Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema Serikali itaendelea kutumia mfumo wa Mahakama Mtandao kuwawezesha wafungwa na mahabusu kusikiliza mashauri yao wakiwa magerezani, hususan wakati wa viashiria vya matishio ya usalama, ili kulinda amani na mali za wananchi.

Akizungumza leo Aprili 30, 2025 jijini Dodoma wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) katika Gereza la Isanga, Bashungwa amesema mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usalama na utoaji haki kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
“Jeshi la Polisi linapopata taarifa za kiintelijensia kuhusu uwezekano wa fujo, kama ilivyotokea hivi karibuni kutokana na matamko ya baadhi ya viongozi wa Chadema, linaweza kushirikiana na Mahakama kuendesha kesi kwa njia ya Mahakama Mtandao. Hili linasaidia kudhibiti machafuko mitaani na bado haki inatolewa,” amesema Bashungwa.
Amesema baadhi ya matamko ya kisiasa yamekuwa na viashiria vya kuvuruga amani, na kwamba ni jukumu la vyombo vya dola kuhakikisha hali ya utulivu inaendelea kutawala nchini.
“Niendelee kuliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha sheria inazingatiwa. Hata yule ambaye hataki amani, sisi tutamlazimisha kwa mujibu wa sheria kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama,” amesema.

Katika ziara hiyo, Kamati hiyo ya Bunge ilikagua makasha ya kisasa ya Mahakama Mtandao yaliyopo Gereza la Isanga, ambayo yanawawezesha mahabusu na wafungwa kusikiliza mashauri yao bila kutoka gerezani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Vita Kawawa, amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji haki kwa kutumia teknolojia, akisema hatua hiyo ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.