Sababu wageni kupewa maeneo ya kuchimba gesi, mafuta

Dar es Salaam. Matumizi ya gharama kubwa katika kuchimba visima vya gesi imetajwa kuwa sababu ya Serikali kunadi vitalu vyake, ili kuita wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali.

Wawekezaji hao wanapopewa maeneo hufanya shughuli zao kupitia utaratibu wa mikataba ya kugawana mapato (PSA) ambayo huingiwa kati ya Serikali, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni za kimataifa za nishati (IECs).

Hayo yamesemwa wakati ambao Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) imeendelea na maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu 26 vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia ambapo kwa mara ya mwisho lilifanyika mwaka 2013.

Akizungumza na wanahabari leo Mei 19, 2025, Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Charles Sangweni amesema Serikali imeamua kunadi vitalu hivyo kwa kutambua umuhimu wake kwa ustawi wa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.

Amesema wanatumia njia ya kuita wawekezaji katika sekta hiyo kwani inahitaji fedha nyingi huku akitolea mfano wa kuchimba kisima kimoja nchi kavu gharama yake ni takriban dola 20 milioni za Marekani (Sh 53.82 bilioni) huku kisima cha baharini gharama yake ikiwa ni dola za 80 milioni za Marekani (Sh216.4 bilioni).

“Na kuna wakati baharini tulichimba kwa dola milioni 175 (Sh 473.38 bilioni) na hatukupata kitu. Mpaka sasa Tanzania tumeshachimba visima 96 na 44 kati yake ndiyo tulipata gesi 52 tulitoka patupu,”

“Unaweza kuona ni ngumu kiasi gani kwa Mtanzania kumuambia aweke dola milioni 20 za Marekani (Sh 53.82 bilioni) au TPDC halafu akute kavu wakienda bungeni watagawanya fedha zilizotumika kwa idadi ya zahanati ambazo wangeweza kujenga,” amesema.

Amesema jambo hilo ndiyo sababu ya kuziachia kampuni kuhusika na utafutaji kwa sababu baadhi yao wanazo sehemu za kufidia, huku akifafanua zaidi kuwa huenda wamewekeza maeneo mengine kama Uarabuni.

“Na kampuni zilizowekeza huko unakuta labda walichimba Uarabuni ambapo wakati huo uchumi ulikuwa unaonyesha mafuta yatauzwa labda kwa lita Sh300 watarejesha fedha lakini hadi kufikia wakati wanaogundua wanakuta bei imefika Sh600, ile fedha ya ziada wanaweza kuleta huku waendelee na ugunduzi,” amesema Sangweni.

Kwa mujibu wa mikataba ya PSA, mwekezaji hutumia fedha zake katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia, ambapo akikosa huwa anarudisha eneo kwa Serikali na kuondoka.

Lakini, akipata mafuta au gesi asilia fedha zipatikanazo baada ya mauzo ya rasilimali iliyopatikana hulipa mrabaha, hurudisha mtaji aliowekeza, hulipa kodi na tozo mbalimbali na kinachobaki hugawiwa kwa wabia wa mkataba ikiwemo Serikali na TPDC.

Akizungumzia sababu ya vitalu hivyo kutopata wateja tangu viliponadiwa kwa mara ya mwisho mwaka 2013, Sangweni amesema baada ya kutangazwa kwake, mwaka 2014 bei ya mafuta ilishuka kutoka dola 100 hadi dola 30 kwa pipa.

“Hali hiyo ilifanya wawekezaji wakakosekana, pia ujio wa sheria mpya ulileta mkanganyiko hasa walipotaka kufanyiwa mapitio. Ila kupitia hili waliimarisha miundombinu yao ya kisheria na kiusimamizi kwani moja ya malalamiko ya wawekezaji kuwa TPDC ni mdau katika utafutaji, na ndiyo msimamizi ndiyo maana Pura ikaanzishwa kama chombo huru,” amesema.

Wakati wa uongozi wa awamu ya tano kwa mujibu wa Sangweni kulitolewa maagizo ya kutaka kufanywa mapitio ya mikataba ya kugawana mapato (PSA) kwani iliyokuwapo ilidaiwa kuwa haikuingiwa vizuri.

Hali hiyo ilifanya Bunge kuridhia kufanywa mapitio hayo hivyo mwanasheria mkuu alipewa kazi lakini ilipofika awamu ya sita waliamua kubadilisha muundo na waliendelea na kazi kwa sababu dunia inahama, huku wakihofia kuwa utafika wakati gesi itakuwa kama makaa ya mawe.

“Tuliamua twende kwa kasi tuitoe gesi tuitumie hata kikanda tupate thamani ya kile tulichonacho hata dunia ikihama tuwe tumeshahama,” amesema Sangweni.

Hata hivyo, hayo yote yanafanyika huku wakiangalia yaliyokwamisha hilo kufanikiwa kwa wakati ule, wanaboresha ikiwemo mabadiliko ya kisheria yaliyotokea kwa wakati huo.

Akieleza faida za kunadiwa vitalu hivyo, Sangweni amesema utafutaji wa mafuta na gesi asilia huongeza uwekezaji katika sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini, jambo ambalo litachochea ugunduzi na uzalishaji wa bidhaa hizo nchini.

“Itasaidia kukua kwa uchumi wa nchi kutokana na mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi asilia, kuwezesha upatikanaji wa data za petroli utakaoongeza wigo wa taarifa zitakazosaidia katika kuchochea utafutaji zaidi wa mafuta na gesi asilia nchini,” amesema Sangweni na kuongeza

“Pia itatoa fursa za ajira kwa Watanzania na matumizi ya bidhaa na huduma kutoka kwa wafanya biashara na watoa huduma wa Kitanzania,” amesema.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mwakilishi wa msemaji wa Serikali, Revocastus Kassimba aliishukuru Pura kwa kukubali kuja mbele ya vyombo vya habari kwani wameonyesha kwa vitendo kile kilichofanywa na Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *