyuo kuanzia ngazi ya vijiji hadi chini na matokeo yake yanaonekana.

“Hii ndiyo sababu hata sisi sasa tumeamua kufanya mabadiliko kwa kutambua umuhimu wa ngazi hii ya elimu kwa sababu kuna kazi nyingi ambazo kada ya kati inaweza kufanya. Ndiyo maana Serikali imeamua kuweka Veta karibu kila eneo na kuanzisha mfuko wa kusaidia hawa vijana katika kada ambazo zimechaguliwa,” amesema.

Amesema kuwapo mfuko huo ni kutaka kusaidia vijana kuingia katika uzalishaji moja kwa moja baada ya kuhitimu.

“Hivyo si kwamba watu hawa wanaajiriwa kwa sababu ya kulipwa ujira kidogo ikilinganishwa na wale wa vyuo vikuu lakini kuhitajika kwao sokoni ndiyo sababu,” amesema.

Mdau mwingine wa elimu, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla amesema: “Kama uhitaji wao (wa vyuo vikuu) sokoni ni mdogo basi wachukuliwe wachache wanaoweza kuajiriwa baada ya kumaliza vyuo, wengine waende vyuo vya kati ambako fursa nyingi zinapatikana,” amesema.

Mgalla amesema kwa kawaida Serikali ina utaratibu wa kutoa mafunzo kwa vijana kwa ngazi mbalimbali, akieleza anayekwenda ngazi za juu anapata elimu ya juu zaidi tofauti na aliyehitimu chuo cha kati na kidato cha nne.

Amesema muhitimu wa elimu ya juu anakuwa na maarifa zaidi ndiyo maana hata katika ajira mishahara na malipo yanatofautiana. Ametoa mfano mtu mwenye Shahada ya Uzamivu (PhD) anakuwa na mshahara mkubwa kuliko Shahada ya Uzamili (masters).

“Hata yule mtu wa masters mshahara wake huwezi kuulinganisha na mtu mwenye shahada ya kwanza na mtu wa shahada ya kwanza hawezi kulingana na astashahada au stashahada. “Lakini mwalimu wa stashahada mwenye miaka 10 kazini hawezi kufanana mshahara na yule wa shahada anayeanza ajira kwani atakuwa amepata ongezeko la mshahara kila mwaka,” amesema.

Amesema ni wakati sasa wa kuendelea kuwapa mafunzo kuwawezesha kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.

Mgalla amesema Serikali kwa kutambua mahitaji yaliyopo sokoni iliamua kufanya mapitio ya mtalaa na kuongeza masomo ya amali ili kuwaandaa wanafunzi vyema katika soko la ajira.

Tayari baadhi ya shule zinatumia mtalaa wa amali ambao unatoa fursa ya wanafunzi kujifunza stadi mbalimbali kama upishi, uchomeleaji na upakaji rangi.