Zanzibar. Mwanamuziki wa Singeli nchini Baba Kash, amesema muziki huo umekuwa ukipokea mitazamo ya kuwa wa kihuni kutokana na chimbuko lake.
Akizungumza na Mwananchi, msanii huyo leo Februari 16,2025 amesema licha ya mitazamo hiyo kwa sasa muziki huo umebadilika tofauti na ulivyokuwa awali.
“Muziki wa Singeli asili yake umetokea uswahilini. Baadhi ya waliokuwa wanafanya walikuwa hawana maadili mazuri. Mwanzoni muziki ulikuwa ukisikiliza mzuri lakini ukienda kwenye shoo zao kuna vitu vingi vya ajabu vinatokea, kama vile wizi lakini kwa sasa imebadilika haipo tena,” amesema msanii huyo.

Msanii huyo ambaye ni mara yake ya kwanza kupanda kwenye Jukwaa la Sauti za Busara,
amesema ili muziki huo uvuke mipaka unahitaji ubunifu zaidi na uwekezaji zaidi.
“Mimi mwanzoni nilikuwa naimba na Dj, lakini nikaona hapana. Nikaanza kutengeneza ladha ya Singeli, Mchiriku na Mnanda kwa pamoja nikiwa napiga bendi. Nimefanikiwa katika hilo ndiyo maana nimepata nafasi ya kutumbuiza Sauti za Busara 2025,”amesema.
Licha ya hayo amesema msanii mzuri ni yule, anayeweza kuimba kwenye bendi, kwani wengi wao hubebwa na studio.
“Live bendi kwa msanii ni muhimu sana kwa sababu ukiona hajiwezi kufanya hivyo ujue siyo muimbaji. Mimi pia ni prodyuza naona wasanii tunavyosumbuana studio. Unakuta mtu anarudia sana hadi kupata kitu kizuri,” amesema Baba Kash.
Hata hivyo, amemalizia kwa kusema, bado watu wengi hawaamini kwenye muziki huo, kwani hakuna nguvu kubwa inayowekwa kama ilivyo kwenye aina nyingine ya muziki.