Sababu Mkuchika kutogombea tena ubunge Newala Mjini

Dar es Salaam. Mbunge wa Newala Mjini (CCM), George Mkuchika ameeleza sababu za kutogombea tena ubunge katika jimbo hilo kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ikiwamo ya uzee.

Mkuchika ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), aliwaeleza hayo wananchi jimboni kwake, jana, Machi 22, 2025.

Kabla ya kuzungumza na wananchi hao, Mkuchika alitoa tangazo hilo kwa mara ya kwanza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Newala.

Mkuchika ambaye amekuwa mbunge kwa miaka 20, ameshika nafasi mbalimbali serikalini kama mtumishi wa umma na mwanasiasa, hivyo ameona sasa ni wakati wake wa kustaafu kwa kuwa muda wake umekwisha.

“Kwenye mkutano ule (halmashauri kuu ya wilaya), nimetangaza kuwa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mwaka huu, sitagombea, japo watu hawakutaka kusikia tangazo hilo, lakini wakati ni ukuta, ukishindana nao wala hufanikiwi.

“Kwa hiyo, ndugu zangu, wengine vijana, wananifahamu nimeshazeeka,” amesema Mkuchika wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.

Akielezea uzoefu wake, amesema mwaka huu anatimiza mwaka wa 52 katika utumishi wa umma, ambapo alimaliza chuo kikuu mwaka 1973 na kufanya kazi na chama cha Tanu na CCM kwa miaka 10.

Amesema mwaka 1983, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alimteua kuwa mkuu wa wilaya na alipoondoka akaingia hayati Ali Hassan Mwinyi ambaye alikaa naye miaka 10 yote ya uongozi wake.

“Akaingia Rais Mkapa (Benjamin), nikafanya ukuu wa wilaya kwa miaka miwili, akanipandisha cheo kuwa mkuu wa mkoa, kwa hiyo ukuu wa wilaya, mimi nimefanya miaka 14,” ameeleza mbunge huyo.

Ilipofika mwaka 2005, amesema aliitwa na wazee wa Newala akiwemo Mzee Nangwanda Sijaona wakati alipokwenda likizo, na kumwambia wanatafuta mbunge katika jimbo la Newala wa kuwaletea maendeleo.

“Tumeangalia tukanona wewe kazi hii unaiweza, kutokana na kuaminiwa na Nyerere, Mwinyi na Mkapa mpaka Kikwete, acha ukuu wa mkoa na uje nyumbani,”aliambiwa na wazee hao.

Amesema aliamua kuacha ukuu wa mkoa na kwenda kuwa mbunge licha ya kuwa maruprupu ya mkuu wa mkoa ni makubwa zaidi kuliko ya mbunge.

Amesema aliamua kufanya hivyo kwa kuwa Mzee Sijaona ni kati ya wazee walioiletea heshima nchi hii, hivyo asingeweza kumkatalia ombi lake.

Ameeleza kuwa wakati nchi ipo katika mapambano ya kudai uhuru, Mwalimu Nyerere alipofika kwa mara ya kwanza Newala alilala kwa mzee huyo.

Wakizungumzia hatua hio, wachambuzi wa siasa, Dk Conrad Masabo, amesema kuna mambo mawili katika hilo moja ikiwemo hilo la kudai kutaka kupumzika ukizingatia ni umri wake umeenda kidogo.

“Kwa hiyo kutokana na umri alionao anaona mikiki ya siasa haiwezi ukizingatia pia siasa imeingia mambo tofauti,  ambapo kwa waliofanya siasa halisi wanaweza wasiendane nayo.

“Kwa mfano zamani haya mambo ya machawa hayakuwepo, kwa hiyo kwa mtu aliyefanya siasa halisi za CCM, lazima za sasa hivi zimuudhi,” amesema mchambuzi huyo.

Jingine, Dk Masabo amesema ni kutoendana na mtazamo wa kisiasa wa sasa kwani waliofanya kazi na CCM ikiwa chama kimoja na chama tawala, kulikuwa na namna ya  chama kujitathimini na kujiendesha jambo ambalo sasa hivi hali hiyo imepotea.

“Kwa hiyo, sasa hivi mambo yanafanywa ilimradi chama kinashinda au kinabaki madarakani bila hata kujiuliza mnafanya nini, nadhani kuna siasa zimeibuka Tanzania za ushabiki bila sababu ya msingi, ambazo huenda zinamuwia ngumu yeye kuziishi,” ameeleza msomi huyo.

Akizungumzia uamuzi wa Mkuchika kuachana na ubunge, mchambuzi wa masuala ya siasa na kijamii, Dk Richard Mbunda amesema Mkuchika ni amana kubwa kwa chama na Serikali.

Hata hivyo, Dk Mbunda amesema hatua alizochukua mbunge huyo ni jambo jema ukizingatia wakati ni ukuta na yeye ameshaona umri umempiga mkono.

“Inafikia kipindi inabidi upishe damu changa iingie kwenye siasa, alichokifanya mbunge huyo na waziri ni jambo jema kwani katika mambo haya ya siasa sio mpaka usubiri ushindwe, yaani mtu aje akushinde, wapigakura wako waje waanze kuona kwamba hauna tena ushawishi au pengine nguvu zimeisha.

“Hivyo, kikawaida tunategemea viongozi wenye busara waamue wenyewe kwamba muda umefika nang’atuka na inakuwa ni heshima kubwa kisiasa.

“Isitoshe Mkuchika ni mfuasi wa Baba wa Taifa, hivyo anaonyesha kuwa ikifika muda inatakiwa tu ung’atuke ili upishe damu changa iendelee na mapambano ya utumishi wa nchi,” amesema Dk Mbunda

Mchambuzi huyo amesisitiza kuwa ili upate kuheshimika katika uongozi ni lazima uwe na kiasi kwa kuwa watu wanahitaji mawazo mapya na anaamini akiingia kijana Newala Mjini, anaweza kuleta mabadiliko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *