Sababu ugonjwa wa ukoma kupungua nchini

Dar es Salaam. Takwimu za wagonjwa wapya wa ukoma hapa nchini Tanzania zinaonyesha ugonjwa huo kupungua kwa kasi ukilinganisha na miaka ya nyuma.

 Kwa mujibu wa Wizara ya Afya kiwango cha  wagonjwa wapya kimepungua kutoka wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,263 mwaka 2024 sawa na punguzo la asilimia 45.

Idadi hiyo ni punguzo kutoka wagonjwa 1,309 mwaka 2023 ambayo ilikuwa ni sawa na punguzo la asilimia 57.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 26,2025 Mratibu wa Ulaghbishi, Mawasiliano na Uhamasishaji wa Wizara ya Afya. Juma Said amesema, “kwa tafsiri hii, mwaka 2024 nchi yetu ilikuwa na wagonjwa wawili katika kila watu 100,000,  hii inaiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizofikia kiwango kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) cha kutokomeza ugonjwa wa ukoma,  yaani kuwa chini ya mgonjwa mmoja kati ya watu 10,000.”

Hata hivyo, pamoja na jitihada hizo amesema bado kuna halmashauri 10 katika mikoa ya Morogoro, Lindi,  Mtwara, Ruvuma, Shinyanga na Tanga ambazo hazijafikia viwango vya utokomezaji, huku juhudi zikiendelea.

Ukoma ni nini?

Ukoma ni ugonjwa sugu unaosababishwa na vimelea vya bakteria waitwao Mycobacterium leprae, wanaoshambulia mishipa ya fahamu. Maambukizi ya ukoma ni kwa njia ya hewa kupitia majimaji kutoka mfumo wa upumuaji wa mtu mwenye maambukizi akipiga chafya au kukohoa.

Ugonjwa huu hauambukizwi kwa kugusana au kushikana mikono dalili zake ni vijinundu kwenye ngozi, mabaka mwilini yenye rangi ya shaba yasiyo na hisia, mishipa ya fahamu kuvimba pamoja na ganzi kwenye mikono na miguu.

Ugonjwa huu unaweza kusababisha ulemavu wa kudumu ikiwa ni pamoja na vidonda sugu mikononi     na miguuni, kukakamaa viungo, kuharibu sura ya mtu, kukatika viungo na upofu.

Njia pekee ya kujikinga dhidi ya madhara ni kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na utambuzi wa mapema wa dalili zake, ili kupata matibabu. Ugonjwa huu unatibika iwapo mgonjwa atagundulika mapema, atapata matibabu ya dawa na kupona kabisa.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, daktari mstaafu aliyehudumu eneo hilo kwa muda mrefu, Lucas Maricha amesema ugonjwa wa ukoma zamani ulikuwa unaonekana kama ugonjwa tishio kwa namna ulivyokuwa unamuathiri mwanadamu.

Anasema ugonjwa huo unamuathiri mtu yeyote ingawa wanaoweza kuambukizwa ni watu wanaokaa na mgonjwa mwenye wadudu wengi kwa kipindi kirefu na anayeambukizwa ni yule mwenye kinga ya mwili ndogo.

“Ugonjwa huu unaathiri ngozi na mishipa ya fahamu, mtu anapata uvimbe kwenye masikio macho na kwenye ngozi. Mabaka yasiyokuwa na mguso ambayo hayamfanyi mgonjwa kusikia maumivu,” amebanisha.

Amesema mgonjwa wa ukoma akiwahi kupata matibabu anapona kabisa lakini akichelewa anapata madhara ikiwemo vidonda na vidole kusinyaa.

“Ukoma hauui ila kinachoua ni yale madhara yake kwa mgonjwa mfano amepata vidonda anaweza akaingiliwa na vidudu, watu hawa pia lishe yao sio nzuri, kunyanyapaliwa kwa hiyo hata msongo wa mawazo tu unaweza ukasababisha mtu akafa,” amesema.

Dk Maricha amesema hadi mgonjwa kuonyesha dalili tangu kupata wadudu inaweza ikachukua miaka 20 hadi 30.

Amesema ugonjwa huu unaenda unapungua kutokana na juhudi za wizara ya afya kwani programu ya kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma iliyoanza tangu mwaka 1977 ilisaidia kutoa elimu na matibabu.

“Wagonjwa kwa hapa kwetu ni wachache sana kila wilaya na mkoa kuna mratibu ambaye anashughulikia mgonjwa mpya akijitokeza,” amesema.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kuwatibu wenye dalili lengo ikiwa kuutokomeza kabisa.

Aidha, kupitia waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, kushirikiana na vituo vyote vya kutolea. huduma za afya nchini kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa ugonjwa wa ukoma katika kaya zote zenye wagonjwa wapya na kutoa tiba.

Katika maadhimisho ya ugonjwa huo mwaka huu kauli mbiu ni,“Tokomeza, Pinga Unyanyapaa na Imarisha ustawi wa Afya ya Akili” dhidi ya Ukoma.