
MABOSI wa Yanga inaelezwa jana waliitana na kujifungia ili kujadili hukumu ya kesi waliyoifungua Mahakama wa Kimataifa ya Usuluhishi ya Michezo (CAS), iliyotupiliwa mbali, huku zikitajwa sababu tatu zilizosababisha kesi kufutwa na ushauri waliopewa mabosi hao wa Jangwani.
Yanga ilikimbilia CAS baada ya mechi ya Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba kuahirishwa saa chache kabla ya kufanyika Machi 8, mwaka huu, ikidai kanuni za ligi zilikiukwa kimakusudi ili kuinufaisha Simba iliyotangaza isingecheza kwa kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho Kwa Mkapa na mabaunsa wanaodaiwa kuwa wa Yanga. Hata hivyo, juzi hukumu ya kesi hiyo ilisambaa mtandaoni ikielezwa imefutwa na Bodi ya Ligi kutoa taarifa kuwa ilikuwa ikijianda kutoa ratiba mpya ya pambano hilo na mengine yaliyobaki ya ligi iliyosaliwa na raundi tatu kabla ya kufikia tamati. Mapema jana asubuhi ilielezwa mabosi wa Yanga waliitana ili kujadili na walikuwa wakijiandaa kutoa taarifa ya klabu, lakini mwanasheria na mwandishi mzoefu wa habari za michezo, Wakili Alloyce Komba aliyewahi kuwa wakili wa Yanga enzi za Yusuf Manji ametaja sababu tatu za kesi hiyo kufutwa na kwamba kila kitu kimeshaisha na Yanga iendelee na mambo mengine tu kwa sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Komba alisema kesi ya Yanga haipo kwa sababu kuu tatu ambazo alizitaja kuwa ni CAS imekosa mamlaka ya kusimamia kesi hiyo, kukosa hukumu iliyoifanya Yanga kukimbilia CAS na kushindwa kukamilisha mchakato kwa kufuata utaratibu.