Sababu upatikanaji wa dola sasa kutosumbua

Dar es Salaam. Hali ya upatikanaji wa dola nchini imeimarika kwa kiasi kikubwa katika wiki chache zilizopita wakati nchi ikiongeza mapato ya fedha za kigeni kutokana na kuongezeka kwa mapato kutoka kwenye utalii, dhahabu na mauzo ya nje.

Hali imekuwa nzuri kiasi kwamba Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Paul Makanza   wakati wa tuzo za Rais za Mtengenezaji Bora wa Mwaka (PMAYA) wiki iliyopita kuwa, amesema nchi haikabiliwi tena na uhaba wa dola.

“Sasa hivi hakuna anayezungumza kuhusu uhaba wa dola, kwa sababu zinapatikana kwa urahisi,” amesema.

Akizungumzia kauli hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, alithibitisha kwa gazeti dada la The Citizen leo Jumatatu Novemba 11 2024 kuwa, kweli kumekuwa na maboresho makubwa katika upatikanaji wa fedha za kigeni nchini katika wiki chache zilizopita.

“Upatikanaji wa dola nchini umeongezeka kutokana na kuongezeka mauzo ya nje, hasa bidhaa za kilimo. Tumeshuhudia minada inayoendelea kwa korosho, ufuta na kunde,” amesema.

Ameongeza kuwa,  kuongezeka kwa bei na kiasi cha dhahabu duniani kumechangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania, hivyo kuongeza thamani ya dola.

Aidha, amebainisha kuwa msimu wa watalii mwaka huu umeleta idadi kubwa ya wageni Zanzibar, wakati kuanzishwa kwa Reli ya Kisasa (SGR) kukirahisisha watalii kutembelea maeneo kama Mikumi na Kilosa.

Kwa mujibu wa taarifa ya mapitio ya uchumi ya kila mwezi (MER) ya BoT ya Oktoba 2024, akiba ya fedha za kigeni ya Tanzania ilifikia dola bilioni 5.414, Septemba 2024.

Fedha hizo, kwa mujibu wa BoT, zilitosha kugharamia miezi 4.4 ya makadirio ya uagizaji wa bidhaa na huduma, kiwango ambacho ni juu ya kiwango cha kitaifa ambazo ni miezi 4.

Hii inaashiria kuwa, akiba ya fedha za kigeni imeimarika kwa takriban asilimia 11 katika mwaka uliopita.

Septemba 2023, akiba ya fedha za kigeni ya Tanzania ilikuwa ni Dola  4.88 bilioni.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania inakua katika mauzo yake yote nje, huku mauzo ya jadi yakiongezeka hadi Dola  1.073bilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2024, kutoka Dola 853.8 milioni mwaka uliotangulia.

Hii ilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya nje ya tumbaku na korosho. Kwa kuwa, biashara ya korosho ya mwaka huu ilianza wiki saba zilizopita baada ya MER ya hivi karibuni ya BoT kuandaliwa, wachambuzi wana matumaini kuwa kiwango kitaonyesha kuimarika zaidi.

Aidha, takwimu zilizotolewa Mtwara mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, zinaonyesha kuwa msimu wa 2024/2025 ulianza kwa mafanikio na sasa uko katika wiki yake ya saba.

Amesema mwishoni mwa wiki kuwa, wakulima wa korosho wamepata jumla ya Sh879.699 bilioni katika kipindi cha wiki saba zilizopita, kutokana na mazingira bora ya biashara, ambayo ni pamoja na kuteuliwa kwa Bandari ya Mtwara kama lango la mauzo ya nje ya zao hilo.

Kwa upande wa mauzo yasiyo ya jadi, katika mwaka ulioishia Septemba 2024, mauzo ya nje yaliongezeka hadi Dola 6.8bilioni, ikilinganishwa na Dola  6.3 bilioni kwa mujibu wa takwimu za BoT.

Ongezeko hilo lilichangiwa na mauzo ya dhahabu, madini hayo yalileta takriban Dola 3.26 bilioni kutoka Dola  2.98bilioni mwaka uliotangulia. Mauzo ya bidhaa za kilimo cha bustani yaliongezeka hadi Dola 484 milioni kutoka Dola 378milioni  mwaka uliopita.

Pamoja na ongezeko kubwa la idadi ya watalii, mapato ya huduma ya Tanzania yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 18 kufikia Dola  6.98 bilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2024, kutoka Dola 5.89 bilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2023.

Mapato kutoka utalii, kwa mujibu wa BoT, yaliongezeka hadi Dola3.82 bilioni  katika mwaka ulioishia Septemba 2024 kutoka Dola  3.15bilioni katika mwaka ulioishia Septemba 2023.

“Ufanisi huu umechangiwa na ongezeko la idadi ya watalii, ambao wameongezeka kwa asilimia 21.2 hadi kufikia wageni 2,068,856, sababu zikiwa ni juhudi za Serikali na sekta binafsi katika kukuza Tanzania kama kivutio cha watalii,” inaeleza ripoti ya BoT.

Wachambuzi wana mtazamo kwamba kutokana na msimu wa utalii, siku za usoni zinaweza kuwa za kufurahisha.

Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Abel Kinyondo alisema msimu wa watalii umechangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa dola nchini.

Hata hivyo, alikuwa na mtazamo kuwa juhudi zinapaswa kufanywa kuhakikisha maeneo mengi zaidi ya vivutio yanatengenezwa ili kuhakikisha watalii wanakuja mwaka mzima.

Mapato ya usafirishaji, hasa kutoka ada za mizigo, yaliongezeka hadi Dola 2.57 bilioni  katika mwaka ulioishia Septemba 2024, kutoka Dola 2.27 bilioni katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Hii inahusishwa zaidi na uboreshaji unaoendelea wa shughuli za bandari na miundombinu ya usafiri.

Kwa uboreshaji unaoendelea katika bandari kuu za Tanzania, wachambuzi wanaamini kuwa, mambo yataendelea kuimarika.

Rais wa Chama cha Mawakala wa Usafirishaji Mizigo Tanzania (Taffa), Edward Urio  amesema upatikanaji wa dola nchini umeharakisha mchakato wa kutoa mizigo bandarini.

“Hapo awali, mawakala walikuwa wakitafuta dola ili kufanya malipo kabla ya mizigo kutolewa. Sasa, baadhi ya ada kama ada za kuhifadhi mizigo na ada za usafirishaji, ambazo hulipwa kwa dola zimeondoka,” amesema.

Changamoto ya upatikanaji wa dola nchini ilianza mwanzoni mwa mwaka jana, Mei 2023, Serikali ilikiri suala hilo, ikielezea uhaba huo kutokana na nakisi ya biashara ya nje ambayo ilifikia Dola  5.4 bilionimwaka 2022.

Sababu kadhaa zilitajwa kuchangia nakisi hiyo, ikiwa ni pamoja na athari za janga la Uviko-19, kuongezeka kwa gharama za uagizaji bidhaa kutokana na mgogoro wa Urusi na Ukraine, na mahitaji makubwa ya Dola kwa ajili ya miradi mikubwa ya kitaifa kama vile SGR na Mradi wa Umeme wa Maji wa Mwalimu Nyerere.