Sababu uzinduzi kituo cha gesi UDSM kupigwa kalenda

Dar es Salaam. Uzinduzi wa kituo cha kujaza gesi kwenye vyombo vya moto eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilichopangwa kuzinduliwa leo, Jumatatu, Februari 3, 2025 umeahirishwa kwa mara nyingine.

Meneja Msimamizi wa mradi wa CNG Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Aristides Katto akizungumza na Mwananchi leo amesema kuahirishwa huko kutokana na mambo yanayokamilishwa na mkandarasi.

Katto amesema kinachoendelea sasa ni uwekaji wa mazingira salama kwa ajili ya kupitisha gesi asilia.

“Tutatoa tarehe nyingine baada ya kukamilisha asilimia chache zilizobaki, kuna vitu vichache vinakamilishwa na mkandarasi vinavyohusu usalama wa kituo,” amesema Katto alipoulizwa na Mwananchi.

Ahadi hizo zinaendelea wakati watumiaji wa gesi kwenye vyombo vya moto wakiendelea kupitia changamoto kutumia zaidi nusu siku hadi siku nzima kupata nishati hiyo.

Kituo hicho kinachomilikiwa TPDC, kipo barabara ya Sam Nujoma, UDSM kilianza kujengwa kutokana na mkataba uliosainiwa Mei 20, 2024. Mkataba huo ni baina ya TPDC na kampuni ya Sinoma East Africa Company ikishirikiana na kampuni ya kimataifa ya Sinoma makubaliano ujenzi miezi minane, yaani kukamilika Desemba 2024.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio alipotembelea kukagua ujenzi wa kituo hicho Julai 18, 2024 aliagiza kituo kikamilike Desemba 2024 kama ilivyopangwa.

“Januari 16, tutaanza majaribio   na yatafanyika kwa wiki mbili na mwishoni mwa Januari, gari la kwanza litaanza kujazwa gesi kwenye kituo hiki, kazi inafanyika hapa kwa saa 24, eneo la karakana ya kubadili mifumo ya gari kutumia gesi nayo imefikia asilimia 90,” alisema.

Kauli kama hiyo ilitolewa pia Agosti 21, 2024 na Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue alipotembelea kituo hicho na kuahidi kitakamilika Desemba.

Baada ya Desemba, Januari 6, 2025, Dk Mataragio alirudi tena kufanya ukaguzi wa kituo hicho na kuahidiwa kingeanza majaribio Januari 16.

Sababu zilizowekwa bayana kutokamilika kwa kituo hicho kwa wakati, ni kuchelewa kufika Tanzania kwa meli iliyobeba mitambo ya ujenzi wa kituo husika.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TPDC, Derick Moshi akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea mradi huo Januari 25, alieleza sababu ya kutokamailika kwa mradi huo kwa wakati.

Alisema utekelezaji wa mkataba wa ujenzi wa kituo hicho ni kwa muda wa miezi minane na ulipangwa kukamilika Desemba 2024.

 “Changamoto ya mvua kubwa za mwaka jana zilisababisha eneo hii kujaa maji mengi kutokea sehemu za miinuko ya chuo kikuu cha UDSM na kuathiri uondoshaji wa udongo wa juu na kujaza mawe na kifusi kipya cha kokoto,” alisema.

Ukiwa ni mwendelezo wa kutembelea kituo hicho, Januari 9, 2025 Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko alitembelea kituo hicho na kutangaza kitaanza kufanya kazi Februari 3, mwaka huu akisema ameridhishwa na kazi ya ujenzi.

Changamoto hiyo inachochewa na uchache wa vituo vilivyopo, kwani mpaka sasa kuna vituo vinne vinavyotoa huduma ya kujaza gesi kwenye magari katika maeneo ya Ubungo Maziwa, Tabata TOT, eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Tazara.

Uwezo wa kituo

Januari 25 mwaka huu, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TPDC, Moshi alisema kituo hicho kikikamilika watatoa huduma ya gesi kwa vyombo vya moto tofauti.

 “Kituo kitahudumia magari manane kwa wakati mmoja na kwa siku kitatoa huduma kwa magari 1,200, kituo kitakuwa na pampu za kujaza malori matatu ya kupeleka gesi kwenye vituo vidogo na viwandani,”alisema.